Breaking News

WANANCHI WILAYANI KISARAWE, MKOA WA PWANI WAMPONGEZA JPM KWA KUIAGIZA DAWASA IWAPATIE MAJI YA UHAKIKA. WAKABIDHI FIMBO MAALUMU ILI ITUMIKE KWA AJIRI YA KUCHAPA MAFISADI KABLA YA KUFUNGWA GEREZANI

 MKUU wa Mkoa wa Pwani, Mhandisi Everist Ndikilo, (kushoto), akipokea fimbo maalumu kutoka kwa mzee Kondo Mwele, kwa niaba ya Rais, Dk. John Magufuli, ili itumike kwa ajili ya kuwachapa mafisadi
 WANANCHI WILAYANI KISARAWE, MKOA WA PWANI WAMPONGEZA JPM KWA KUIAGIZA DAWASA IWAPATIE MAJI YA UHAKIKA. YAMZAWADIA FIMBO MAALUMU ILI  ITUMIKE KWA AJIRI YA KUCHAPA MAFISADI KABLA YA KUFUNGWA GEREZANI.
 NA MWANDISHI WETU.
BAADHI ya wananchi wa wilaya ya Kisarawe, mkoani Pwani wamempongeza Rais, Dk. John Magufuli kwa kuiagiza Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA), kuipatia maji ya uhakika wilaya hiyo.
Walisema wilaya hiyo pamoja na kuwa na Ardhi nzuri inayofaa kwa kilimo na mambo mengine mengi, ilisahaulika kwa kipindi kirefu na hivyo kudumaa kiuchumi.
Kwa mujibu wa wananchi hao, kitendo cha Rais Magufuli kuiagiza DAWASA kupeleka maji ya uhakika, safi na salama ni cha kupongezwa kwani kitafungua ukurasa mpya wa kufufua uchumi wa wilaya yao.
“Lazima tumpongeza sana Rais wetu Magufuli kwa uamuzi wake huu. Sisi tutazidi kumwombea ili awe na afya njema na familia yake aweze kuwatumikia wananchi kwa uadilifu huu anaokwenda nao,” alisema Asha Juma.
Pongezi hizo zilitolewa jana kwa nyakati tofauti wakati wa hafla ya kutia saini mkataba wa ujenzi wa mradi wa kulaza bomba la maji na matenki kutoka Kibamba hadi Kisarawe Mkoani Pwani.
Katika hafla hiyo iliyofanyika wilayani humo, Mamlaka ya Majisafi na Majitaka Dar es Salaam (DAWASA) ilitiliana saini mkandarasi China Henan International Cooperation Group mkataba wa ujenzi wa mradi wa kulaza bomba la maji na matenki kutoka Kibamba hadi kisarawe mkoani Pwani kwa gharama ya sh. Bilioni 10.8.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Halmashauri ya Wilaya ya Kisarawe Khamis Dikupatile, alisema kutiwa saini mkataba wa mradi huo kumeweka historia wilayani humo.
Alisema wilaya hiyo ina tatizo sugu la upatikanaji wa maji safi na salama ambapo wananchi wamekuwa wakinunua maji kutoka kwa wafanyabiashara na pindi wanapokosa fedha za kununulia maji hayo, hutumia ya kwenye visima visivyo salama.
“Mheshimiwa Waziri wa maji tunakuomba ufikishe salamu zetu kwa mhe Rais Mgufuli. Mwambie tunamshukuru sana kwa jambo hili la kutupatia maji, lakini pia tunakuomba ukamwambie kwamba shukrani tupu hazitoshi.
“Sisi wazazi wake wa Kisarawe, tunamuita aje huku atutembelee ili tuweze kumuombea.Tumshike kichwa awe salama aendelee kuwatumikia wananchi,” alisema Dikupatile.
Alisema wananchi wa wilaya hiyo usiku wa kuamkia juzi hawakuamini maishani mwao baada ya kusikia gari la matangazo likipita mitaani na kutanza kwamba kesho (jana) kutakuwa na hafla ya kutiliana saini mkataba wa ujenzi wa bomba la maji.
Kwa mujibu wa Dikupatile, tangazo hilo sio kwamba lilishtua wengi, bali lilileta mshangao kwa kila mwananchi maana haikuwa jambo la kawaida kutokea.
“Lakini pia niwashukuru na kuwasifu DAWASA kwa utendaji wao mzuri na kutimiza kwa wakati agizo la Rais Magufuli.
“Hatukutemea kama wenzetu hawa wangefanya haraka kutafuta fedha za mradi huu na leo hii tunashudia wakitiliana saini mkataba,” alisema.
Alisema kitendo hicho ni cha kiungwana sana kwa wananchi wa Kisarawe na kwamba wanawapa ushirikiano wa karibu katika kuutekeleza mradi huo.
Naye Mzee Kondo Mwele, alisema Rais Magufuli ni kiongozi wa aina yake ambaye hajawahi kutokea hivyo auungwe mkono na kila mmoja na kuzidi kumwombea na familia yake.
Alisema kitendo cha kupambana na mafisadi na kuwabana kila kona si cha kawaida bali kinahitaji ujasiri wa kutosha.
“Pamoja na kutupatia maji, namsifu na kumpongeza kutokana na kuwabana mafisadi mpaka yanashindwa kupumua.
“Kwa kuliona hili kama ni kikwazo katika uchumi wa nchi, ndio maana akaanzisha na kujenga mahakama za mafisadi,” alisema.
Hata hivyo, alisema mahakama hizo peke yake hazitoshi na badala yake amemzawadia fimbo yenye jina lake (Magfuli), kwa ajili ya kuwachapa bakora mafisadi kabla ya kwenda kutumikia kifungo gerezani.
“Hii fimbo nakukabidhi umpelekee. Ni fimbo maalumu yenye jina lake kwa ajili ya kuwachapa mafisadi kabla ya kwenda kutumikia kifungo,” alisisitiza mzee Mwele.
Alifafanua kuwa hatua hiyo ya kuwabana mafisadi imesaidia kwa kwa kiasi kikubwa kukua kwa uchumi wa nchi.
MHANDISI Ndikilo akiwaonyesha waandishi wa habari fimbo hiyo jana, iliyoandikwa jina la JPM. Kulia ni Mbunge wa Viti Maalumu Zainab Vullu.
VIONGOZI mbalimbali waliyehudhuria hafla hiyo ya utiwaji saini mkataba wa mradi wa ujenzi wa kulaza bomba la maji kutoka Kibamba kwenda Kisarawe mkoani Pwani wakiwa katika picha ya pamoja.

No comments