Breaking News

DK. KALEMANI AAGIZA MJI WA KATORO UWAKE UMEME NDANI YA SIKU SABA

WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, akizungumza na wananchi katika Kijiji cha Mapinduzi, Kata ya  Buseresere, wilayani Chato, mkoani Geita, mara baada ya kufika kijijini hapo kukagua mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu.


Na Teresia Mhagama, Geita

WAZIRI Nishati, Dk. Medard Kalemani, amemuagiaza Meneja wa TANESCO mkoani Geita, Eng. Joachimu Ruweta,  kuhakikisha mitaa yote katika  Mji mdogo wa Katoro wilayani Geita inawaka umeme ndani ya siku saba.

Agizo hilo alilitoa jana Novemba 24,2018 baada ya kukagua ujenzi wa miundombinu ya umeme katika mji huo na kukuta kuna nguzo zilizosimikwa kwa muda mrefu bila wananchi kuunganishiwa umeme.

Pia, aliagiza kuwa wananchi hao waunganishiwe umeme kwa bei ya sh.i 27, 000 tu na siyo gharama za TANESCO zinazoanzia sh.177,000.

Katika hatua nyingine, Waziri Kalemani, alimtaka meneja huyo kuongeza nguvu kazi ya vibarua ili kazi ifanyike kwa wakati uliopangwa.

Waziri Kalemani, licha ya kuagiza wananchi hao wafungiwe umeme ndani ya siku saba kuanzia sasa, pia aliaahidi kurudi wilayani humo baada ya siku hizo ili kujiridhisha kama agizo lake limefanyiwa kazi.

Alisema, akibaini kuwa agizo lake halikufanyiwa kazi ndani ya muda huo, atahakikisha anachukua hatua kali za kinidham.

WAZIRI Kalemani akifafanua jambo.

Wakati huo huo, Waziri Kalemani,  akiwa katika Kata ya Buseresere wilayani Chato,  alikataa kuzindua mradi wa umeme katika Kijiji cha Mapinduzi, baada ya kubaini kulikuwa na  wananchi saba tu katika Kijiji hicho ndio waliounganishiwa umeme huku kukiwa na nguzo za umeme zilizosimikwa  kwa muda mrefu bila kuwa na nyaya.

Hivyo,  baada ya kukagua miundombinu ya umeme katika kijiji hicho, alimuagiza Meneja wa TANESCO wilaya ya Chato, Eng. Nyaonge Nyabinyiri, kuhakikisha kuwa wananchi wengi katika  kijiji hicho pamoja na cha Ibondo wanaunganishwa na umeme ifikapo Disemba 5, mwaka huu.

Aidha,  aliwaagiza watendaji wa TANESCO kufungua dawati la kuhudumia wateja katikati  ya Mji Mdogo wa Katoro na Kata ya Buseresere ili kuwapunguzia adha wananchi ya kufuata huduma mjini Geita au Chato.

Kwa upande wao  mameneja hao, walimuahidi Waziri Kalemani  kuwa watatekeleza maagizo hayo ndani ya muda.

No comments