Breaking News

WANAWAKE WENYE WAPENZI WENGI KUPATA SARATANI YA KIZAZI


Wanawake wenye wanaume wengi,
hatarini kupata saratani ya shingo ya kizazi.

NA MWANDISHI WETU.

SARATANI ya shingo ya kizazi (cervical cancer) ni ugonjwa unaoshambulia shingo ya kizazi (cervix), sehemu inayounganisha tumbo la uzazi na uke.

Aina hii ya saratani husambaa toka shingo ya kizazi na kuathiri pia njia ya uke, kibofu cha mkojo, njia ya haja kubwa, tezi zilizopo katika nyonga na huweza  kufika sehemu ya mbali zaidi.

Dk. James Chapa, Mtaalamu wa Magonjwa ya Wanawake na Upasuaji wa Fistula katika Hospitali ya CCBRT, Dar es Salaam, anauelezea ugonjwa huu kwamba ni aina ya saratani inashika nafasi ya pili kwa kuathiri wanawake wengi duniani.

Pia, anabainisha kuwa ndiyo inayoongoza kwa kusababisha vifo vingi vya wanawake duniani, ambapo takribani asilimia 85 ya vifo hivyo hutokea katika nchi zinazoendelea.
Kwa hapa nchini saratani ya shingo ya kizazi ndiyo inayoongoza kwa kuathiri na kuua wanawake wengi zaidi.
Dk. Chapa anataja aina hii ya saratani kwamba huchangia asilimia 30 ya wagonjwa wote wa saratani wanaopata matibabu katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Takimu zinaonyesha kuwa wagonjwa zaidi ya 7,000, wanagundulika na saratani ya shingo ya kizazi nchini, kila mwaka ambapo 6,000 kati yao hufariki dunia.

Hata hivyo, anasema inakadiriwa kwamba kufikia mwaka 2025, kutakuwa na wagojwa zaidi ya 12,000, na vifo 9,000 kwa mwaka.
Kuhusu kundi linaloathirika zaidi na ugonjwa huo, daktari huyo anasema ni wanawake walio katika umri wa uzazi.

Hata hivyo, anasema asilimia 50 ya wanaogundulika kuwa na tatizo hilo ni wanawake wenye umri wa zaidi ya miaka 65.
“Umri mwingine unaoathirika zaidi ni ule wa kati miaka 40 hadi 50, kwa hiyo ugonjwa huu kwa upande wa umri una vilele viwili, kile cha umri wa kati na umri wa juu,” anasema.

DALILI

Dk. Chapa anataja dalili za saratani ya shingo ya kizazi, kuwa ni kutokwa damu ukeni ambayo si ya hedhi, hutoka katika shingo ya kizazi hususan inapoguswa wakati wa kujamiiana au wakati wa kujisafisha sehemu za siri.

Dalili zingine ni mwanamke kutokwa na maji yenye harufu kali katika sehemu zake za siri ikiwemo kupatwa na maumivu kwenye nyonga (iwapo saratani imesambaa) na  mwanzoni huwa haileti maumivu.

Anasema mwanamke anaweza kupatwa na tatizo la upungufu wa damu iwapo imetoka kwa wingi, ambapo  moyo kwenda kasi kuliko kawaida na kuchoka sana ni miongoni mwa dalili za ugonjwa huo.

“Kutokwa haja kubwa au ndogo ama zote kwa pamoja bila kujijua, ni miongoni mwa dalili za saratani hii, iwapo itakuwa imesambaa kufikia kwenye njia ya haja kubwa au kibofu cha mkojo,” anasema.

Pia, kutapika sana na kuvimba mwili humtokea mgonjwa iwapo saratani ya shingo ya kizazi itakuwa imeathiri figo.
ATHARI
Mtaalamu huyo wa magonjwa ya wanawake na upasuaji wa fistula, anataja athari zinazotokana na saratani ya shingo ya kizazi kuwa ni mgonjwa kupata fistula.

“Hutokea katika njia ya haja kubwa na ndogo, inaposambaa kwenda kwenye kibofu cha mkojo au njia ya haja kubwa,” anasema.

Anataja athari ingine kuwa ni kufeli kwa figo, kutokana na saratani hiyo kusamba kwenye nyonga ambapo huifanya mirija ya mkojo kushindwa kupitisha mkojo ipasavyo, mkojo huo hujaa katika figo na kuziua.

Saratani ya shingo ya kizazi inaweza kusababisha kifo kama isipogundulika na kutibiwa katika hatua za awali.
SABABU
Kirusi aina ya ‘Human Papilloma’ (HPV), ndicho kisababishi kikuu cha saratani ya shingo ya kizazi kinachoenezwa kwa kujamiiana bila kutumia kinga.

Hata hivyo, daktari huyo anasema zipo aina nyingi za virusi jamii ya HPV, kwa Tanzania kirusi aina ya ‘HPV 16’ husababisha takriban asilimia 41 ya saratani zote za shingo ya kizazi.

Aina nyingine ya virusi vya HPV vinavyosababisha saratani ya shingo ya kizazi ni HPV 18, 31 na 45.

Dk. Chapa, anataja hali ambazo ni hatarishi kwa mwanamke kuweza kupatwa na ugonjwa huo kuwa ni kushiriki tendo la ndoa na wapenzi wengi bila kutumia kinga.

“Kushiriki tendo la ndoa katika umri mdogo (miaka 16 au chini), kuzaa watoto wengi (7 au zaidi) na kutumia dawa za uzazi wa mpango, hususan vidonge kwa zaidi ya miaka 10, husababisha aina hii ya saratani,” anasema.

Vile vile, uvutaji wa sigara, upungufu wa kinga mwilini kwa sababu yoyote ikiwemo upungufu unaosababishwa na virusi vya ukimwi, huweza kusababisha saratani ya shingo ya kizazi.

KINGA

Dk. Chapa anasema aina hii ya saratani ni miongoini mwa saratani zinazoweza kukingwa zisitokee.

Kinga inahusisha kuepuka hali hatarishi ikiwemo kuingia katika masuala ya uzazi katika umri sahihi ambao ni miaka 18 au zaidi, kutojamiiana katika umri mdogo na kupanga uzazi.

Daktari huyo anashauri kwamba ni muhimu kutumia kinga wakati wa kujamiiana, kuwa waaminifu katika uhusiano na kuepuka matumizi ya tumbaku na sigara.

MATIBABU

Matibabu ya saratani ya shingo ya kizazi hufanywa kwa kutumia mionzi na dawa za mishipani na yanapatikana katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road.

Dk. Chapa anasema chanjo dhidi ya virusi vya HPV inapatikana nchini, na hufanya kazi vizuri zaidi zinapotolewa kabla mwanamke au msichana hajaanza masuala ya kujamiiana.

Anataja umri muafaka wa kupatiwa chanjo hiyo kuwa ni kati ya miaka 9 hadi 15, lakini pia huweza kutolewa hadi miaka 25, na kwa yeyote ambaye hajapata maambukizi ya virusi hivyo.

Uchunguzi na tiba ya viashiria vya saratani unajulikana kwa lugha ya kitaalamu ‘pre-malignant cervical lesion’ na ni  upimaji unaofanywa kwa kutumia vipimo kama ‘pap-smear’, na pia ‘VIA’ na ‘VILI’.

Anasema njia hizo mbili za mwisho ni rahisi na hufanywa hata katika vituo vya afya kama zahatani, havina gharama kubwa na yeyote anaweza kumudu uchunguzi huu.

Daktari huyo anasema, mgonjwa akifanyiwa uchunguzi na kugundulika na viashiria vya saratani, hutibiwa na kumuepusha kupata saratani ya shingo ya kizazi.

USHAURI

Kuepuka hali hatarishi kama ilivyoshauriwa kwenye kinga, Dk. Chapa anawataka wanawake kujenga tabia ya kuchunguza afya zao ikiwemo ya shingo ya kizazi.
Early treatment to prevent cervical cancer

“Ni muhimu kuwahi hospitali mapema mara mtu anapogundua mojawapo ya dalili za saratani hii ambayo inazo hatua kuu nne na ikigundulika mapema hutibiwa na kupona kabisa hasa katika hatua za kwanza na ya pili,” anasema.

Anasema mgonjwa akichelewa kupata matibabu na saratani kufikia hatua za juu za ugonjwa, uwezekano wa kutopona ni mkubwa.
Mary Nangali, mkazi wa Makongo, Dar es Salaam, anayepatiwa huduma katika Taasisi ya Saratani ya Ocean Road, anaeleza kwamba anaugua ugonjwa huo kwa muda wa miezi minane sasa.

“Ugonjwa huu umevuruga ndoto maishani mwangu, kwani hivi sasa nipo kitandani tu nikiugua, napata maumivu makali kwenye nyonga, nawashukuru madaktari wanajitahidi kunipatia huduma nzuri,” anasema.

Anna Ndimbo, mkazi wa Temeke, Dar es Salaam ni mgonjwa mwingine anayetibiwa hospitalini hapo, anasema amechelewa kupatiwa matibabu ya saratani kutokana na kutogundua mapema alichokuwa anaumwa.

“Namuomba Mwenyezi Mungu anisaidie nipone, lakini kwa sasa hali bado si nzuri, kuhusu uhusiano wa kimapenzi, ni kweli niliolewa na kuachika mara kadhaa (si ndoa, kuishi kinyumba) na baadae kuamua kuwa na wapenzi tu lakini sio wa kuishi nao,” anasema.

Hivyo, ni wajibu wa kila mtu kufata ushauri wa wataalamu wa afya ili kuepuka magonjwa kupatwa mbalimbali.

Ni muhimu kupima afya kila mara na kufuata mtindo wa maisha ambao ni sahihi.
Mwisho

No comments