Breaking News

MBUNGE MATTEMBE AWAPA NENO WAZAZI.Na mwandishi wetu, Singida.
WAZAZI wametakiwa kuacha kuitumia vibaya dhana ya elimu bure iliyoasisiwa na Rais Dk John Magufuli na badala yake washiriki katika kusaidia kuwezesha wanafunzi kusoma kwenye mazingira tulivu jukumu ambalo halipaswi kuachwa kwa serikali pekee. 

Wito huo umetolewa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, wakati akizungumza kwenye mahafali ya Kidato cha Nne katika Sekondari ya Mughunga mkoani hapa, ambapo amesema bado wazazi wana jukumu la kuendelea kuwahudumia watoto wao kwa kuwanunulia sare za shule pamoja na kufuatilia maendeleo yao darasani.


Amesema kuna baadhi ya wazazi wamekuwa wakitumia vibaya dhana ya elimu bure kwa kuacha hata kuwajibika katika kununua sare za wanafunzi, wakisubiri serikali kufanya kila kitu jambo ambalo ni kinyume kabisa na malengo yaliyokusudiwa.

Alisema Watanzania wamepata bahati kwa kuwa na Dk. Magufuli, ambaye ni kiongozi mwenye mapenzi mema na nchi na amepanga kuhakikisha wanafunzi wanasoma kwenye mazingira tulivu bila usumbufu na ndio sababu amefuta karo na michango mengine kuanzia shule ya msingi hadi kidato cha nne hivyo, ni jukumu la wazazi kuwa karibu na wanafunzi.


"Kwanza tunapaswa kumshukuru Rais Magufuli na serikali yake kwa kufuta michango yote shuleni kuanzia elimu ya msingi hadi kidato cha nne, lakini kuna baadhi ya wazazi wanatumia dhana ya elimu bure vibaya. 

“Wazazi ni lazima tushiriki katika kufuatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni na kuchangia kuwanunua sare nzuri na michango mingine midogo midogo ambayo inatugusa moja kwa moja. 

"Naomba sana tusiiangushe wala tusiibebeshe serikali mzigo wa kufuatilia maendeleo ya watoto wetu shuleni, naomba kwenye mambo mengine tushiriki hata kwa kuchangia nguvu na mawazo tu," alisema Mattembe.

Katika mahafali hayo, Mattembe alikabidhi vyeti kwa wahitimu, ambapo alitumia muda huo kuwaasa wanafunzi kusoma kwa bidii ili kuhakikisha wanatimiza malengo na kujiepusha na tamaa ili wasiingie kwenye mitego ya wanaume mafataki.

"Wadogo zangu hapa ni mwanzo tu wa safari ya kutafuta elimu na maisha bora, mnatakiwa kufunga mkanda kwelikweli ili mfike chuo kikuu na serikali inawategemea kuja kushika nafasi mbalimbali za uongozi hivyo, msikubali kurubuniwa na wanaume ama kujiingiza kwenye vishawishi bali mjitunze ili mfikie malengo," alisema.

Akiwa, shuleni hapo Mattembe alikabidhi zawadi mbalimbali ikiwemo vifaa vya michezo kwa timu za wanawake na wanaume ikiwa ni kuendeleza jitihada zake za kuinua michezo mashuleni, ambapo tayari amezipatia shule mbalimbali mkoani Singida vifaa vya michezo kwa ajili ya timu za shule.

Kabla ya mahafali hayo, Mattembe ametembelea Zahanati ya Mughunga kwa ajili ya kukagua ujenzi wa jengo jipya la zahanati, kuangalia utoaji huduma kwa wananchi hasa wajawazito ambapo, baadaye alipata nafasi ya kuzungumza na wagonjwa na watumishi wa zahanati hiyo.


No comments