Breaking News

DKT KALEMANI ARIDHISHWA NA UZALISHAJI WA NYAYA ZA UMEME KATIKA KIWANDA CHA EVERNa Mwandishi Wetu.
WAZIRI wa Nishati, Dkt Medard Kalemani ameeleza kuridhishwa kwake na uzalishaji wa nyaya za umeme unaofanyika katika kiwanda cha Everwell Cable & Engineering kilichopo mkoani Pwani ambacho kina uwezo wa kuzalisha nyaya za urefu wa kilometa 24,000 kwa mwaka.


Hayo ameyaeleza akiwa katika ziara ya kikazi mkoani Pwani na Dar es Salaam ambapo alikagua uzalishaji wa nyaya katika kiwanda hicho pamoja ujenzi wa vituo vya kupoza umeme vya Dege na Kurasini.

“ Kwa sasa kuna viwanda vitano vinavyozalisha nyaya za kutosha na za ukubwa mbalimbali hivyo bado nasisitiza agizo la Serikali la kutonunua nje ya nchi vifaa vya umeme vinavyopatikana hapa nchini,” alisema Dkt Kalemani.

Aidha, Dkt Kalemani amesema kuwa, Serikali haitawavumilia wakandarasi au wataalam wanaochelewesha utekelezaji wa miradi ya umeme kwa kisingizio cha kutokuwa na vifaa wakati vinapatikana kwa wingi na gharama nafuu ukilinganisha na vifaa kutoka nje ya nchi.

Akiwa katika kituo cha kupoza umeme cha Dege wilayani Kigamboni, alieleza kuridhishwa na hatua za ujenzi zilizofikiwa hadi sasa lakini alitoa agizo kwa watendaji wa Shirika la Umeme Tanzania (TANESCO) kuhakikisha kuwa ujenzi wa kituo hicho unakamilika ifikapo Februari mwaka 2019 badala ya Oktoba, mwakani.


Alisema kuwa kituo hicho kitafungwa mashine zenye uwezo wa megawati 200 lakini itaanza kufungwa mashine moja yenye uwezo wa megawati 50 itakayohudumia eneo la Kigamboni ambalo mahitaji yake ya umeme ni chini ya megawati 25.


No comments