Breaking News

BALOZI SEIF AIOMBA TUME YA NGUVU ZA ATOMIKI TANZANIA {TAEC} KUANDAA MAFUNZO KWA WAJUMBE WA BARAZA LA WAWAKILISHI WANAOWAKILISHA WANANCHI KATIKA MAJIMBO YAO.BALOZI Seif, (kushoto), akizungumza na Busagala


Na Mwandishi Wetu, Zanzibar

WATANZANIA lazima waendelee kubaki salama na afya chini ya matumizi sahihi ya mionzi inayotokana na Teknolijia ya Nyuklia Duniani ambapo kwa hapa nchini,  yanaratibiwa na Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC}.

Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania, Profesa Lazaro Busagala, alisema hayo leo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar  Balozi, Seif Ali Iddi Vuga Mjini Zanzibar alipofika kujitambulisha rasmi baada ya kuteuliwa kuiongoza Taasisi hiyo ya Teknolojia.

Profesa Busagala alisema, Tume hiyo iliyoanzishwa kwa sheria ya Bunge Nambari 7 ya Mwaka 2003 kulingana na kifungu nambari 6{1} cha sheria ya Atomiki imepewa jukumu la kudhibiti matumizi salama ya mionzi, kuhamasisha na kupanua matumizi salama ya Teknolojia ya Nyuklia pamoja na kutoa ushauri na taarifa tofauti za Kisayansi na Teknolojia ya Nyuklia.

Alisema, udhibiti huo una lengo la kulinda umma, wafanyakazi pamoja na mazingira dhidi ya madhara ya mionzi,  jukumu linalowapa mamlaka ya kufanya ukaguzi wa vituo vitoavyo huduma ya mionzi nchini ili kujiridhisha na hali ya usalama.

Profesa Busagala,  alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba zipo Hospitali 72 Nchini Tanzania zilizofungiwa kutoa huduma za mionzi baada ya kubainika matatizo yanayosababisha kuathiri kwa wagonjwa wasiopungua Laki 262,000 kwa mwaka.

Alisfafanua kuwa, ugonjwa wa Saratani unaoibuka kutokana na sababu mbali mbali zikiwemo zile za mionzi umeongezeka kwa asilimia 30  hadi 40 katika kipindi cha miaka mitatu iliyopita hali inayowafanya Wataalamu wa Tume hiyo kuwa makini katika utekelezaji wa majukumu yao katika kusimamia udhitibi mzuri wa matumizi ya mionzi.

Profesa Busagala,  alisema matumizi ya Teknolojia ya Mionzi Nchini,  hivi sasa tayari yameibua vianzio zaidi ya 700 vinavyotokana na huduma za hospitali, viwanda pamoja na vifaa ya utengenezaji wa bara bara.

Akizungumzia masuala ya ufundi wa vifaa vinavyotokana na mionzi, Busagala alisema tume ina maabala maalumu inayofanya kazi ya kuratibu, kutoa huduma ya kudhibiti ubora wa vifaa vya nyuklia pamoja na mafunzo ya ufundi.

Alisema wakati Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar tayari imesharidhia kuipatia Tume hiyo eneo la ujenzi wa maabara kwa upande wa Zanzibar ili iendelee kutekeleza majukumu yake ya ufanisi mzuri zaidi lengo la maabara hizo ni kuimarisha  uwezo wa Taifa katika ufundi wa vifaa vya nyuklia.

Kwa mujibu wa Busagala, baadhi ya huduma zinazotolewa na maabara kufuatia maombi ya wadau mbali mbali ni pamoja na matengenezo ya mashine za hospitali za X – Ray, vifaa vya kisayansi vinavyotumika katika utafiti, Viwanda na Hospitali.

Kuhusu mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya kilimo kwa matumizi bora ya mionzi, Busagala alisema lipo ongezeko kubwa la uzalishaji katika kilimo cha Mpunga, Migomba, Mahindi na Shairi hatua iliyowapa matumaini makubwa wakulima hasa upande wa Zanzibar.

Profesa Busagala alisema mafanikio hayo yalikwenda sambamba na udhibiti wa maradhi mbali mbali kwenye mimea na matunda yaliyokuwa yakisababishwa na wadudu Mbuno ambapo Zanzbar ilifanikiwa kupiga vita maradhi hayo mnamo Mwaka 1998 baada ya upandishaji mbegu za kuzuia ongezeko la wadudu hao chini ya utaalamu wa Shirika la Nguvu za Atomiki Duniani {IAEA}.

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliueleza Ujumbe wa Viongozi wa Tume hiyo ya Nguvu za Atomiki Tanzania kwamba jamii bado ina uelewa mdogo juu ya tafrisi sahihi ya masuala ya nguvu za Atomiki.

Balozi Seif alisema watu wengi wana ufahamu wa Atomiki na masuala yanayotokana na nguvu za Kijeshi wanazofikiria zinaweza kuleta athari ya maangamizi wakati wowote iwapo wasimamizi wake watatumia visivyo stahiki.

Alisema ipo haja ya wataalamu wa tume hiyo kuendelea kutoa taaluma kwa jamii ili iondoe shaka sambamba na kujilinda na masuala ya mionzi katika misingi halali inayokubalika kitaaluma.

Akielezea furaha yake kutokana na uelewa na majukumu ya tume hiyo, Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar aliuomba uongozi wa juu wa Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania {TAEC} kuandaa mafunzo kwa Wajumbe wa Baraza la Wawakilishi wanaowakilisha Wananchi katika majimbo yao ili kwa hatua za awali Taaluma ya Teknolojia ya Nuklia isambae kwa jamii nzima.

BALOZI Seif (kulia), akimkaribisha Busagala

Tume ya Nguvu za Atomiki Tanzania yenye Makao Makuu yake mjini Arusha iliyoanzishwa kwa sheria ya bunge namba 7 ya mwaka 2003, awali ilikuwa ikijuilikana kama Tume ya Taifa ya Mionzi iliyoanzishwa kwa sheria ya bunge namba 5 ya mwaka 1983.

No comments