Breaking News

UBUNGO YAWEKA HISTORIA, YAZINDUA RASMI MIKOPO YA WANAWAKE NA VIJANA YENYE THAMANI YA TSH 1.9 BILIONI


NA MWANDISHI WETU

Katika kuhakikisha wananchi wa Ubungo wanawezeshwa kiuchumi Halmashauri ya Manispaa ya Ubungo leo imeweka historia ya kuzindua rasmi utoaji wa mikopo ya wanawake na vijana katika viwanja vya Barafu Mburahati Wilaya ya Ubungo Jijini Dar es Salaam.
Akizindua mikopo hiyo Mgeni rasmi, Naibu Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI *Mh.  Joseph Kakunda* kwa niaba ya Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais TAMISEMI *Mh. Selemani Jafo* ameipongeza Halmashauri ya Manispaa Ubungo kwa kuwa mfano wa kuigwa licha ya uchanga wa Manispaa hiyo imeweza kutenga asilimia 10 ya mapato yake ya ndani nakufikisha kiasi cha Tsh *1.9 Bilioni* kwa ajili ya Wanawake na Vijana. Na katika mchakato ujao ameuagiza Uongozi wa Manispaa kuhakikisha wanatenga fedha kwa ajili ya vikundi maalumu vya walemavu na wenyewe wapate mikopo hiyo waweze kujikwamua kiuchumi.

Sambamba na hilo Mh. Kakunda ameahidi kumwagiza Katibu Mkuu TAMISEMI kuandika barua ya pongezi kwa Manispaa ya Ubungo Kwa kuwa Manispaa ya mfano kwa kutenga kiasi kikubwa cha fadha licha ya kuwa ndio kwanza ina takribani mwaka mmoja na miezi kadhaa.Pia kuanzia bajeti ijayo ya mwaka wa fedha ameziagiza Halmashauri zote nchini kuhakikisha zinatenga sehemu ya Mapato yake ya ndani asilimia 10 kwa ajili ya wanawake na Vijana na itakuwa moja ya kigezo cha kupima utendaji kazi wa viongozi katika Halmashauri husika.

Katika uzinduzi huo mgeni rasmi alikabidhi hundi mbili za mfano kwa vikundi viwili. Kikundi cha kwanza ni kikundi cha vijana Mabu Group ambacho kilipokea hundi ya Tshs milioni saba kwa niaba ya vikundi vya vijana. Kikundi cha pili ni Energy Women Group ambacho kilipokea hundi ya Tshs milioni 18.2. Katika kiasi kilichotengwa, vikundi 365 vinatarajia kufaidika na mkopo huo.Amesisitiza wanawake na vijana  wa Manispaa ya Ubungo kutumia fursa hiyo  kwa kuwa itawaongezea kipato na baadae kuwa na jamii yenye wanawake na Vijana wenye Ustawi.


Kwa upande wa Uongozi  wa Manispaa ya Ubungo Mh. Joseph Kakunda amewaagiza kuhakikisha wanatenga maeneo zaidi hata kwa kufidia ili vijana na wanawake wapate sehemu za kufanya biashara kwa amani.

Lakini pia amewataka CRDB kwa kuwa ndio weliopewa dhamana ya Kutoa mikopo hiyo, mikopo itolewe kwa utaratibu mzuri kusiwe na kero ya aina yoyote.

Naye mkurugenzi wa Manispaa ya Ubungo Ndg John Kayombo wakati akitoa taarifa ya mikopo hiyo amesema yeye kwa kila pesa inayoingia katika Manispaa kabla ya matumizi yeyote anatenga kabisa asilimia 10 kwa ajili ya Mikopo ya wanawake na vijana.


Aidha Mkuu wa Wilaya ya Ubungo Mhe.Kisare Makori alimshukuru Naibu Waziri kwa kuitikia wito wa kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi huo. Aliongeza kuwa Halmashauri ya Manispaa ya  Ubungo itaendelea kuwa mfano wa kuigwa kwa Halmashauri nyingine na itahakikisha inatenga asilimia 10 ya vijana na kinamama katika mapato yake ya kila mwaka wa fedha.

Meya wa Manispaa hiyo, Boniface Jacobo, alisema mikopo hiyo ni kwa wote ambao wamekidhi vigezo vya ujasiliamali.

‘’ Mikopo hiyo haingalii dini kabira wala vyama ni kwa watu wote ambao wamekidhi vigezo na ambao ni wakazi wa manispaa hiyo,’’alisema.

No comments