Breaking News

WAZIRI MKUU ATAKA WANAOTOA TAARIFA ZA UONGO WADHIBITIWE.

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, ameliagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi wawachukulie hatua kali wananchi wote wanaotumia vibaya namba za mawasiliano za jeshi hilo kwa kutoa taarifa za uongo kuhusu matukio ya majanga ya moto.
Sambamba na hilo, aliiagiza Jeshi la Zimamoto na Uokoaji nchini kuendelea kutoa mafunzo kwa wananchi juu ya namna ya kujikinga na kupambana na majanga ya moto pindi yanapotokea katika maeneo yao.

WAZIRI  Mkuu, Kassim Majaliwa (kushoto), akizungumza na Kamishina Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji, Thobias Andengenye, wakati alipotembelea Kituo cha  Zimamoto za  na Uokoaji cha Mkoa wa Ilala eneo la Fire Jijini Dar es salaam juzi. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)

 Pia, aliziagiza halmashauri zote nchini kuwa na magari ya zimamoto pamoja na magari ya kubeba wagonjwa kwenye vituo vyote vya Zimamoto na Uokoaji katika maeneo yao.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo juzi wakati alipofanya ziara katika Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa pamoja na Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Mkoa wa Ilala, Dar es Salaam.
Alisema ili kudhibiti wananchi wanaopiga simu za kuomba msaada wa kutaka kuokolewa, huku kukiwa hakuna tukio lolote la janga la moto lililotokea kwenye maeneo yao, ni vema watu hao wachukuliwe hatua kali ili iwe fundisho kwa wengine wenye tabia kama hiyo.
 
WAZIRI Mkuu, Majaliwa, akizungumza na askari wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji wakati alipotembelea  Kituo cha Jeshi hilo cha Mkoa wa Ilala eneo la Fire Jijini Dar es salaam. Kushoto ni Kamishina Jenerali  wa Jeshi hilo, Thobias Andengenye.
Waziri Mkuu alitoa agizo hilo baada ya Kamishna Jenerali wa Jeshi la Zimamoto na Uokoaji,  Thobias Andengenye, kumweleza baadhi ya changamoto zinazolikabili jeshi hilo kuwa ni pamoja na wananchi kupiga simu wakidai kuna ajali ya moto imetokea katika maeneo yao na baada watu wa uokoaji kufika wanabaini ni uongo.
Hata hivyo, Waziri Mkuu aziagiza halmashauri zote nchini kuwa na magari ya zimamoto pamoja na ya kubebea wagonjwa kwa ajili ya kutoa huduma pindi majanga yanapotokea kwenye maeneo yao ili kuharakisha utoaji wa huduma za dharura.
Pia, alilitaka Jeshi hilo kuendelea kutoa elimu kwa wananchi ili kila Mtanzania aweze kuwa na uelewa wa kutoa huduma za awali pindi majanga ya moto yanapotokea katika maeneo yao ikiwa ni pamoja na kutumia vifaa vya kuzima moto.
Waziri Mkuu, ambaye alitembelea kituo cha Jeshi la Zimamoto cha Ilala, alijionea magari ya kuzimia moto likiwemo la aina ya Bronto Sky Lift lenye uwezo wa kufika futi 54 na kuzunguka nyuzi 360. 
Alielezwa kuwa katika Bara la Afrika, magari ya aina hiyo yapo matatu tu, ambayo yapo nchini Tanzania, Misri na Afrika Kusini. Kwa upande wa Tanzania, gari hilo lilinunuliwa miaka 10 iliyopita kwa sh. bilioni 1.5. 
 
 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akikagua baadhi ya vifaa, magari na mitambo inayotumiwa na Jeshi la Zimamoto na Uokoaji  wakati alipotembelea Kituo cha Zimamoto na Uokoaji cha Mkoa wa Ilala, eneo la Fire. Kushoto  kwake ni Kamishina Jenerali wa Jeshi hilo, Thobias Andengenye.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alitembelea Kituo cha Operesheni na Mawasiliano ya Dharura ya Maafa, ambapo aliwasisitiza viongozi wa kituo hicho kutoa elimu kwa wananchi juu ya madhara yatokanayo na kuishi kwenye maeneo hatarishi hususan mabondeni.
Waziri Mkuu alisema licha ya kuwapa elimu, pia wanatakiwa kuwashawishi wakazi wa maeneo hayo kuondoka kabla ya kutokea kwa maafa badala ya kusubiri majanga yatokee. Pia aliwataka wawe na mpango wa kuonesha eneo lenye maafa na kuujulisha umma.
Pia, aliwataka watendaji wanaohusika na kamati za maafa waimarishe mawasiliano katika ngazi zote kuanzia ya Kijiji hadi Taifa na wafanye kazi kwa ushirikiano ili kurahisisha utoaji wa huduma kwa wananchi pindi maafa yanapotokea.
Awali, Waziri Mkuualitembelea Ofisi za Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Jijini Dar es salaam ambapo mbali na mambo mengine, alijionea moja kati ya mitambo ya kwanza ya Mpiga  Chapa wa Serikali uitwao  Original Heidelberg wenye zaidi ya miaka 100 ambao bado unafanya kazi vizuri.

 
WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa, akitazama moja kati ya mitambo ya kwanza ya Mpiga  Chapa wa Serikali uitwao  Original Heidelberg wakati alipotembelea Ofisi za Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali Jijini Dar es salaam juzi. Mtambo huo wenye zaidi ya miaka 100 bado unafanya kazi vizuri.


MAJALIWA,  akipata maelezo  kutoka kwa Mohammed  S. Mohammed (kulia) ambaye ni Mtalaam na mwendeshaji  mkongwe wa mitambo ya uchapaji kuhusu jarada lililochapwa na mtambo uitwao Original Heidelberg wenye umri wa zaidi ya miaka 100 wakati alipotembelea Ofisi za Mpiga Chapa.WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa,  akipata maelezo kuhusu mtambo unaochapa majarada ya Serikali kutoka kwa Kaimu Mpiga Mkuu Chapa wa Serikali, John Kaswalala (kushoto), wakati alipotembelea Ofisi hizo. Kulia ni mwendeshaji wa mtambo huo, Dismas Shayo.


MAJALIWA (kulia),  akikagua moja ya karatasi zenye nembo na maadishi yalisioonekana kwa macho ya kawaida  kwenye  Kitengo cha Digitali wakati  alipotembelea ofisi hizo. Katikati ni Kaimu Mpiga Chapa Mkuu wa Serikali, John Kaswalala na kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Digitali, Ali Machupa. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments