Breaking News

WAZIRI MKUU AHIMIZA MATUMIZI YA MIFUMO YA ULINZI WA MIJI YA KIELEKTRONIKI, MASAUNI, AMSHUKURU JPM UJENZI NYUMBA ZA POLISI. SIRRO ATOA ONYO KALI KWA WALIOPATA MSAMAHA WA RAIS.

WAZIRI Mkuu  Kassim Majaliwa,  akikata utepe kufungua Kituo cha Polisi cha Kiluvya Wilaya ya Kipolisi Ubungo. . Kutoka kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam ambaye pia ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Felix Lyaniva, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhadisi, Hamad masauni na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro. (Picha zote na Ofiosi ya Waziri Mkuu) 
WAZIRI Mkuu,  Kassim Majaliwa, ameiagiza Wizara ya Mambo ya Ndani  kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi waangalie umuhimu wa kutumia mifumo ya ulinzi wa miji ya kieletroniki (City Surveillance System) ili kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao.
Alitoa agizo hilo jana wakati akizungumza na mamia ya wananchi na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam na viongozi wa Jeshi la Polisi kwenye viwanja vya Mbweni, wilayani Kinondoni,  mkoani humo baada ya kuzindua vituo vya polisi vya kisasa vya Mburahati, Kiluvya-Gogoni na Mbweni.
“Katika suala zima la kuimarisha usalama, napenda niwape changamoto Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi ili zitoe kipaumbele kwenye matumizi ya City Surveilance System (CCTV). Usimikaji wa mifumo hiyo utasaidia kupunguza uhalifu na kuongeza usalama wa wananchi na mali zao,” alisema Majaliwa.
Waziri Mkuu alitoa mfano wa Jiji la Nairobi la Nchini Kenya, kuwa tayari linatumia mifumo ya aina hiyo hivyo, haoni ni kwa nini Tanzania bado haijawa na mifumo kama hiyo.
Alisema, uwepo wa mifumo hiyo, utasaidia si tu kutambua kwa wepesi wahusika wa matukio ya uhalifu kama vile ukwapuaji, wizi wa magari na uharibifu wa mali, bali pia utaongeza shughuli za kibiashara na utalii.
"Tanzania hatujaanza kutumia mifumo hii lakini, ifike mahali tuanze kubadilika. Tafuteni wataalamu wenye ujuzi watufungie mifumo hii ili iwe rahisi kufuatilia matukio mbalimbali. Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani fuatilia mifumo hii ili tuanze na majiji yetu na tuweze kufuatilia matukio ya kihalifu barabarani na mitaani.
"Nitoe rai kwa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Jeshi la Polisi wachukue hatua za haraka kurahisisha upatikanaji wa matumizi ya mifumo hiyo hususan katika majiji yetu kwa ajili ya kuimarisha usalama wa watu na mali zao," alisema Waziri Mkuu.
Mapema, Naibu Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Mhandisi Hamad Yusuf Masauni alimshukuru Rais, Dk, John Magufuli kwa kukubali kutoa kiasi cha sh.Bilioni 10 kwaajili ya ujenzi wa nyumba za polisi.
Alisema kutokana na fedha hizo, nyumba takriban 400 za askari polisi, zinatarajiwa kujengwa katika maeneo mbalimbali nchini.
Akitoa taarifa ya ujenzi wa vituo hivyo vitatu, Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro alisema ujenzi wa kituo cha Mburahati umegharimu sh. bilioni 1.2, Kiluvya (sh. milioni 227) na Mbweni (sh. milioni 667).
Alisema ujenzi wa vituo hivyo umeshirikisha wananchi wa maeneo husika, Jeshi la Polisi na wadau werevu ambao ni walipa kodi wazuri na wazalendo zikiwemo taasisi na watu binafsi.
Katika hatua nyingine, IGP, Sirro, alitoa onya kali kwa watu waliopata msamaha wa Rais, Dk. John Magufuli, Aprili 26, mwaka huu wajichunge tabia na matendo yao.
Alisema nia ya Rais Magufuli, kuwapa msamaha ilikuwa njema lakini, kuna baadhi ya watu wameitumia vibaya fursa hiyo na hadi sasa watu watano wamekwishauawa na wananchi kutokana na kujihusisha tena na vitendo vya uharifu.
 “April 26, mwaka huu, Rais aliwapa msamaha baadhi ya watu lakini, wameutumia vibaya msamaha huo na kuanza na kurejea kwenye matendo yao maovu na hadi sasa watu watano walishauawa na wananchi,” alisema IGP, Sirro.
 Alisema anatoa onyo kwa wote waliopata msamaha na kutataka kurejea kwenye matendo yao maovu. “Ukitoka gerezani kwa msamaha, maana yake umerekebisha mwenendo wako na wananchi wanatarajia uwe hivyo, lakaini kama ukifanya vinginevyo, Serikali isilaumiwe,” alionya.
 Akielezea kuhusu utendaji wa Jeshi la Polisi, Kamanda Sirro alisema tangu ashike madaraka hayo, jeshi hilo limewapeleka askari 1,267 kwenye mafunzo ya medani za kivita na kwamba jeshi hilo liko imara.
 “Pia, tumepeleaka askari wa upelelezi zaidi ya 1,000 kwenye mafunzo ya ujuzi na ustadi (skills and knowledge) wa kupeleleza kesi mbalimbali. Baada ya kuwapa mafunzo haya, tunataka kesi za kawaida upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi sita na zile kesi kubwa kubwa upelelezi wake uwe umekamilika ndani ya miezi 12. Tunataka kuhakikisha haki za Watanzania zinapatikana kwa wakati,” alisisitiza.
 Kamanda Sirro alitumia fursa hiyo kumshukuru Magufuli kwa kutoa kibali cha ajira kwa askari wapya 1,500 na kuwaruhusu wawapandishe vyeo askari wenye kustahili kuanzia cheo cha Koplo hadi Naibu Kamishna wa Polisi (DCP). 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akizungumza na Inspekta Jenerali wa Polisi, Simon Sirro baada ya kufungua Kituo cha Polisi cha Mbweni Wilaya ya Kipolisi  Kawe,
BAADHI ya mwananchi waliohudhuria katika ufunguzi wa Kituo cha Polisi cha Mbweni , j
Jijini Dar es salaam wakimsikiliza Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa wakati alipofungua kituo hicho,  
MAJALIWA na Sirro wakifurahia jambo.

MASAUNI akizunguza na wananchi katika mkutano huo.

No comments