Breaking News

MABINTI WANAOZALIWA NA WANAWAKE WENYE UMRI MKUBWA HUWEZA KUWA TASA

Mabinti wanaozaliwa na wanawake wenye umri mkubwa huweza kuwa tasa

NA MWANDISHI WETU

Utafiti unaonyesha kwamba wanawake wanaochelewa kuanzisha familia, hususan kupata watoto maishani, binti zao huwa na uwezekano mdogo kuzaa.

Utafiti unaonyesha asilimia 40 ya wanawake waliozaliwa wakati mama zao wakiwa na umri wa miaka 35 na kuendelea, hubaki wagumba maishani.

Matokeo hayo yanalinganishwa na utafiti uliofanywa kwa akina mama waliopata ujauzito katika umri wa miaka ya 20, ambao watoto wao hufanikiwa kupata watoto bila taabu.
Hata hiyo, utafiti huo unaonyesha watoto wa kike kwa kawaida hurithi toka mwenendo wa wazazi wao.

Kwa mujibu wa utafiti huo, wanawake wanaochelewa kuazisha familia, wanapaswa kutambua kwamba wanaweza kuwa sababu ya utasa kwa watoto wao hususan wa kike.

“Mama anavyozidi kuwa mkongwe, anapoamua kuzaa, upo uwezekano mkubwa binti yake akawa tasa maishani,” inaeleza taarifa ya utafiti huo.“Mfumo wa uzazi wa mwanamke mwenye umri mkubwa, kwa kiasi kikubwa unaweza kuathiri rutuba ya mtoto aliye tumboni mwake,” wanasema watafiti hao.

Kwa mujibu wa jarida la masuala ya uzazi wa binadamu, wanasayansi wanataarifu uhusiano mkubwa uliopo baina ya umri wa uzazi kwa mwanamke,  unavyomwathiri binti atakayezaliwa.

“Wamama waliozaliwa na wanawake wenye umri mkubwa, kwa kiasi kikubwa huwa na uwezekano wa kukosa watoto maishani mwao,” linaeleza jarida hilo.

Utafiti huo ulijumuisha takribani wanawake 43,000, wenye umri wa miaka 44 na zaidi, na kutoa matokeo hayo.

Pia matokeo ya utafiti huo yanaonyesha mabinti wenye elimu ya ngazi ya juu (walioelimika kwa kiwango kikubwa), wanao uwezekano mdogo kupata watoto maishani mwao.

Pengine ni kutokana na kuishi maisha marefu wakiwa masomoni kabla ya kuanzisha familia, ambazo kimsingi  huzianzisha wakiwa na umri mkubwa ambao si rahisi kupevusha mayai.

“Lakini katika kulinganisha wanawake wenye kiwango sawa cha elimu, inaendelea kuthibitika kuwepo kwa uhusiano kuhusu kutozaa na umri wa mama zao walipowazaa wao.

Utafiti uliofanywa kwa wanyama na Chuo Kikuu cha McGill, Mjini Montreal, Nchini Ufaransa, unaonyesha baolojia ya matumbo makongwe kuathiri mfumo wa uzazi wa watoto waalio katika matumbo hayo.

Kwa mfano; panya mkongwe mwenye jinsia ya kike, anao uwezekano mkubwa wa kupata matatizo katika mfuko wake wa uzazi.

Lakini jopo la watafiti hao lilikubaliana na ukweli wa matokeo kwamba si lazima binti wa mwanamke mkongwe kuwa na kiwango cha chini cha uwezekano wa uzazi.

Hatimaye jopo hilo lilihitimisha kwamba “iwapo matokeo ya utafiti wetu yanahusiana na sababu za kibaolojia, kitabia, kijamii ama kiuchumi au mchanganyiko wa vyote, hata hivyo suala hili linahitaji utafiti zaidi ili kuthibitisha ukweli halisi,”.

Maoni mbalimbali yanatolewa na wanajamii kuhusu suala hili, ambapo Lina Temba anasema yeye alizaliwa mama yake akiwa na umri wa miaka 27, lakini hivi sasa ana miaka 45 na hajabahatika kupata mtoto.
Anasema aliolewa akiwa na umri wa miaka 22, hivyo utafiti huo bado hauhusiani kiuhalisia na suala lake.
Faith Colman, anasema suala la muhimu ni kujitahidi kuchagua mwenza sahihi, lakini kwa kiasi kikubwa kupata ama kutopata watoto licha ya masuala ya kibaolojia, linahusiana zaidi na  majaaliwa ya Mwenyezi Mungu.

Anasema utafiti unaweza kusema hivi ama vile, lakini anatolea mfano wa  ukoo wao ambapo kuazia bibi zake, wanawake wameendelea kupata watoto hadi kipindi cha kabla ya ukomo wa hedhi.

Enny Amaniel, anasema mama yake alimzaa akiwa na umri wa miaka 21, lakini baada ya yeye kuolewa akiwa na miaka 29 alikaa miaka 5 kabla ya kubahatika kupata ujauzito.
“Hivi sasa nina miaka 34, ndio nimejifungua mtoto wangu wa kwanza (wa kiume) mwezi uliopita, namshukuru Mwenyezi  Mungu,” anasema.

John Kamugisha, anasema walifunga ndoa na mkewe Aichi wakiwa na umri sawa wa miaka 29, walisubiri hali yao ya uchumi iboreke ndipo wazae.

“Hivi sasa tuna umri wa miaka 37 ndio tumepata watoto mapacha juzi na tunategemea kuzaa tena iwapo tutajaaliwa, miaka miwili ijayo,” anasema.
Kuhusiana na utafiti huo, Kamugisha anasema haamini kwamba kila mwanamke asiye na mtoto, ni tasa.
Hata hivyo, Daktari Bingwa wa Magonjwa ya Wanawake, Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, Dk. James Chapa, anaeleza kwa kiasi namna anavyofahamu kitaalamu kuhusiana na suala hili.

Anasema mama anavyozidi kuzeeka mayai nayo yana umri (huzeeka), hivyo sio tu kwenye suala la urutubishwaji mayai, bali pia hata yanaporutubishwa mtoto husika huweza kuzaliwa na upungufu fulani.

Ingawa si wote, lakini upo uwezekano mkubwa umri wa mama unapoongezeka, kuzaa mtoto mwenye mapungufu.
 “Upo ugonjwa unaoitwa ‘down syndrome’ ambao huwapata watoto hususan waliozaliwa na akina mama wenye umri mkubwa,” anasema.

Akieleza kuhusu ugonjwa huo, Dk. Chapa anasema ni watoto hao kutozaliwa na hali ya kawaida, bali huwa na upungufu ambapo mara nyingi ni matatizo ya kijenetiki (kurithi).

Hata hivyo anasema matatizo hayo hutokea si katika umri wa miaka 42, bali kwa wanawake wenye umri mkubwa zaidi kuanzia miaka 45, baadhi ndio huwa na uwezekano wa kupata watoto wenye upungufu huo.

“Si lazima suala hili kutokea, kwani nimewahi kuona mwanamke mwenye  na umri wa miaka 54 akiwa amezaa mtoto wa kawaida kabisa.

Lakini ni vema ikafahamika kwamba uwezekano wa mwanamke kuzaa mtoto mwenye upungufu umri ukiwa umekwenda, ni mkubwa zaidi kuliko anayezaa katika umri mdogo,” anasema.

Kuhusu utasa, anasema mtoto kuzaliwa akiwa na upungufu wowote huweza kutokana na matatizo mengine, licha ya ukweli kwamba watoto wenye tatizo la ‘down syndrome’ ambao huzaliwa na wamama wenye umri mkubwa, huweza kuwa na tatizo la utasa.

Hivyo anafafanua kwamba, utasa si lazima likawa ni tatizo la msingi, lakini upo uhusiano unaotokana na upungufu anaozaliwa nao mtoto.

“Hivyo kuhusu utafiti huo, siwezi kukanusha ama kuthibitisha, kwani sijakutana na utafiti ukieleza bayana kuhusiana na tatizo hilo,” anasema Dk. Chapa.

Hivyo ni muhimu kwa wanawake kufuata ushauri wa wataalamu kuhusu suala la uzazi bora na salama, kabla ya kuchukua uamuzi, hususan kuchelewa kuzaa.

No comments