Breaking News

UONGOZI WA CHUO CHA KIMATAIFA CHA SAYANSI NA BIASHARA CHA NCHINI OMAN KUJENGA CHUO KINGINE KIPYA CHA KIMATAIFA VISIWANI ZANZIBAR.


 
Dk. Muneer Moh’d Al – Naamany akifafanua zaidi malengo ya chuo chake mbele ya  Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga Mjini Zanzibar.

Na Mwandishi Malumu, Zanzibar

UONGOZI wa Chuo cha Kimataifa cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman, unakusudia kuanzisha chuo kingine kipya cha Kimataifa Visiwani Zanzibar, kitachopewa jina la American and Europe of  East Africa kwa lengo la kupanua Sekta ya Elimu ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki.

Mkuu wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini humo Dk. Muneer  Moh’d Al – Naamany, alitoa kauli hiyo wakati ujumbe aliouongoza wa chuo hicho ulipofanya mazungumzo na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga, Mjini Zanzibar jana.

Dk. Muneer Moh’d Al – Mastar,  alisema Zanzibar lazima iwe kituo cha Elimu katika Ukanda wa Mashariki na Kusini mwa Bara la Afrika kitakachomjengea  mwanafunzi uwezo wa ajira ya kuaminika  mahali popote Duniani baada ya kumaliza masomo katika chuo hicho.

 MKUU wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini humo DK. Muneer Moh’d Al – Naamany wa pili (kulia), akielezea msimamo wa uongozi wa chuo chake kutaka kuanzisha kunzishwa Zanzibar.

Alisema mazingira ya kumfundisha mwanafunzi katika muelekeo wa chuo hicho kinachokusudiwa kuanzishwa Zanzibar,  unatokana na uzoefu wa miaka 20 tokea kuanzishwa kwake . Chuo hicho kina  Wahadhiri kutoka pembe zote za Dunia wanaofundisha kwenye taasisi yao.

Mkuu huyo wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Oman mwenye asili ya Zanzibar, alimueleza Balozi Seif , kwamba uongozi wa chuo chake ulifikiria mpango huo kwa nia ya kuirejeshea hadhi yake Zanzibar kuwa kituo cha masuala mengi katika enzi zilizopita hasa harakati za biashara na usafiri uliokuwa ukiunganisha Dunia.

 Dk. Muneer Moh’d Al – Naamany, akisisitiza jambo wakati akizungumza na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Id
di Vuga Mjini Zanzibar.

Kwa upande wake Naibu Mkuu wa Chuo hicho Dk. Ahmed Al – Naamany, alisema mfumo wa ufundishaji utakaotumika utampa mwanafunzi uwezo wa kuendelea na masomo yake hata akiwa nje ya Zanzibar.

Dk. Ahmed alisema, mwanafunzi hata akiwa Dar Es Salaam, Nairobi au sehemu yoyote ya Afrika ya Mashariki ataweza kuunganishwa katika mfumo wa mafunzo ya mtandao wa teknolojia ya kisasa akienda sambamba na wanafunzi wenzake watakaokuwa chuoni.

NAIBU Mkuu wa chuo hicho, Dk. Ahmed Al – Naamany, akimueleza Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, aliyeshiriki mazungumzo hayo fursa zitakazopatikana katika mafunzo yatakayotolewa na chuo chake.

Naibu Mkuu huyo wa Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman,  alimuhakikishia Makamu wa Pili wa Rais, kwamba mwanafunzi atakayemaliza mafunzo yake ‘atauzika’  katika taasisi zozote zile iwe za Kitaifa au Kimataifa bila wasi wasi wowote.

Akitoa ufafanuzi kwa ujumbe huo wa Oman, Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, alisema wazo la uongozi wa chuo hicho kwakuwa limelenga kuimarisha Sekta ya Elimu.

Waziri Riziki alisema,  katika kuunga mkono mawazo hayo, vipo vyuo vilivyo chini ya Chuo Kikuu cha Taifa cha Zanzibar (SUZA) ambavyo uongozi huo unaweza kuangalia mazingira yake iwapo utapatikana uwezekano wa kuunganishwa katika muelekeo walioukusudia.

Hata hivyo, waziri huyo alieleza kwamba wizara yake inayachukuwa mawazo hayo kwa kuyafanyia kazi mara moja ili baadaye kuyawasilisha serikalini kwa hatua sambamba na maamuzi muwafaka.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar, Balozi Seif Ali Iddi (kulia), akizungumza na Uongozi wa Chuo cha Kimataifa cha Sayansi na Biashara  cha Nchini Oman uliofika Ofisini kwake Vuga kwa lengo lakutaka kutaka kuanzisha Chuo Kikuu Visiwani Zanziba

Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais, Balozi Seif aliuhakikishia  uongozi wa chuo hicho kwamba Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuupa fursa uongozi huo kuanzisha chuo chake visiwani humo.

Balozi Seif alisema,  kinachohitajika hivi sasa kwa uongozi huo ni kuandika maombi rasmi na kuyafikisha serikalini kwa hatua itakayostahiki ili ile azma yao ya kupanua Sekta ya Elimu ndani ya Ukanda wa Afrika Mashariki iweze kufanikiwa vyema.

MAKAMU wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, akiangalia baadhi ya vitabu vynye mfumo wa Mitaala ya Chuo cha Sayansi na Biashara cha Nchini Oman. (Picha zote na Ofisi ya OMPR-ZNZ).                            


Uongozi wa chuo hicho endapo utapata fursa hiyo umelenga kuanza mradi wao wa chuo mapema Septemba mwakani kwa kuanzia na majengo muhimu machache.

No comments