Breaking News

BALOZI IDDI AZINDUA MELI MPYA YA KISASA YA SEA STAR.


 
 MELI Mpya ya Kampuni ya Sea Star ikiwa imetia Nanga baada ya kuwasili katika Bandari ya Malindi,  Zanzibar. (Picha zote na OMPR – ZNZ).

Na Othman Khamis Ame, OMPR – ZNZ.


KAMPUNI ya Usafirisaji  wa Baharini Sea Star imeleta meli mpya   yenye uwezo wa kubeba Mizigo Tani 1,400 na Abiria 1,500 ili  kuongeza huduma za usafiri wa baharini katika Mwambao wa Bahari ya Afrika Mashariki.
Meli hiyo iliyopewa jina la Sea Star  itafuatiwa na boti nyingine Mbili za mwendo wa kasi zinazotarajiwa kuingia Visiwani Zanzibar  Juni mwakani.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi leo  akiwa na baadhi ya Viongozi na watendaji wa mamlaka zinazosimmamia usafiri wa baharini alipata nafasi ya kukagua sehemu mbali mbali za Meli hiyo iliyopo bandarini Malindi ambapo aliliridhika na  ubora wake.
SEHEMU kubwa ya kuwekea mizigo mbali mbali ndani ya meli mpya ya Sea Star yenye uwezo wa kubeba mizigo tani 1,400 na abiria 1,500 ikiwepo Bandarini Malindi.
Meli hiyo yenye sehemu kubwa ya kubebea mizigo, vyumba vya watu mashuhuri (VIP)  pamoja na abiria wa kawaida itaanza na safari za Zanzibar-Pemba – Tanga, Zanzibar – Dar es salaa, Zanzibar – Mtwara na baadae kuendelea na safari za mbali kwa kuanzia Visiwa vya Comoro.Safari ya Zanzibar - Dar es salaam huchukuwa muda unaokadiriwa wastan wa saa tatu wakati safari ya Zanzibar – Pemba itachukuwa wastani wa saa nne na nusu.
Akitoa maelezo ya uwepo wa meli hiyo nchini mwakilishi wa Kampuni ya Sea Star Salum Turky alisema uongozi wa kampuni hiyo umejidhatiti kutoa huduma bora za usafiri wa baharini kwa wananchi wote.
Turky alisema miongoni mwa mambo yatakayozingatiwa na uongozi huo katika uendeshaji wa biashara hiyo ni kuhusika katika  kufuata taratibu zote zilizoainishwa na Mamlaka ya Usafiri wa Baharini.
EHEMU za kukaa watu mashuhuri (VIP) zilizomo ndani ya Meli ya Sea Star.
Alisema Abiria wa kawaida atawajibika kulipia nauli shilingi 25,000/, mtoto wa kawaida atalipiwa nusu nauli na yule aliye na umri kati ya siku moja hadi miaka sita atachukuliwa bila ya malipo.
Salum Turky alimueleza Balozi Iddi  kwamba uongozi huo umeahidi kuunganisha safari za Visiwa vya Comoro kufuatia ahadi aliyoitoa  Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,  katika kuimarisha uhusiano kati ya Zanzibar na Viosiwa hivyo.
Katika kuimarisha huduma hizo za usafiri wa baharini mwakilishi huyo wa Sea Star aliiomba Serikali kuwapatia sehemu maalum na ya uhakika kwa ajili ya kuuzia tiketi ili kuwaondoshea usumbufu wananchi wanaohitaji huduma hizo.
 MUONEKANO wa sehemu za nje za abiri wa kawaida zilizopo juu kabisa ya meli mpya ya abiria na mizigo ya Kampuni ya Sea Star One.
Kwa upande wake Naibu Waziri wa Biashara na Viwanda Zanzibar, Hassan Khamis Hafidh aliushauri uongozi wa Sea Satar kwenda na  ushindani wa kibiashara huku pia wakizingatia huduma nafuu kwa wananchi.
Hassan alisema Serikali imeamua kuweka milango wazi ya uwekezaji nchini katika azma ya kuona maeneo yote ya huduma za umma yanawafikia vyema na kwa wakati Wananchi walio wengi hasa wale wenye kipato cha chini.
KAPTENI wa Meli Mpya ya Sea Star Nassor Abubakar, akimpatia maelezo Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, kwenye chumba cha mawasiliano alipofika kuikagua.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi aliipongeza kampuni hiyo ya kizalendo kwa uwamuzi wake wa kuongeza huduma za usafiri wa baharini nchini.
Balozi Seif  alisema uamuzi wa kampuni hiyo wa kuimarisha huduma za usafiri umekuja kwa wakati huku ukizingatia kwenda sambamba na mabadiliko ya maisha ya wananchi yanayowapa fursa ya kuingia katika mzunguuko wa kibiashara unaohitaji zaidi huduma za usafiri.
BALOZI Iddi (katikati) akibadilishana mawazo na Uongozi mzima wa Sea Star juu kabisa ya Meli ya Kampuni hiyo baada ya kumaliza ziara ya kuikagua sehemu mbali mbali.
Kampuni ya Sea Star iliwahi  kuwa na boti mbili ziendazo kwa kasi za Sea Star One na Sea Star Two zilizotoa huduma za usafiri wa baharini kati ya Bandari ya Zanzibar na ile ya Dar es salaam kwa zaidi ya miaka 13 iliyopita.

No comments