Breaking News

OPERESHENI ZA UZAZI ,CHANZO MAUMIVU YA MGONGO
 Operesheni za uzazi, chanzo maumivu ya mgongoNA MWANDISHI WETU

MGONGO ni sehemu ya mwili ambayo huuwezesha kuwa na umbile maalumu linalowezesha mwili kusimama ikiwemo kuulinda uti wa mgongo ambao ni rahisi kudhurika.

Pia mgongo ni kiunganishi cha kichwa na kiwiliwili na mahali unapoishia, hufanyika kiungo muhimu kumwezesha binadamu kutembea.
Endapo mgongo utaathirika kwa namna yoyote na kupata maumivu, mgonjwa hatahisi chochote maeneo ya makalio au miguu, matokeo yake kushindwa kujongea ipasavyo.

Dk. Joseph Ndali wa Kituo cha Afya cha Kimara (KHC), anaeleza kuhusu maumivu ya uti wa mgongo na kusema huambatana kupungua uzito na homa.

Maumivu ya mgongo ni moja ya matatizo ya kiafya yanayojitokeza mara kwa mara na huathiri zaidi misuli na mifupa ya mgongo wa binadamu.

SABABU
Anataja sababu za maumivu ya mgongo kwamba hutegemea shughuli mtu anazofanya. Kwa mfano, kukaa muda mrefu kwenye kiti chenye urefu wa sentimeta 30 na kufanya shughuli kama kupiga chapa, kazi za kuinama muda mrefu, dalili ya malaria na kukaa muda mrefu safarini.

Anasema wasafiri wanaoathirika zaidi ni wale wanaotumia njia za barabara zisizo na viwango, zenye mashimo na matuta mengi.

“Wanawake wengi zaidi hupatwa na tatizo la maumivu ya uti wa mgongo ikilinganishwa na wanaume, kutokana na suala la uzazi, kwa kuwa ukaaji wa mtoto tumboni huweza kuumiza mgongo.Mama anapaswa kupumzika kwa muda usiopungua miezi mitatu baada ya kujijifungua, hapaswi kufanya shughuli zozote nzito, ili kuepuka tatizo hili,” anasema.

Anasema umuhimu wa kupumzika unatokana na kutumia nguvu nyingi wakati wa kujifungua, mtoto anapokuwa katika harakati za kutoka tumboni hugusa mishipa ya fahamu, hivyo kuusababishia mgongo usumbufu.

Hata hivyo, daktari huyo anaelezea kuanza ghafla kwa maumivu ya mgongo wakati mwingine huweza kuwa ni dalili ya kuumwa magonjwa mengine hususan ugonjwa wa malaria.

Pia huenda ikawa ni dalili za ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo na si maumivu ya kawaida ya mgomgo.

Hivyo ni vema kuwahi hospitali kwa ajili ya kuchunguza afya na kubaini tatizo halisi, iwapo ni mgongo wenyewe ama ni dalili za magonjwa mengine.

Tatizo la maumivu ya uti wa mgongo, Dk. Ndali anaeleza kwamba huweza kutokana na maambukizi ya bakteria au aina fulani ya virusi.

“Mara nyingi maambukizi ya bakteria hudhihirisha ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo, ikiwa ni virusi huweza kuwa malaria au uti wa mgongo kuvimba na kusababisha maumivu,” anasema.

Pia kwa wanaojifungua kwa njia ya operesheni, husababisha maumivu ya mgongo kutokana na nevu kuguswa.

Anataja sababu zingine za kuumwa mgongo kuwa ni uzito uliopitiliza, ambapo mara nyingi watu wa aina hii hawafanyi mazoezi.

 Anaelezea kuhusu ugonjwa wa homa ya uti wa mgongo kuwa ni uvimbe wa tando za uti wa mgongo na ubongo ambao husababishwa na virusi.

Anasema ugonjwa huo unaweza kusababisha kifo kwa kuwa uvimbe huo hufanyika katika karibu na ubongo.

Anatajha dalili zake kuwa ni kuumwa kichwa, shingo, kupata homa, kuchanganyikiwa akili na kutostahimili mwanga.

TIBA
Mtu anayeumwa mgongo, anapaswa kufanya mazoezi kwa kuwa husaidia kwa kiasi kikubwa kutibu tatizo hilo.

Anaiasa jamii kuacha tabia ya kubweteka kwa kuwa kufanya hivyo huleta maumivu ya baadhi ya viungo vya mwili.

Anashauri kutembea umbali fulani kwa siku, pia kuwa ni mazoezi mazuri

Wanaume wengi ni watu wa mazoezi kutokana na shughuli wanazofanya, ambazo zinatumia nguvu nyingi, isipokuwa wanaofanya kazi zilizoorodheshwa hapo juu.

Dk. Ndali anashauri kuwahi hospitali pindi tatizo linapoanza kwani takwimu zinaonyesha kuwa tatizo hili Iinawaathiri takribani asilimia 40 ya watu wte nchini, ambapo asilimia 12 kati yao wana maumivu sugu ya zaidi ya wiki 12, wanaporipoti hospitalini.

Hata hivyo, asilimia 40-90 ya wagonjwa wenye maumivu ya mgongo huweza kutibiwa na kupona kabisa, iwapo mgonjwa atatibiwa chini ya wiki sita tangu kuanza kuugua.

DALILI
Dk. Ndali anasema mara nyingi mtu huhisi maumivu pindi anapoanza kunyanyua kitu, kunyanyuka na kupiga hatua, kujigeuza wakati amelala au kujinyoosha mwili.

Maumivu ya mgongo hujitokeza zaidi kwa watu wenye umri kuanzia miaka 25 hadi 40 na kuendelea, kwa mujibu wa daktari huyo kwani ndiyo mara nyingi wanaofika hospitali kutibiwa tatizo hilo.

Wastani wa wagonjwa wanaofika katika kituo hicho kutibiwa tatizo hilo ni wanne kwa siku, ambapo hugundulika na shida mbalimbali ikiwemo malaria.

Pia takwimu zinaonyesha nusu ya wagonjwa hupata maumivu makali kadri siku zinavyokwenda kabla ya kutibiwa.

“Maumivu yakiwa sugu, husababisha matatizo mengine ikiwemo kukosa usingizi wakati wa usiku, kusinzia wakati wa mchana kutokana na kutolala ipasavyo usiku.

Watu wenye umri mkubwa zaidi hupata tatizo la maumivu ya mgongo ambayo huweza kukomaa na kuwa sugu.

Mara nyingi chanzo cha maumivu hayo hakifahamiki mapema, lakini kitaalamu hutokana na kujeruhiwa kwa misuli au mifupa ya mgongo, kama ilivyoelezwa awali.

Miriam Samuel (66), anaeleza  namna maumivu ya mgongo yanavyomtesa, kwa miaka 11 sasa.
“Nilianza kidogo kidogo kuumwa mgongo, baadaye nilianza matibabu ambapo hadi sasa nimeshatibiwa hospitali nyingi lakini sijapona kabisa,” anasema Miriam.


Anasema amepata ushauri wa aina nyingi kutoka kwa watu tofauti ikiwemo wataalamu wa afya, amejitahidi kuzigatia, badala yake anapata nafuu tu na si kupona kabisa.

Emmanuel Maganga (71), ni miongoni mwa watu wanaoumwa mgongo, anasema anachukulia tatizo hilo kuwa ni miongoni mwa hatua katika maisha ya mwanadamu.

“Nilianza kuumwa mgongo tangu nikiwa na umri wa miaka 46, nafanya mazoezi kila mara na kutumia dawa za maumivu, napata nafuu na wakati mwingine tatizo linarudi,” anasema.

Upo usemi usemao ‘kinga ni bora kuliko tiba’, ni vema kuwahi kuwaona wataalamu wa afya kabla tatizo halijazidi, badala kusubiri lifikie katika hali mbaya.

Matibabu ya aina zote yanapatikana hivi sasa katika hospitali mbalimbali nchini, kufuatia maendeleo ya teknolojia, vipo vipimo vya kisasa.

Hivyo, inapaswa kuwahi hospitali na kufuata ushauri wa daktari baada ya kubainika na tatizo la aina yoyote.


No comments