Breaking News

Dk. Magufuli geukia ‘jipu’ la bomba la Dar –Mwanza

RAIS DK MAGUFULI

* Mradi uliopendwa na Nyerere watimiza miaka 34

*Africommerce  waiomba serikali kuwaunga mkono

NA THOMAS MTINGE
RAIS Dk. John Magufuli, hili ni ‘Jipu Uchungu’ linahitaji kupasuliwa. Ndivyo unavyoweza kusema  baada ya mradi mkubwa wa Bomba la Mafuta Dar-Mwanza uliobuniwa na Wazawa wa Kampuni ya Africommerce International Ltd kukwama kutokana na kile kinachoelezwa ukiritimba wa baadhi ya vigogo Serikalini.

Elisante Muro
Mradi huo mkubwa wenye sifa kwa Watanzania ulibuniwa tangu mwaka 1983, lakini umekwama mpaka sasa kutokana na ukiritimba huo usiokuwa na tija kwa Watanzania.

Akiwa kwenye ndege ndogo akisafiri kutoka Dar es Salaam-Mwanza, promota wa mradi huo alishtuka wakiwa angani kwamba kuona ndege hiyo ikiwa imebeba mafuta ndani ya ‘cabin’ ya abiria. Hiyo ilikuwa mwaka 1982.

Kwa wakati huo, Rubani ilibidi afanye hivyo kutokana na uhaba wa mafuta uliokuwepo huko Mwanza, akiwa na maana baada ya kufika huko, rubani angechukua mafuta aliyobeba kutoka Dar es Salaam na kuyajaza kwenye ndege kabla ya safari yake ya  kurudi Dar es Salaam kuanza.

 Kutokana na hali hiyo, mwaka 1983 jitihada zilianza kufanyika na promota wa mradi alianza kufanya utafiti, akianza na ule wa kiufundi kisha kufuatia wa kiuchumi ikiwemo kuandaa ramani kuonyesha bomba litakapopita.

Baada ya jitihada za muda mrefu, mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta Dar- Mwanza ambao mpaka mwaka 2005 ulikadiriwa kugharimu zaidi ya dola za Marekani milioni 400 (zaidi ya bilioni 400), ulipata idhini ya utekelezaji kutoka Ikulu Julai 17,1989.

Katika mradi huo, Wakala wa Serikali kwenye utekelezaji wake alikuwa Shirika la Mafuta ya Petroli (TPDC) ambaye alijitoa kwenye mradi huo ilipofika Oktob 1996 kwa barua iliyoandikwa na Mkurugenzi Mtendaji, Yona Kilagane.

Katika barua yake, TPDC ilisema kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo mabadiliko katika sera ya mafuta, haitaweza kuendelea tena katika mradi huo na hasa kuufadhili hata kwa kiasi kidogo hivyo wanakabidhi suala hilo zima kwa mbia wao Africommmerce International Limited.

 “TPDC inaunga mkono mradi na itahakikisha utakapoanza kazi utatumika ipasavyo,” ilisema sehemu ya barua hiyo ya Wakala wa Serikali kujitoa katika mradi.

Ili kuendelea na mradi huo, kampuni ya Africommerce ilibidi kufuatilia vibali mbalimbali na ambavyo vilipatikana vikiwemo vya Wizara ya Ardhi ambayo ilieleza kuunga mkono mradi huo, na kutaka baadhi ya masharti kutekelezwa ikiwa ni pamoja na kuonyesha ramani ya sehemu litakalopita bomba hilo na utaratibu wa ulipaji fidia.

Nakala ya kibali hicho cha Juni 4, 1997 ilitumwa kwa Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha Uwekezaji (TIC).
 Kibali kingine ni cha Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa kilichopatikana Novemba 25, 1998 huku kibali cha Kituo cha Uwekezaji kikipatikana Oktoba 16, 1997.

UTEKELEZAJI WA MRADI
 Katika kutekeleza mradi huo, ilipofika Agosti 28,1996 Kampuni ya Africommerce walimpata Mshauri wa kiufundi kampuni ya Jackson $ Tull kutoka New York, Marekani.
Africommerce pia walimpata Mshauri wa Fedha Kampuni ya Fieldstone private Capital Group kutoka New York, Marekani.

Baada ya kuwapata washauri hao, hatimaye kampuni ya Africommerce na mwekezaji kutoka Marekani pia ambao baada ya kuwasili nchini ilishuhudiwa na kusheherekewa na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Nishati na Madini wakati huo, Dk. Abdallah Kigoda (marehemu), Makamu wa Rais Elpaso, Balozi wa Marekani nchini Charles Stith, aliyekuwa Mkurugenzi wa TIC, Samweli Sitta na wengineo.

Mwekezaji huyo wa kampuni ya Elpaso alifungua ofisi hapa nchini na kuanza kukamilisha utekelezaji wa mradi. Katika kipindi hicho, mengi yalifanyika na Elpaso walitumia takribani dola milioni 2.5.

 Mradi pia ulipata baraka za Rais Benjamin Mkapa na Rais Yoweri Museveni, ambao waliutaja katika taarifa yao ya pamoja baada ya mkutano wa Agosti 1997, mjini Kampala, Uganda.

Baadae kampuni ya Elpaso iliamua kujitoa kwenye mradi huo kwa kuwa walihitaji msaada wa Serikali ili kuhakikisha kwamba ujenzi wa bomba hilo unapata baraka zake, lakini kutokana na ukosefu wa uzoefu (wakati ule) Serikali haikumpa hamasa ya kutosha.

Baada ya kujitoa kwa mwekezaji huyo, mradi uliandamwa na mambo na madai mbalimbali kutoka wizarani ikiwemo barua za kutishiwa kunyang’anywa mradi kwa Kampuni ya Africommerce.

Julai Mosi, 2004, Wizara ya Nishati na Madini ilitia saini mkataba wa makubaliano ya awali na Kampuni ya Richmond Development Company (RDC) ya Huston Marekani kwa ajili ya kuundeleza mradi wa bomba la mafuta la Dar-Mwanza.

Kwenye makubaliano hayo, RDC ilitakiwa kufanya upembuzi yakinifu na kuuwasilisha ndani ya miezi 18.

Katika kutia saini mkataba huo, TPDC ilielezwa kuwa itatoa msaada mkubwa kwa RDC ili kufanikisha upembuzi yakinifu huo, hata hivyo kampuni hiyo ilishindwa kufanikisha malengo hayo.

RAIS MKAPA AKIHUTUBIA BUNGE
Akihutubia kikao cha mwisho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano mwaka 2005, mjini Dodoma, Rais Benjamin Mkapa, alisema angependa kuona wawekezaji Watanzania ndiyo wanafaidika zaidi ya ilivyokuwa wakati huo.

“Vivutio vya uwekezaji vinatolewa sawa baina ya wawekezaji wa ndani na nje. Ninaendelea kuwahimiza Watanzania kutumia fursa na vivutio vya uwekezaji.

“Ningependa Watanzania ndiyo wawe wanafaidika zaidi ya ilivyo sasa,” anasema Rais Mkapa ambaye sasa ni mstaafu.

Kauli hiyo ya Mkapa ilifurahisha wafanyabiashara na wananchi wengi kwa imani kuwa Serikali itakuwa mstari wa mbele kuwasaidia Watanzania kunufaika na uwekezaji katika nyanja mbalimbali nchini.

Ni kweli katika mfumo wa sasa wa utandawazi duniani kote, nchi zote zinashindana kuvutia wawekezaji ikiwa ni nia pekee kuweza kuingiza nchini teknolojia ya kisasa, mitaji, ajira na uwezo wa ushindani kwenye uchumi wa soko duniani.

Kauli ya Rais mstaafu Mkapa kwa kiasi kikubwa, ilitoa fursa kwa wawekezaji wa ndani kuendesha miradi mbalimbali mikubwa ama wao binafsi au kwa ubia na kampuni nyingine za nje.

Wananchi wengi walipongeza kauli hiyo ya Mkapa kwa kuwa, kwa kiasi kikubwa ilifuta hisia zilizokuwa zimejitokeza kwao kuwa, mfumo mzima wa ubinafsishaji unanufaisha wageni zaidi kuliko wawekezaji wazawa.

Hisia za wengi zilikuwa zimeelekea kwenye kuwepo kwa upendeleo kwa wawekezaji wa kigeni hata kama hawana uwezo kulinganisha na wa hapa nchini lakini kwa kuwa tu wanatoka nje basi wanapewa fursa na wananchi kuachwa bila msaada.

Miongoni mwa wafanyabiashara Wazalendo waliopongeza kauli hiyo ya Mkapa ni Mwenyekiti wa Africommerce 
International Ltd, Elisante Muro.

Muro anasema kauli ya Mkapa (wakati huo) ilileta faraja kubwa kwa wafanyabiashara wa hapa nchini, ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakishiriki kuinua pato la taifa na kwa kiasi kikubwa wamefanikiwa kwa kuwa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa ya kiuchumi.

“Ni kweli wawekezaji Watanzania wanastahili kunufaika na mfumo mzima wa ubinafsishaji kwa kuwa hii ni nchi yetu na matunda yake inabini tufaidi wenyewe badala ya wageni ambao baada ya kuchuma wanakwenda kufaidi kwao…nilimpongeza sana Mkapa kwa kuliona hilo.” anasema Muro.

Agizo la Mkapa lilikuja kipindi kifupi baada ya Bunge la Jamhuri ya Muungano kupitia Kamati ya Fedha na Uchumi, kuagiza Wizara ya Nishati na Madini kutekeleza makubaliano yaliyofikiwa, ambapo Wizara iliagizwa kutafuta njia muafaka ili Africommerce wasaidiwe kuutekeleza mradi wa ujenzi wa bomba la mafuta Dar- Mwanza.

Kamati iliitaka Serikali kuwapa fursa pekee Africommerce kuutekeleza mradi huo ikizingatiwa kazi kubwa, gharama na mikasa ya aina mbalimbali ambayo kampuni hiyo waliikabili kwa takribani miaka 10.

Uamuzi huo wa Kamati ya Bunge ulitolewa baada ya Wizara ya Nishati na Madini kutoa ‘Exclusivity Right’ kwa kampuni ya Richmond ya Marekani.

“Katika kikao chetu cha April 6, 2005, tulikubaliana waziri (Yona), ungetafuta njia muafaka ya kufanikisha azma yetu hiyo.

“Huu ni mradi ambao Wazalendo wetu, kwa ufanisi wa aina ya pekee, walithubutu kuutolea jasho na ujasiriamali kwa uvumilivu mkubwa sana. Kwa hakika wanastahili msaada wetu,” inasema barua ya Kamati.

“Kamati yetu (Bunge) ina imani kwamba watendaji husika Wizarani kwako wataagizwa ipasavyo wakutane na Kampuni ya Wazalendo hawa wa Africommerce kwa ajili ya kufanikisha tuliyokubaliana,” inasema barua ya Kamati hiyo kwenda kwa Waziri wa Nishati na Mdini, Daniel Yona.

AFRICOMMERCE INASEMAJE KUHUSU MRADI?
 Mwenyekiti wa Africommerce,  Elisante Muro, anasema mradi huo bado unahitajika na kwamba unavutia kama binti mdogo anayechumbiwa.

“Mradi huu naweza kuufanananisha na msichana mdogo mzuri anayevutia na kutamanisha wanaume wengi kutaka kumchumbia.

“Kutokana na uzuri wa msichana huyu, wapo wanaume wanaojitangazia eti ni mchumba wao, wapo wanaosema wameshatuma barua ya uchumba.

“Chakushangaza pamoja na mbwembwe zote hizo,  hakuna hata mmoja wao aliyepata nafasi ya kukutana naye uso kwa uso. Wahenga wanasema chema chajiuza kibaya chajitembeza,” anasema Muro.

Anasema yeye ndiye mbunifu halisi wa mradi huo na hajawahi kushindwa kuufanikisha bali alipata vikwazo kutokana na mradi kushughulikiwa na Wizara badala ya TIC, ambacho ni chombo pekee kilicho na miundombinu ya kusimamia mradi huo.

 Muro anasema Kampuni yake ya Africommerce imetumia gharama ya mabilioni ya fedha pamoja na muda mrefu kuufikisha mradi hapo ulipo mpaka ukavutia na wengine kuwa na tamaa ya kuutekeleza bila hata kumshirikisha.

Anasema ‘matatizo kidogo’ yaliyojitokeza kwenye mradi 
huo, yaliwashtua kwa kiasi kikubwa baada ya kampuni nyingine kuingia mkataba wa kuuendeleza badala ya kampuni yake.

Mwenyekiti huyo anaongeza kuwa, Africommerce wanaona RDC ilitumiaa mlango wa nyuma kuingia mkataba na Serikali baada ya kampuni za ushauri za Africommerce za Fielstone Private Capital na Jackson $ Tull kuwa ndizo zilizotambulishwa kampuni hiyo na Africommerce.

“Kutokana na sera ya sasa ya nje na masuala ya
Uchumi. Africommerce iliueleza ubalozi wa Tanzania nchini Marekani kusaidia kuupromoti mradi nchini humo, ndipo ubalozi ulipoitambulisha kampuni ya RDC kwa 
Africommerce ikionyesha nia ya kuingia kwenye ubia wa mradi huu,”anasema Muro.

Anaongeza kuwa: “Kwa kuwa washauri wetu wa ufundi na fedha pia ni kampuni za Marekani, tuliwaeleza wawasiliane na RDC ambapo walitushauri kuwa sio wawekezaji wazuri katika mradi huu.”

Muro anasema iliwachukua Africommerce miaka 15 kuutangaza mradi huo hadi hatua iliyofikia wakati huo mwaka 2005 na kuhoji iweje RDC wafanikishe mradi huo kwa kipindi cha miezi 18 tu?

Vilevile, Africommerce inahoji iweje wakati wakishughulikia mradi huo, TPDC ilitangaza kujiondoa na kuiachia kampuni hiyo lakini sasa imerudi tena na kutaka kuisaidia RDC.

Muro anampongeza Mkapa kwa kuona umuhimu wa kuwasaidia wawekezaji Watanzania ili wafaidike na mfumo mzima wa ubinafsishaji, lakini wamekuwa wakikwamishwa na ‘wajanja’.

Kutokana na dosari chache zilizojitokeza , Mwenyekiti wa Africommerce, Muro anapongeza Bunge la Jamhuri ya Muungano kwa kuona jitihada walizofanya hadi kuufikisha hapo ulipo mradi huo na hivyo kuamua wakabidhiwe tena kwa nia ya kuendeleza.

Pia anapongeza jitihada za Waziri Yona katika kuhakikisha kampuni hiyo inarudishiwa mradi kama alivyokubaliana na Kamati ya Bunge ya Uchumi na Fedha.

“Maamuzi haya kama ilivyokuwa kwa City Water yanawezekana. Lakini sio kuwezekana tu, bali yanatia moyo sisi wafanyabiashara Watanzania kuendelea na jitihada za kuwekeza ili kufaidi matunda kwa pamoja. Serikali ya awamu ya tatu ni ya kupongezwa sana na kwa kweli imefanya mengi kuinua uchumi,” anasema Muro.

Muro anasema baada ya taarifa ya Kamati ya Bunge na kauli za Mkapa, wawekezaji mbalimbali kupitia balozi za Tanzania , wamekuwa wakiwasiliana na kampuni yake kuhusu mradi huo kwa lengo la kuingia ubia.

VIKWAZO.
Hata hivyo, Muro anasema wakati wakisubiri utekelezaji wa makubaliano ya Kamati hiyo ya Bunge na Waziri Yona(wakati huo), Februari 8, 2007, Serikali kupitia Wizara ya Mipango, Uchumi na Uwekezaji kupitia Waziri wake, Alhaji Juma Ngasongwa, ilitangaza kuipa mradi huo Kampuni ya kigeni M/S Oil and Industrial Technology Ltd (NOIT).

Anasema kitendo hicho cha Serikali kiliipa wakati mgumu sana, kampuni yake kutokana na hila za makusudi zilizokuwa zikifanywa dhidi yao kuhusu mradi huo.

“Tuliona na kusikia kupitia vyombo vya habari Waziri Ngasongwa (wakati huo) akitangaza rasmi serikali kuipa kampuni hiyo ya kigeni mradi huo.

“Huu ulikuwa uamuzi wa kibabe usiojali Wazalendo kwani badala ya kuisaidia kampuni yetu kwa kutekeleza makubaliano ya Kamati ya Bunge ilivyoagiza, ikawa kinyume chake,” anasema Muro.

Muro anasema pamoja na ubabe huo, hakukata tamaa na badala yake aliitisha mkutano na waandishi wa habari akieleza kampuni nia ya kutaka kwenda mahakamani kupinga uamuzi huo wa serikali wa kupora mradi wao.

Anasema katika mkutano wake na waandishi wa habari Muro alieleza bayana kwamba kampuni yake ndiyo mbunifu wa mradi huo tangu mwaka 1983 na kwamba hawaoni tija serikali kuupora na kuipa kampuni ya kigeni.

“Niliiwambia waandishi wa habari iweje mtoto wangu wa kike niliemzaa mwenyewe akaozwe na watu wengine wakati mwenyewe nipo?

“Kama kuzaa niliachiwa mwenyewe kwanini nisioze mwenyewe?. Kwa ufupi nilipinga kwa nia njema uamuzi huo kutokana na serikali kutonishirikisha,” anasema Muro.

Muro anasema kuwa mradi huo ulikuwa ukifuatiliwa kwa karibu na Hayati Baba wa Taifa, Mwalimu Julius Nyerere na kama asingefariki ndani ya kipindi cha miezi sita, ungeweza kuwa umeanza utekelezaji wake.

Anasema kuwa fedha za kuendesha mradi huo wanazo na wanachohitaji kwa sasa ni Baraka kutoka kwa serikali ili mradi huo uweze kuanza.

MAJIBU YA SERIKALI
Kwa mujibu wa taarifa kwa vyombo vya habari iliyotiwa saini na Waziri wa Mipango, Uchumi na Uwekezaji, Dk. Juma Ngasongwa, Februari 2007, ilieleza kuwa, mradi unaozungumzwa na kampuni ya Africommerce ulihusu kujenga bomba la mafuta pekee na mradi wa NOIT ulioidhinishwa na serikali unahusisha kujenga kiwanda cha kusafisha mafuta ghafi na bomba  la kusafirisha mafuta kutoka Dar es Salaam hadi Mwanza na tawi lingine la bomba hilo kuelekea Kigoma.

Kwa mujibu wa taarifa ya Ngasongwa, mradi huo wa NOIT ni tofauti na mradi wa Africommerce kwa ukubwa wa mtaji, upana wa mradi na hata soko linalolengwa.

SERIKALI AWAMU YA TANO
Moja ya jitihada za serikali za awamu ya tano, chini ya Rais John Magufuli, ni kuwajali wawekezaji wa ndani. Kwa maana hiyo, ni wakati sasa suala hili likatafutiwa ufumbuzi wa haraka ili mradi huo uweze kufanya kazi.

Kwa mujibu wa Dk. Magufuli, wakati akizungumza na wafanyabuishara nchini, alihimiza uwekezaji wa ndani kwa kuwataka wafanyabishara wazawa kuungana na serikali katika kuinua uchumi wa taifa.

Dk. Magufuli aliwaeleza kuwa, serikali yake ipo tayari kushirikiana na wafanyabishara wanaotaka kuwekeza na kuagiza kwamba, mtendaji atakayechelewesha kibali cha leseni ya kibiashara atachukuliwa hatua kali.

Kwa msingi huo, ni wakati sasa kwa kampuni za wazawa ambazo zimejitolea na kuonyesha uwezo wa kufanya uwekezaji wa ndani kuangaliwa kwa jicho la pili ili watekeleze majukumu yao.

Kitendo cha kujengwa kwa bomba hilo, kutasaidia kuokoa uharibifu wa barabara unaofanywa na malori ya mafuta na  matokeo yake kuhitaji matengenezo ya mara kwa mara.

Endapo Serikali ikitilia maanani mradi huu kwa kutoa ushirikiano mzuri kwa WAZAWA waliouanzisha, utaweza kuchochea uchumi wa viwanda na biashara na kutoa ajira nyingi kwa Watanzania kama ilivyo sasa katika mradi wa bomba la mafuta kutoka Nchini Uganda kuja Tanzania.


Katika mradi huo Rais Dk. Magufuli alionyesha msimamo wake kwa Watanzania kupewa ajira nyingi na si vinginevyo.
Elisante Muro akiwa  na Baba wa Taifa Hayati Mwalimu Nyerere katika kipindi cha kuanzishwa mradi huo
Elisante akijadiliana jambo na aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini Profesa Sospeter Muhongo kuhusu mradi huo

No comments