Breaking News

ASILIMIA 85 YA WANAWAKE MKOANI MARA WANAJIFUNGUA KATIKA VITUO VYA AFYA * MGANGA MKUU ASEMA BADO KUNA UHABA MKUBWA WA MADAKTARI.WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Mhe.Ummy Mwalimu, asisitiza jambo alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma na miundombinu katika Hospitali ya Mkoa wa Mara jana Novemba 30, 20o18.

Na WAMJW - MARA.

ASILIMIA 85 ya Wanawake Mkoani Mara, wanajifungua kwenye vituo vya Afya, hali iliyosaidia kupunguza idadi kubwa ya  vifo vya mama na mtoto wakati wa kujifungua.

Hayo yalisemwajana Novemba 30, 2018 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu,  wakati alipotembelea Hospitali ya Mkoa wa Mara kukagua hali ya utoaji huduma.

WAZIRI Ummy, akiwa kwenye ziara ya kukagua hospitali hiyo.

"Mko asilimia 85, kitaifa tupo asilimia 51, kwahiyo niwapongeze kwa hilo, lengo letu ilikuwa ifikapo 2020 tunataka angalau asilimia 80 ya wanawake wajawazito wajifungulie kwenye vituo vya afya," alisema Waziri Ummy.

Pia, Waziri Ummy aliitaka mikoa mingine nchini kuiga jitihada zinazofanywa na mkoa wa Mara za kupunguza vifo vya mama na mtoto kwa kuhakikisha wanawake wajawazito wanajifungulia katika vituo vya kutolea huduma za afya.

WAZIRI Ummy, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi wengine wakati wa ziara hiyo hospitalini hapo.

"Sitaielewa mikoa mingine kwa kushindwa kuhamasisha na kuweka Mazingira mazuri kwa wanawake kwenda kujifungulia katika vituo vya kutoa huduma za afya," alisema Ummy.

Hata hivyo, Waziri Ummy Mwalimu, alimwagiza Mganga Mkuu wa Mkoa wa Mara, Dk. Francis Mwanisi,   kuhamasisha jamii hususan wanawake katika maeneo mbali mbali kuhudhuria kliniki angalau mara 4 katika kipindi cha ujauzito.

UMMY, akihoji juu ya gharama za huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali ya Mkoa wa Mara.

"Wanawake ambao wanahudhuria kliniki angalau mara 4 ni asilimia 45, hivyo hamjafanya vizuri  kwasababu kitaifa ni asilimia 51, mjenge tabia ya kuwahamasisha wanawake kuhudhuria kliniki angalau mara 4, kama watoa huduma za afya wanavyotushauri," alisema.

Aidha, Waziri Ummy, alimtaka Dk. Mwanisi, kuhakikisha ifikapo Desemba 30, mwaka huu, angalau kaya zote mkoani Mara ziwe na vyoo bora, ikiwa ni pamoja na kutoa elimu na kuhamasisha wananchi juu ya umuhimu wa matumizi ya vyoo bora kiafya na kiuchumi kwa mwanadamu.

WATUMISHI wa Kada mbali mbali za Afya wakimsikiliza Ummy (hayupo pichani) wakati wa ziara hiyo.

"Kaya zilizo na vyoo bora kwa Mara naona ni asilimia 40, kwahiyo tunahitaji kuongeza elimu na kutoa mwamko kwa jamii kuhusu kujenga vyoo bora na kuvitumia" alisema 
Ummy.

Mbali na hayo, Waziri Ummy alisema kuwa serikali inaendelea kuboresha huduma za afya mkoani humo kupitia kuboresha vituo vya afya 14, na kujenga hospitali 3 za wilaya ambazo ni Lorya, Musoma DC na Bunda, jambo ambalo litalopunguza mzigo kwa Hospitali ya Mkoa ili iweze kujikita katika kutoa huduma za rufaa.

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Ummy Mwalimu akisikiliza maoni ya wagonjwa.


Sambamba na hilo Waziri Ummy alisema, kuwa serikali itaendelea  kuboresha huduma bora kwa wananchi kwa  kupeleka jumla ya watumishi 25 katika Hospitali ya Mkoa wa Mara, huku akiwahasa viongozi mkoani hapo kujenga mazingira mazuri yakuwavutia watumishi ili wafanye kazi kwa bidii na kubaki katika vituo vyao vya kazi.

Kwa upande wake Mganga Mfawidhi wa Hospitali ya Mkoa wa Mara Dk. Hosea Bisanda, alisema kuwa hospitali hiyo iliweza kupunguza vifo vya akina mama vitokanavyo na uzazi kutoka vifo 23 mwaka 2015, vifo 14 mwaka 2016, vifo 10 mwaka 2017, na vifo 6 hadi kufikia Oktoba mwaka huu.

 WAZIRI Ummy ,  akitoa maoni juu ya namba za mawasiliano zilizopo kwenye ubao mdogo wa matangazo katika Hospitali Rufaa ya Mkoa wa Mara, alipofanya ziara ya kukagua ubora wa huduma.

Dk. Bisanda, alisema kuwa licha ya serikali kuwaletea watumishi 25,  hospitali hiyo inatakiwa kuwa na watumishi 684, lakini na kwamba waliopo sasa ni 305, hivyo bado kuna upungufu wa watumishi 379 sawa na asilimia 55.

Alisema, hospitali hiyo ina uhaba wa watumishi hasa madaktari bingwa, madaktari wasaidizi, wauguzi, wateknolojia, maabara pamoja na wateknolojia madawa.

No comments