Breaking News

JINSI MIONZI YA NYUKLIA INAVYOSAMBARATISHA UVIMBE MWILINI


Namna mionzi ya nyuklia inavyosambaratisha uvimbe mwilini

NA MWANDISHI WETU.


MATIBABU na vipimo vya saratani na tezi dume kwa njia ya mionzi ya nyuklia, ni teknolojia ambayo haijafahamika katika jamii.

Uchunguzi wa afya kwa njia hii hutoa majibu ya haraka na kupendekeza aina ya matibabu anayopaswa kufanyiwa mgonjwa kwa kadri alivyoathirika.

Daktari Bingwa wa matibabu hayo wa Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, Tausi Maftah, anasema mionzi ya nyuklia inayotumika kutibu na kupima magonjwa kwa binadamu, haina uhusiano na mionzi ya kutengenezea mabomu.

Anaeleza mionzi ya nyuklia inayotumika katika matibabu na vipimo imepimwa mahsusi kwa ajili ya kutumika katika matibabu na uchunguzi, hivyo hakutakuwa na madhara ya mionzi hiyo mwilini.


Kwa mujibu wa daktari huyo, mionzi  hutofautiana ambapo ya kutibu ina nguvu zaidi na haiwezi kutoka nje ya mwili.

Mionzi hii hufanya kazi ya kuua chembe za saratani au ugonjwa mwingine ulio mwilini, lakini inayotumika kwa ajili ya vipimo hutoka nje ya mwili ili kusaidia kubaini aina ya ugonjwa.

Kipimo cha mionzi ya nyuklia, anasema  husaidia kuonyesha saratani imeenea kwa kiasi gani mwilini kabla ya matibabu kutolewa kwa mgonjwa.

Kusambaa kwa saratani mwilini  hunatofautiana kulingana na aina ikiwemo  matibabu, ambapo wagonjwa wengine watafanyiwa upasuaji kulingana na eneo saratani ilipo.

Pia anasema lengo la matibabu kwa njia ya mionzi ni kuua chembe za seli zilizosalia baada ya kufanyika upasuaji wa kuondoa uvimbe wa saratani.

Dk. Tausi anatoa mfano namna saratani ya matiti inavyosambaa mwilini kawamba ni tofauti na saratani ya tezi dume, mifupa pamoja na mapafu ambapo zote hutofautiana tabia katika usambaaji.
“Kwa mfano, saratani ya matiti hukimbilia  kwenye ini, mapafu, ubongo na matezi za kwapa, hivyo miozi hii hutumika kubaini usambaaji wa magonjwa haya kwa usahihi,” anasema.  
Mionzi hii Dk. Tausi anasema inao uwezo wa kutibu na kupima magonjwa ya tezi dume, maumivu katika mifupa, saratani ya matezi ya mfumo wa homoni ikiwemo aina zingine za saratani na magonjwa yasiyo saratani.

Anaeleza namna kipimo hiki kinavyotumika katika matibabu ya magonjwa hayo ambapo mgonjwa huchomwa dawa maalumu yenye mionzi ya nyuklia ambayo huenda moja kwa moja kwenye mifupa na kuonyesha taswira nzima ya fuvu la binadamu.

Sehemu ambayo inayokutwa na ugonjwa hususan saratani, wataalamu huweza kuona  ukubwa wa ugonjwa na kumshauri mgonjwa kufanyiwa upasuaji, wakati mwingine saratani hufikia hatua ya kuathiri uti wa mgongo na mgonjwa kupooza,” anasema.


Dk. Tausi anasema hatari ya mgonjwa kupooza inaweza kuondolewa na kipimo cha mionzi ya nyuklia kabla ya athari kuwa kubwa na wataalamu kufanya matibabu ya haraka kwa mgonjwa katika eneo lililoathirika.

Anasema saratani ya matiti ikigundulika mapema, matibabu yanaweza kufanyika kwa dawa maalumu.

“Tunachanganya dawa hiyo na mionzi ambapo huweza kusambaratisha uvimbe na kubadilisha mfumo wa matibabu, iwapo  mgonjwa alikuwa afanyiwe upasuaji.

Tunapobaini ugonjwa, licha ya kutibu tunafanya pasuaji kwa kulenga moja kwa moja eneo ambalo uvimbe umeonekana,” anasema.

Utaalamu mwingine anaoelezea ni kuhusu kifaa cha kusaidia uchunguzi wa saratani kiitwacho PET- CT, ambacho hutumia mionzi ya nyuklia katika uchunguzi wa saratani.

Anasema kipimo hiki kinauwezo wa kubaini chembechembe ndogo zaidi za saratani mwilini na kuelekeza tiba sahihi iwapo  mgonjwa anafaa kufanyiwa upasuaji au kutibiwa kwa njia ya kawaida.

“Kwa mfano mgonjwa wa saratani ya mapafu, tunaangalia ni tezi gani imeathirika ili kubaini iwapo mgonjwa atafanyiwa oparesheni au kupatiwa dawa ya dripu ya mionzi. Iwapo ugonjwa umehamia katika pafu lingine au kwenda nje ya mapafu, kifaa hiki kinaonyesha,” anasema.

“Hivyo kifaa hiki kinaweza kuonyesha aina ya ugonjwa kabla ya tiba na iwapo mgonjwa alipatiwa dripu ya mionzi iliyochanganywa na dawa, huonyesha  kama amepona au ugonjwa unarudi,”  anasema.

Vipimo vya Mionzi ya Nyuklia kwa Tezi dume
Anasema PET-CT hutumika kwa kuchanganywa na vimelea vilivyoko ndani ya tezi dume, hushika maeneo yanye tezi na kuonyesha aina ya ugonjwa .

Dk. Tausi anasema kipimo hicho kina uwezo wa kupima maradhi yaliyo kwenye ini na mifupa, kwa matibabu ya tezi dume,  ugonjwa ukigundulika mionzi ya nyuklia huchanganywa na vimelea vya tezi dume na mgonjwa kudungwa ambayo huondoa ugonjwa huo mwilini.
 “Hivyo tunatibu saratani kwa kujua aina na eneo ilipo, tunachunguza tabia yake na kutafuta kitu chenye tabia inayofanana na ugonjwa huo kasha tunaiwekea mionzi ya nyuklia halafu dawa hiyo inakwenda hadi eneo lenye tatizo na kutibu.

 “Tunapotibu tezi dume tunaweza kumpa dawa za kupunguza vichocheo vya kiume, ugonjwa ukisamba mwilini na kuleta athari katika mifupa au sehemu zingine tunatoa matibabu kwa njia ya mionzi ya nyuklia,” anasema.

Mionzi ya nyuklia kwa uvimbe kwenye kizazi na saratani .
Kutokana na mtu mwenye uvimbe kwenye kizazi na kutokwa damu nyingi bila mpangilio, matibabu ya kwanza anayotaja Dk. Tausi ni upasuaji wa kuondoa uvimbe.

Anasema matibabu kwa njia ya mionzi kwa mtu mwenye uvimbe kwenye kizazi hatumiki, lakini mgonjwa akiwa na saratani katika mji wa uzazi mgonjwa anaweza kutibiwa kupitia mionzi ya nyuklia, baada ya upasuaji.

“Kwa mfano upasuaji wa kuondoa saratani katika tezi ya shingo (rovu), ubakiza vimelea vya ugonjwa huo, mgonjwa akiachwa hivyo  ni  lazima ugonjwa utarudi, hivyo lazima tutumie mionzi ya nyuklia kuchoma vimelea hivyo katika mji wa uzazi,” anasema.

Mgonjwa wa goita na Mionzi ya Nyuklia 
Anasema wagonjwa wenye uvimbe kwenye shingo hawaruhusiwi kutumia aina za samaki samaki ambazo hukinzana na mionzi ya nyuklia, kulingana na maelekezo ya  wataalamu.

Kuhusu tatizo la rovu, Dk. Tausi anasema wagonjwa wenye matatizo hayo kwa utaalamu wa hali ya juu, wanaweza kutibiwa na kupona.
“Ugonjwa huu unatibika, wagonjwa waje wasiogope kupata huduma hii ya tiba ambayo itnaasaidia kuponya kabisa,” anasema.
Unywaji wa kahawa na uhusiano wa  matibabu ya nyuklia .

Mionzi ya nyuklia katika kubaini maradhi ya moyo na mishipa kuziba, inafanya kazi kwa kiwango kikubwa ikiwemo kwa watu wanaovuta sigara, wasiofanya mazoezi na wenye kisukari.

Kipimo  hiki cha nyuklia kinaweza kutoa taarifa endapo moyo unaanza kufanya kazi kwa kiwango cha chini.

Upande wa moyo ulioziba wataalamu kwa kutumia vipimo hivyo, huweza kutoa mapendekezo ya kuzibuliwa kwa mirija ya moyo na kuruhusu damu kusambaa ipasavyo mwilini.

Dk.Tausi anaeleza kwamba wakati wa vipimo mgonjwa haruhusiwi kutumia kahawa kutokana na matibabu hayo ya nyuklia kukinzana na kahawa, kwa kuwa hubadilisha mapigo ya moyo na kukifanya kipimo kutogundua matatizo ya moyo.

Pia anasema kwa wagonjwa wenye maradhi ya figo, mionzi ya nyuklia huchangwa na dawa maalumu ambayo huenda kwenye figo na kuonyesha utaratibu mzima wa namna inavyofanya kazi.
Hapo hubaini maradhi ikiwemo kufeli kwa figo, kuwepo kwa mawe na mkojo kubaki kwenye figo.

Dk.Tausi anasema wanaweza kuona ni kwa namna gani figo imeathirika na kutoa mapendekezo iondolewe au kushauri njia nyingine ya matibabu.

Wagonjwa wanaopandizwa figo Dk. Tausi anasema kutokana na utaalamu wa matibabu kwa njia ya mionzi ya nyuklia wanaweza kupendekeza aina gani ya figo inayomfaa mgonjwa, wanaotoa figo hawaruhusiwi kutumia kahawa.

Hilo ni kutokana na kusababisha athari katika mfumo wa uchujaji taka mwilini, wakati mwingine kahawa huathiri ufanyaji kazi wa nyuklia mwilini.

Wataalamu wenye ujuzi wakutoa huduma hii ni wachache ikilinganishwa na umuhimu wake, hata hivyo serikali inajitahidi kupeleka wataalamu nje ya nchi kusoma.

Dk. Tausi anasema wataalamu wachache waliopo wameanza kutoa mafunzo kupitia warsha kwa wataalamu wa magonjwa mbalimbali ikiwemo kuwapa ujuzi juu ya matibabu kwa njia ya mionzi ya nyuklia.
Stela Japhet, anasumbuliwa na saratani ya matiti ambapo anasubiri majibu ya kipimo cha miozi ya nyuklia, anasema ana matumaini kwani ameeleazwa na wataalamu kwamba  kipimo hicho kinasaidia kutibu saratani hata iliyosambaa.
Anasema mara ya kwanza alikuwa na uvimbe mdogo katika titi la upande wa kulia, lakini baadae alianza kuhisi maumivu makali ambapo kwa mujibu wa maelezo ya wataalamu, alijihisi ana saratani ya matiti.
Stela anasema mionzi hiyo itamsaidia kuondoa vimelea vya saratani, ambavyo vinaweza kusambaa na kutengeneza saratani nyingine mwilini.

Alphonce Maliki, anazungumzia teknolojia ya matibabu kwa njia ya mionzi ya nyuklia kama matibabu ya kisasa zaidi na kusema  kadri siku zinavyokwenda watu watakuwa hawafanyiwi upasuaji wa kuondoa uvimbe mwilini.

Lakini anasema elimu kwa jamii ndogo, wanajamii wanapaswa kupima afya zao na kubaini iwapo ni wagonjwa na saratani  ipo katika hatua gani ili kudhibiti isienee.

Maliki anasema baadhi ya watu wanadhani  mionzi ya nyuklia ni hatari, hivyo wanahofu ya kupata madhara.

Anashauri wataalamu kufanya vipindi  katika runinga na kufanya makongamano mbalimbali ya afya, kueezea teknolojia hiyo ili kuamsha ari kwa wananchi kuchangamkia huduma hiyo.

Paulina Meshak anaeleza kuwa na tatizo la mifupa kusuguana katika miguu kwa zaidi ya miezi miwili sasa, ambapo humpa ugumu wa kutembea kutokana na maumivu makali.

“Kwa mara ya kwanza natamani kutumia kipimo hicho ili kubaini hitilafu iliyopo  katika maungio ya goti na kunisababishia maumivu,” anasema.

Serikali haina budi kupongezwa kwa jitihada za kujali afya za Watanzania, vinginevyo wangelazimika kupata huduma hii nje ya nchi na kwa gharama kubwa.

No comments