Breaking News

DK. MPOKI ULISUBISYA AKEMEA TABIA YA ABIRIA NA MADEREVA 'KUCHIMBA DAWA' MAENEO YASIYO SALAMA.


 DK. ULISUBISYA akizungumza katika mkutano huo jana Jijini Dodoma.


Na WAJMW-Dodoma

MADEREVA wa mabasi yaendayo mikoani na abiria wametakiwa kuacha tabia ya kujisaidia ‘kuchimba dawa’ katika maeneo yasiyo rasmi ili kutunza na kuepuka uharibifu wa mazingira unaoweza kujitokeza ikiwa ni pamoja kusababisha magonjwa ya milipuko.

Kauli hiyo ilitolewa jana na Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Mpoki Ulisubisya, wakati akifungua mkutano unaojumuisha maofisa afya kutoka mikoa na halmashauri mbalimbali nchini, pamoja na wadau wa mazingira, katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma.

KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dk. Mpoki Ulisubisya, akikagua maonesho ya vyoo baada ya kufungua kikao cha maofisa afya wa mikoa, halmashauri pamoja na wadau wa mazingira jana Jijini Dodoma katika ukumbi wa Jakaya Kikwete.(Picha zote na Ofisi ya Wizara ya Afya).

Dk. Ulisubisya, alikemea tabia hiyo hatarishi kwa ustawi wa mazingira huku akiwataka maofisa afya na wadau wa mazingira nchini, kusimamia afua zilizowekwa zinaendelea kutekelezwa ili kulinda mazingira ambayo yanatuzunguka.

“Kuna watu wengine niliwahi kuwaona kwenye mabasi wakitupa taka hovyo na mabasi mengine yanasimama porini ili abiria wajisaidie, hii tabia siyo nzuri na inatakiwa ikemewe kwa nguvu zote, Dk. Subi na wenzake wanakuja na mpango mkakati  wa kuondoa kabisa dhana ya watu kusimama kujisaidia porini, sisi tunatakiwa kuwa msitari wa mbele kupiga marufuku mabasi  kusafiri bila kuchafua mazingira,”alisema.


BAADHI ya washiriki wafuatilia kwa makini mkutano huo.

Dk. Ulisubisya alisema, ni aibu kubwa kwa taifa kuona watu hawafuati kanuni za usafi huku akiwataka maofisa hao kuhakikisha wanafanya kazi ipasavyo ili kuondoa kero hiyo na kwamba watakaobainika kuchafua mazingira wachukuliwe hatua za kinidhamu na kisheria.

 KATIBU Mkuu Wizara ya Afya Dk. Mpoki Ulisubisya   akiwa katika picha ya pamoja na washiriki wa mkutano huo Jijini Dodoma.Aidha, alisema jamii inatakiwa kuzingatia matumizi ya vyoo bora na kunawa mikono mara baada ya kujisaidia ili kuepuka magonjwa ya milipuko yanayoweza kusababishwa na tabia ya uchafu ikiwa ni pamoja na kuacha tabia ya kujisaidia hovyo porini ili kaulimbiu ya “Nyumba ni Choo” iweze kutekelezwa ipasavyo kwa kujenga vyoo vya kisasa katika maeneo mbalimbali ili huduma ipatikane mahala pote.


Kwa upande wake Mkurugenzi wa Kinga kutoka Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Dk. Leonard Subi, alisema takwimu zinaonyesha kaya zilizokua na vyoo bora mwaka 2012 zilikua asilimia 19.5 lakini hivi sasa nchi nzima kaya zenye vyoo bora ni asilimia 51.4.

Kwa mujibu wa Dk. Subi, kutokana na takwimu hizo, inaonyesha kuna mafanikio katika uhamasishaji kwa jamii kutumia vyoo bora na kuacha kutumia vyoo ambavyo havina viwango na salama kwa matumizi na badala yake serikali inaendelea kutoa elimu na kusisitiza jamii kutumia vyoo bora ili kuepuka magonjwa yanayoweza kuzuilika ikiwemo kipindupindu, magonjwa ya tumbo na kuhara.


Pamoja na hayo, maofisa afya wametakiwa kuongeza nguvu katika kutoa elimu kwa umma, kuhamasisha usafi wa mazingira na kufukia maeneo ya mazalia ya vimelea vya ugonjwa wa Malaria ili kutokomeza ugonjwa huo ambao umekua hatari kwa jamii hasa kwa wanawake wajawazito na watoto. 

                     

Mkutano huo unaojumuisha maofisa afya nchi nzima, una lengo la kutoa elimu na kubadilishana uzoefu wa kufanya kazi huku kukiwa na msisitizo mkubwa wa utunzaji mazingira na kuzingatia kanuni bora za afya, usafi wa mazingira pamona na usafi na afya ya binadamu.

No comments