Breaking News

DK. SHEIN AVITAKA VYUO VIKUU ZANZIBAR KUZINGATIA MITAALA WANAYOFUNDISHIA VYUONI KAMA INAKIDHI MAHITAJI HALISI.


 
MAKAMU wa Pili wa Rais  wa  Zanzibar, Balozi  Seif  Ali Iddi, akifurahia zawadi maalumu aliyokabidhiwa na Kaimu Mwenyekiti wa Baraza la Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu (ZU) Profesa Saleh Idris Mohamed  baada ya kukamilika kwa Mahafali ya 16 ya wahitimu chuoni hapo leo Desemba 19, 2018.
  
Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
RAIS wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein, alisema uongozi wa Vyuo Vikuu vilivyopo Zanzibar, vinapaswa kuzingatia Mitaala wanayofundishia vyuoni iwapo  inakidhi mahitahi halisi ya fursa zinazoweza kuibua wataalamu wa kutosha wa kulisaidia Taifa na jamii katika fani tofauti.
Alisema, jamii hivi sasa inapita katika wakati wa mabadiliko ya Sayansi na Teknolojia Duniani ambayo kwa vyovyote vile italazimika kujikita katika elimu bora itayoweza kuwavusha salama katika mabadiliko hayo muhimu kwa maendeleo ya uchumi na Taifa.
Dk. Ali Mohamed Shein, alitoa kauli hiyo katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi. Seif Ali Iddi wakati wa mahafali ya 16 ya wahitimu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) kiliopo Tungu Mkoa wa Kusini Unguja.
Alisema vyuo hivyo ni vyema vikafanyakazi kwa karibu na Kamisheni ya Mipango Zanzibar inayosimamia mipango ya maendeleo ili iwe rahisi kuyapa kipaumbele maeneo yanayoweza kuwekewa umuhimu wa awali katika Mitaala ya kufundishia.
Hata hivyo, pamoja na mambo mengine Rais wa Zanzibar, alitolea mfano miradi mipya inayotarajiwa kuanzishwa visiwani Zanzibar ya mafuta na Gesi Asilia kufuatia Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar kutiliana saini mkataba  na Kampuni ya Rakgas ya Nchini Ras Al – Khaimah kuhusu mgawanyo wa rasilmali hiyo.
Dk. Shein, alisema vyuo hivyo kwa sasa vina fursa ya kuchangamkia miradi hiyo kwa kuanzisha mafunzo ya mafuta na Gesi Asilia katika nganzi ya Diploma na Stashahada ili wakati utakapowadiua wa kuanza kwa mradi huo Taifa lisijekuwa na upungufu wa wataalamu.
 BALOZI Iddi, akimpongeza Mhadhiri wa Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU)  Ali Ahmed Uki, aliyekuwa Daktari wa  Sheria baada ya kuhitimu masomo yake chuoni hapo huku akiendelea na kazi yake ya Uhadhiri.
Alifahamisha kwamba vyuo vikuu mahali popote pale Dunia ndivyo vyenye dhamana ya kutoa wataalamu na watafiti wa fani mbali mbali ambao ndio chimbuko la  kuimarika kwa uchumi unaopelekea kupunguza changamoto za ajira sambamba na kuongezeka kwa pato la Taifa.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi alivipongeza Vyuo Vikuu vya Zanzibar kwa mchango mkubwa inavyotoa katika kuwafinyanga Wanataaluma hasa vijana kupata msingi imara unaolijengea Taifa umadhubuti wa kuwa na wasomi wanaotegemewa.
Hata hivyo, Dk. Shein alielezea faraja na matumaini yake kutokana na jitihada kubwa zinazochukuliwa na baadhi ya wawazi nchini kuwaandaa vijana wao kuingia katika kundi la wanataaluma ambao mbali ya kuwajengea hatma yao na vizazi vyao, lakini pia Taifa hufaidika kutokana na elimu hiyo.
Alisema wazazi hao mbali ya kutekeleza wajibu wao katika misingi ya imani ya dini katika kuwawekeza watoto wao katika elimu lakini pia hawajatupa kwa kutumia fedha zao kwenye jambo hilo, Fedha ambazo walikuwa wanaweza kuzitumia kwa masuala mengine ya kimaisha.
Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Dk. Ali Mohamed Shein,  ameishukuru Bodi ya Wadhamini ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) chini ya Mkuu wake Profesa Sulaiman Bin Nasser Basahal kwa uamuzi wake wa kuwekeza Visiwani Zanzibar.
Dk. Shein alisema uamuzi huo umeonyesha jinsi gani uongozi wa Bodi hiyo ulivyojitolea kuunga mkono skta ya elimu Zanzibar inayoongeza wanataaluma Visiwani Zanzibar na Tanzania kwa ujumla.
Mapema Makamu Mkuu wa Chuo Kikuu cha Zanzibar Tanguu (ZU)  Profesa Mustafa Roshash alisema uongozi wa chuo hicho kilichoasisiwa mwaka 1998 umepata faraja kutokana na hamasa ya Jamii iliyojielekeza kupata taaluma ya elimu ya juu.
Profesa Mustafa Roshash alitoa wito kwa wanataaluma wanaopitia elimu ya vyuo Vikuu kuendelea na mafunzo yao katika ngazi ya juu zaidi kwa kujielekeza kwenye tafiti kwa kadri ya fani zao walizobobea.
 BAADHI ya wahitimu wa mahafali hayo ya 16 ya katika Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunguu wakiwa katika picha ya pamoja..
Alisema uongozi wa chuo hicho utaendelea kuimarisha mitaala yake hadi kuona kila mwanajamii anapata fursa ya kujiendeleza kwa kadri ya uwezo wake wa kitaaluma.
Aliipongeza Wizara hya Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar kwa kuendelea kukiunga mkono chuo hicho katika malengo yake ya kutoa elimuy hapa nchini na Ukanda wa Afrika Mahsriki kwa ujumla.
Akimkaribisha mgeni rasmi katika mahafali hayo ya 16 ya Chuo Kikuu cha Zanzibar (ZU) Waziri wa Elimu na Mafunzo ya Amali Zanzibar, Riziki Pembe Juma, aliuomba uongozi wa chuo hicho kufikiria kutumia lugha ya Taifa katika mahafali ya mwaka ujao.
Riziki alisema hatua hiyo muhimu itawapa fursa wanafunzi wa nje ya Zanzibar kuondoka na zawadi ya lugha hiyo iliyopata umaarufa na kukubalika katika maeneo mbali mbali Duniani.
Jumla ya wahitimu 1,076 wa fani mbali mbali wamepata vyeti, Diploma, Stashahadapamoja na Shahada.
Chuo Kikuu cha Zanzibar Tunbguu (ZU) kilichoasisiwa mnamo Mwaka 1998 na kuanza kutoa Vyeti, Diploma na Stashahada na Shahada tayari kimeshazalisha wahitimu  9, 344.

No comments