Breaking News

ALLY YAHAYA ;MKONGWE WA DANSI ALIYECHUKIZWA NA MUZIKI WA DANSI KUTOSWA

ALLY  YAHAYA
 Mkongwe anayechukizwa muziki wa dansi kutoswa

NA MWANDISHI WETU

MUZIKI wa dansi nchini umetumikiwa na wanawamuziki wengi wenye umahiri katika upigaji wa ala za muziki, zinazoleta vionjo vya kuburudisha.

Miongoni mwa wanamuziki hao ni Ali Yahaya(57), ambaye ni gwiji wa upigaji wa chombo cha ‘trumpet’, ingawa kuna baadhi ya vyombo anavyovimudu kuvipiga akiwa na bendi tofauti hapa nchini.King Maluu na Yahaya wakipulkiza Saxophene

Mwanamuziki huyo alifanya mahojiano na gazeti hili, katika kufahamu safari yake ya muziki na anavyoendelea kuitumikia fani hiyo.

Yahaya ambaye ni mzaliwa wa Mkoa wa Morogoro, alihusudu kazi ya upigaji wa ala za muziki hususan kifaa hicho na kuanza kujifunza upigaji wa vyombo hivyo.

“Mimi nilianza kujifunza kupiga trumpet mwaka 1971, katika chuo cha muziki, kilichokuwa kikiendeshwa na padri mmoja aliyefahamika kwa jina la Father Kanuti, kilichoko mkoani Morogoro na nilihitimu mwaka 1976.

“Nilifanya mafunzo hayo huku nikiwa naendelea na masomo ya shule ya msingi katika shule ya Msingi Kilakala, iliyoko mkoani Morogoro hadi nilipohitimu kwa hiyo nikawa nafanya vitu vyote kwa wakati mmoja,”anasimulia.

Anaeleza kutokana mapenzi yake katika upigaji wa chombo hicho, hivyo haikumpa tabu ya kujifunza na kuelewa juu ya upigaji wa chombo hicho,  tofauti na baadhi ya wanamuziki waliojifunza kupiga kifaa hicho.

“Wakati najifunza sikupata ugumu wala changamoto yoyote kwasababu nilipenda kifaa hicho kukipiga kwa hiyo sikuwahi kuumia mashavu au kifua kuniuma,”anasema.

Akizungumzia kuvutiwa kupiga chombo hicho, anaweka wazi alivutiwa na kwaya ya chipukizi ya vijana ya mkoani Morogoro, jinsi wanavyopuliza vifaa hivyo.

Anasema umaridadi wa kutumia vyombo hivyo na miondoko yao, ilimhamasisha  hivyo kuwa, na ndoto ya kupiga kifaa hicho.

Anamueleza mkufunzi wa muziki Father Kanuti, ambaye alikuwa ni mkufunzi mkuu katika chuo hicho kuwa, ni chachu ya wanamuziki wengi kujua upigaji wa vyombo hivyo.

Kwa mujibu wa Yahaya, chuo hicho cha muziki kilikuwa ni chachu ya mafanikio ya wanamuziki wapigaji ala muziki katika nchi za Jumuia ya Afrika Mashariki(EAC).

Hata hivyo, anasikitishwa kufa kwa chuo hicho kwani kimesababisha kutokuwepo kwa wapigaji mahiri wa ala za muziki nchini na Afrika Mashariki kwa ujumla.

Pamoja na kufa kwa chuo hicho, anafarijika kwa baadhi ya wadau wameanza kupanga mikakati ya uanzishwaji wa chuo cha aina hiyo jijini, Dar es Salaam.

Mkongwe huyo wa muziki wa dansi, anawahamasisha vijana kupenda kupiga ala za muziki, kwa kujifunza kutoka kwa wakongwe waliobakia.

Kuhusu maendeleo ya muziki wa dansi nchini, anaeleza muziki huo una maendeleo makubwa, lakini unakosa msaada ya kutangazwa na kupewa ufadhili kutoka kwa wadau.

Kulingana na maelezo yake, vyombo vya habari vingi  vimewapa fursa zaidi muziki wa ‘bongo fleva’, hivyo muziki wa dansi kuonekana kama haupo kumbe uko hai.

Anafafanua kuwa, uhai wa muziki huo unajionyesha katika kumbi mbalimbali, ambako bendi hupiga na kukonga nyoyo za mashabiki.

Akizungumzia faida za kufanya kazi yake ya muziki, anasema imemsaidia kumudu maisha yake ikiwemo kujenga nyumba yake na kuweza kumudu mahitaji ya familia yake.

Mbali ya kumudu kupiga trumpet, anasema pia anaweza kupiga kifaa cha ‘alto saxaphone’ na ‘drums’.
                         
                         Safari yake ya muziki
Anaeleza kuwa,  mwaka 1976 hadi 1979, alianza safari yake ya muziki akijiunga na bendi Mzinga Troup, iliyokuwa ikimilikiwa na Jeshi la Wananchi wa Tanzania(JWTZ) mkoani Morogoro.

Anasema mwaka 1980, alijiunga na bendi ya Super Matimila na baadaye mwaka 1981 alijiunga na bendi ya Orchestra Tomatoma zote za jijini Dar es Salaam.

Mwaka 1983, alijiunga na bendi ya UDA Jazz na mwaka huo huo alijiunga na bendi ya Vijana Jazz na mwaka 1984 alijiunga na  Mlimani Park Orchestra.

Anasimulia kuwa, mwaka 1999, alijiunga na bendi ya OTTU Jazz, ambapo mnamo mwaka 2005, alirejea bendi ya Mlimani Park Orchestra.

Wahenga walisema safari moja huanzisha nyingine, hivyo mwaka 2006, mkongwe huyo alitimkia jijini Mwanza na kujiunga na bendi ya Mwanza Carnival na baadaye mwaka 2008 kujiunga na bendi ya Pea Musical ya jijini humo.

Anaeleza kuwa safari yake ya muziki iliendelea mwaka 2014, alipohamia bendi ya Super Kamanyola, ya jijini Mwanza na baadaye mwaka huo huo kurejea bendi ya Mlimani Park.

Mkongwe huyo anasema baada ya kuhangaika katika bendi za watu, aliamua kuanzisha bendi yake mwaka 2014,  inayoitwa La Rhumba, ambayo anaendelea nayo hadi sasa.

Anasema kumiliki bendi kunasaidia kukamilisha mipango ya muziki, aliyojipangia kuliko kumilikiwa na mtu.

Anaeleza bendi hiyo hupiga katika kumbi mbalimbali za burudani, ikijikita zaidi katika upigaji wa nyimbo za zamani.

Hata hivyo, anaweka wazi kuwa, hufanyakazi nyingine katika bendi nyingine kwa mwaliko wa kazi maalum ikiwemo kushiriki katika bendi ya Utalii inayorudia kupiga nyimbo za zamani katika kituo cha televisheni cha Azam.

Ni dhahiri kwamba, wanamuziki chipukizi wana kitu cha kujifunza kutoka kwa mwanamuziki huyo hususan katika safari yake ya muziki.

Ni miongoni mwa wanamuzi wachache waliotumikia muziki wa dansi kwa zaidi ya miaka 40 nchini, hivyo uzoefu wake ni rasilimali kwa wanamuziki chipukizi.

No comments