Breaking News

TIMU YA SOKA YA SIMBA YASHINDWA KUWEKA REKODI YA KUCHUKUA KOMBE BILA KUFUNGWA MSIMU HUU BAADA YA KUPATA KIPIGO CHA BAO 1-0 NA TIMU YA KAGERA SUGAR TAIFA. RAIS MAGUFULI ATAKA SHIRIKISHO LA SOKA TANZANIA (TFF), BARAZA LA MICHEZO TANZANIA (BMT), VILABU NA VYAMA VYA MICHEZO KUWEKA MIKAKATI ITAKAYOWEZESHA TANZANIA KUSHIRIKI NA KUSHINDA MICHUANO YA KIMATAIFA.

 RAIS Magufuli akizungumza uwanja wa Taifa jana

 NA THOMAS MTINGE
TIMU ya Soka ya Simba jana ilishindwa kuweka rekodi ya kumaliza Ligi Kuu ya Vodacom Tanzania (Bara), bila kufungwa, baada ya kupata kipigo cha bao 1-0 na timu ya Kagera Sugar katika uwanja wa Taifa.
Aidha timu hiyo ya soka ya Simba ambayo jana ilikabidhiwa rasmi na Rais John Magufuli Kombe la ushindi katika kipindika cha mwaka 2017/2018, iliweka historia kwa mara ya kwanza kufungwa mbele ya Rais, Dk. John Magufuli, Akizungumza uwanjani hapo, Rais, Magufuli ametoa wito kwa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), Baraza la Michezo Tanzania (BMT), vilabu na vyama mbalimbali vya michezo kuweka mikakati itakayoinua kiwango cha michezo na kuiwezesha Tanzania kushiriki na kushinda michuano ya Kimataifa.
Akiwa uwanjani hapo, Rais, Magufuli alikabidhiwa kombe la mabingwa wa michuano ya soka ya nchi za Afrika Mashariki na Kati (CECAFA) kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 17 baada ya timu ya Tanzania (Serengeti Boys) kuibuka mabingwa huko nchini Burundi.
Pia, alipokea timu ya soka ya watoto wa kike waishio katika mazingira magumu (Tanzania Street Children – TSC) ambayo imeibuka washindi wa pili katika michuano ya dunia iliyofanyika nchini Urusi na kukabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu ya soka Tanzania (Bara), kwa timu ya Simba Sport Club ya Dar es Salaam.
Rais Magufuli alisema Watanzania wanataka kupata furaha kwa kuona timu zao zinashinda na kwamba wamechoka kuona timu zao za Taifa na vilabu vinavyowakilisha katika michuano ya kimataifa vinafanya vibaya.
Aliahidi kuwa Serikali itashirikiana na wadau wote wa michezo kukuza michezo na alitaka katika michuano ya Soka ya Afrika (AFCON) kwa vijana wa umri wa chini ya miaka 17 itakayofanyika mwezi Aprili 2019 ambapo Tanzania itakuwa mwenyeji, Tanzania ionyeshe mfano kwa kuhakikisha ubingwa unabaki hapa nchini.
“Michezo ni furaha, michezo ni afya, lakini pia michezo ni biashara, umefika wakati sasa tukuze michezo yetu, na Serikali ipo tayari kuunga mkono juhudi za kuendeleza michezo” alisisitiza Rais Magufuli.
Kabla ya kuzungumza na wanamichezo Rais Magufuli na viongozi mbalimbali wakiwemo Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk. Harrison Mwakyembe, Naibu Waziri wake, Juliana Shonza na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam Paul Makonda, walishuhudia pambano la ligi kuu ya soka Tanzania bara ambapo mabingwa wa ligi hiyo Simba walipata kipigo cha bao 1- 0 na timu ya Kagera Sugar ya Kagera.
Hata hivyo, katika mchezo huo, Rais Magufuli alionyesha furaha yake kwa Watanzania kwa kuwaeleza bayana kuwa yeye (Magufuli), ni shabiki wa soka nchini na timu yake ni zile za Taifa.
Alisema anapenda sana michezo na amekuwa akifuatilia kwa karibu na mwishoni mwa wiki iliyopita aliangalia mechi ya Barcelona ya Hispania ambayo ilitwaa ubingwa kwa staili kama ya Simba.
Aliongeza kwa kusema licha ya kupenda michezo huwa hapendi kuona timu za Tanzania zikifanya vibaya kwani huchanganyikiwa na kusema anachotaka sasa ni kuona timu zote zitakazoshiriki michuano ya kimataifa zikifanya vyema."
Natamani siku moja niitwe uwanjani kukabidhi au kukabidhiwa kombe la Afrika ambalo timu zetu za Simba, Yanga au timu za taifa zimeshinda hivyo naitaka Simba iwe timu ya kwanza kutwaa ubingwa huo licha ya kuwa kwa mchezo niliouona leo hamuwezi kushinda taji

hilo na hao Yanga nataka nikiwaona wakifanya vizuri katika mashindano ya Kombe la Shirikisho," alisema.Rais Magufuli alisema hatasita kufika uwanjani kama timu yeyote itafanya

vizuri na kusema leo (jana) amekwenda uwanjani kwa kuwa Simba imekuwa ikishinda tangu ligi hiyo ianze licha ya kuteleza katika mchezo wa jana. Licha ya kuipongeza Simba, Rais Magufuli aliipongeza Kagera Sugar na kusema imecheza vyema nakuonyesha soka maridadi mbele ya mabingwa hao.
Akizungumzia ushiriki wa timu ya Serengeti Boys, Rais alisema alikuwa akifuatilia michuano ya Kombe walilochukua kule Burundi na kuipongeza timu hiyo huku akiipongeza timu ya wachezaji waishio kwenye mazingira magumu kwa kushika nafasi ya pili katika mashindano ya dunia yaliyomalizika wiki iliyopita
nchini Russia. 
"Nafurahi sana nikiona timu zikishinda na nina furaha zaidi baada ya kuona msimu huu hakuna timu iliyokwenda Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kudai pointi kama ilivyokuwa huko nyuma,"alisema Rais Magufuli.
Pia, aliupongeza uongozi wa sasa wa TFF chini ya Rais Wallace Karia kwa kuonyesha mabadiliko makubwa ya uendeshwaji wa soka la Tanzania na kusema serikali inaunga mkono jitihada zinazofanywa na uongozi wa shirikisho hilo kwa kuendeleza soka na kuliweka katika mstari nyoofu.
"Serikali ya awamu ya tano itaendelea kuwekeza katika michezo kwa vile inatambua kuwa michezo ni ajira na biashara ambayo ni mkombozi kwa vijana  hivyo, itaendelea kushirikiana na vyama vyote vya michezo ili timu za taifa ziweze kufanya vizuri katika michezo ya kimataifa,"aliongeza.
KASEJA AMNYENYUA KITINI RAIS MAGUFULINA.
Kipa mkongwe Juma Kaseja, alimnyanyua kitini Rais, Dk. John Magufuli, baada ya kupangua penalti ya nyota wa Simba ,Emmanuel Okwi.
Kaseja alipangua penalti hiyo dakika ya 88  baada ya George Kavila kumchezea faulo Okwi aliyekuwa eneo la hatari na hivyo kuondoa kabisa ndoto ya Simba ya kutaka kusawazisha bao walilofungwa na Kagera Sugar ili kuendeleza rekodi yake ya kutofungwa katika ligi ya mwaka huu.
Katika mchezo huo, Kagera Sugar iliibuka na ushindi wa bao 1-0, mchezo uliofanyika kwenye Uwanja wa Taifa Jijini Dar es Salaam,bao la ushindi la Kagera lilifungwa na Edward Christopher dakika ya 84. 
Awali, pambano hilo lilianza kwa kasi huku Simba wakianza kwa kulishambulia lango la Kagera katika dakika ya pili baada ya Okwi kumpa pasi safi Shiza Kichuya, lakini mpira aliopiga uliokolewa na mabeki wa Kagera Sugar.
 Kasi ya Simba ilizidi kupamba moto ambapo kama Kichuya, Said Ndemla na Okwi wangekuwa makini Simba ingeweza kupata bao la kuongoza baada ya kupata nafasi za wazi dakika 19, 23 na 32.
Dakika ya 43 Kagera Sugar ilipata nafasi kupitia kwa Japhary Kibaya ambapo alipiga shuti lililopanguliwa na kipa Said Mohamed kabla ya mabeki wa Simba kuondoa mpira langoni mwao.
Katika kipindi cha kwanza timu hizo zilikwenda vyumba vya mapumziko zikiwa suluhu ya bila kufungana.Kipindi cha pili, kilianza kwa kasi ambapo Simba ilifanya mashambulizi ya haraka haraka dakika ya 53 baada ya Okwi kuwatoka walinzi wa Kagera na kumpa pasi Kichuya ambaye alipiga mpira uliogonga mwamba wa goli kwa chini na kuokolewa na mabeki wa Kagera. 
Dakika ya 68 beki Salum Mbonde, ambaye aliingia kuchukua nafasi ya James Kotei aliumia na nafasi yake ilichukuliwa na John Bocco. 
Mchezo uliendelea kwa Simba kucheza nusu uwanja lakini, Kagera Sugar ilifanya mashambulizi ya kushtukiza ilipopata nafasi hali iliyozaa matunda kwani dakika ya 84 timu hiyo ilifanikiwa kupata bao lililowaacha wachezaji wa Simba wasiamini kile kilichotokea langoni mwao.
Bao hilo liliifanya Simba kujaribu hapa na pale kufanya mashambulizi na kufanikiwa kupata penalti ambayo haikuzaa matunda baada kipa wa zamani wa Wekundu hao wa Msimbazi Juma Kaseja kufanya "vitu vyake" kupangua shuti kali lililopigwa na Okwi. 
Simba iliwakilishwa na Said Mohamed, Nicholas Gyan, Muzamil Yassin, Mohamed Hussein, Paul Bukaba, James Kotei, Salum Mbonde, John Bocco, Erasto Nyoni, Jonas Mkude, Shomary Kapombe, Emmanuel Okwi, Said Ndemla na Shiza Kichuya.
Kagera Sugar: Juma Kaseja, Seleman Magana, Juma Nyoso, Mohamed Fakhi, Pete Mwalyanzi, Japhet Makalai, Ally Ramadhan, George Kavila, Japhery Kibaya, Edo Chris, Atupele Jackson na Omary Bada.
KAULI ZA MAKOCHA KABLA YA MCHEZO
Kabla ya mpambano huo Pierre Lechantre, alisema anawaheshimu Kagera Sugar.
Licha ya kukabiliwa na wachezaji wengi majeruhi bado alikuwa ana imani kwamba wachezaji wake wasingeruhusu kufungwa mbele ya Rais Dk. John Magufuli.
Kocha Mecky Mexime, wa Kagera Sugar alisema walipanga kuingia uwanjani hapo kwa nguvu zote na lengo lao likiwa ni kutibua ushindi wa Simba kwa kuwafunga kwa mara ya kwanza kwenye ligi hiyo kauli ambayo ilitimia .
HALI ILIVYOKUWA
Ulinzi ulikuwa mkali kabla ya mchezo huo ambapo mashabiki wengi walijitokeza huku rangi za nyekundu na nyeupe zikitawala.
Misururu ya foleni ilikuwa mikubwa ya kuingia uwanjani kwa ajili ya kushuhudia mpambano huo.
TIMU KUINGIA UWANJANI
Simba iliingia uwanjani saa 7.02 huku Kagera Sugar ikiingia uwanjani hapo na kuanza kupasha majira ya saa7.18.
Baada ya kupasha wachezaji wa Simba wakiongozwa na  Shomari Kapombe, John Bocco,Jonas Mkude,Paul Bukaba Mzamiru Yassin, Salim Mbonde na Emmanuel Okwi waligawa jezi zao kwa mashabiki.
RAIS DK. MAGUFULI KUWASILI
Rais Magufuli alifika uwanja wa Taifa majira ya saa 7.54 na kisha kukagua timu hizo  saa 8.07.
Alianza kuikagua Kagera Sugar huku akifuatana na Rais wa Shirikisho la Soka Tanzania(TFF) Walace Karia na baadae Simba.
MSAGA SUMU NA VITU VYAKE
Wakati wa mapumziko shamrashamra za Simba zilinogeshwa na msanii Msaga Sumu kwani alifanya onyesho la nguvu uwanjani hapo hata mwisho wa mchezo huo msanii huyo aliwapagawisha vilivyo  mashabiki.
KOMBE KUINGIA UWANJANI
Saa 9.25 kombe la ubingwa lilipelekwa uwanjani hapo kwa ajili ya kukabidhiwa kwa Simba.
KILIO
Kilio kwenye mchezo huo, kilikuwa kwa beki Salum Mbonde ambaye aliumia na nafasi yake ilichukuliwa na Bocco ambapo alitoka huku akilia kufuatia kuumia mara nyingine.
Pia, Okwi  alimwaga machozi baada ya kukosa penalti muda mfupi baada ya mpambano huo kumalizika.
MANAHODHA KUANZA BENCHI.
Kwenye mchezo huo, manahodha wa Kagera Sugar, George Kavila na John Bocco walianza benchi na kisha baadae kuingia uwanjani kucheza mpambano huo.
SHUJAA
Kwenye mchezo huo, alikuwa kipa Juma Kaseja ambaye alipopangua mpira wa penalti iliyopigwa na Okwi na kumfanya Rais Magufuli kunyenyuka kitini kutokana na kitendo cha kipa huyo kupangua shuti huku mashabiki wanaodhaniwa kuwa wa Yanga wakishangilia kwa nguvu.
SHABIKI AZIMIA
Kufuatia kipigo hicho,shabiki mmoja wa Simba alizimia uwanjani hapo na kubebwa kwenda kupatiwa huduma ya kwanza.
Hali hiyo ilitokea baada ya mwamuzi wa mchezo huo kupuliza kipyenga cha kumaliza mchezo huo.
KAULI YA MFUNGAJI
Edward Christopher mara baada ya mchezo huo, alisema anajisikia furaha kuiwezesha timu yake kupata ponti tatu na kuwa timu ya kwanza.
kuifunga Simba."Nashukuru Mwenyezi Mungu kwa kuweza kufunga bao la ushindi dhidi ya Simba,sasa tunaenda kujipanga na mechi zijazo,"alisema Christopher.
KICHEKESHO
Kwenye mchezo huo wa kukabidhiwa kombe,Shiza Kichuya aliingia uwanjani na mtoto ambaye ni rafiki yake.
 Kabla ya mchezo mtoto huyo alikuwa naye na baada ya mpambano huo walikuwa wote na mtoto huyo aliweza kupewa mkono na Rais Magufuli na kupiga picha wakiwa pamoja.
VIKOMBE
Wachezaji walioshiriki michuano ya Kombe la Dunia kwa watoto wa kike wanaoshi katika mazingira magumu walikabidhi kwa Rais Magufuli kikombe,
majira ya saa 10.48, baada ya hapo Serengeti Boys nao walikabidhi kikombe kwa Rais saa 10.50.
Lakini Kagera Sugar walipeana mkono na Rais Magufuli katika saa 10.52 baada ya kutibua rekodi ya Simba kutofungwa.
Wachezaji wote wa Simba  walipewa medali za dhahabu na Rais Magufuli ilikuwa saa
10.56.
Rais Magufuli alikabidhi kombe la ubingwa wa Ligi Kuu majira ya saa10.59 kwa John Bocco na kutawazwa kuwa mabingwa wa Tanzania (Bara) wa ligi ya msimu huu.

 

No comments