Breaking News

'IWE MVUA IWE JUA' UJENZI WA MIRADI YA UMEME VIJIJINI LAZIMA UENDELEE.-SUBIRA.


 NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu akikata utepe ikiwa ni ishara ya wananchi katika Kijiji cha Bulongwa wilayani Makete kuanza kupata huduma ya umeme jana. Kulia kwake ni  Mkuu wa Wilaya ya Makete, Veronica Kessy.

Na Teresia Mhagama, Njombe
NAIBU Waziri wa Nishati, Subira Mgalu amewataka wakandarasi wanaosambaza umeme  vijijini kutochelewesha utekelezaji wa miradi hiyo kwa kisingizo cha mabadiliko ya hali ya hewa kama vile uwepo wa mvua.
Aliyasema hayo jana Desemba 20, 2018, wilayani Makete mkoani Njombe, wakati akikagua kazi ya usambazaji umeme vijijini inayotekelezwa kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu (REA III), mzunguko wa kwanza.
“ Kabla ya Serikali kuwakabidhi kazi hii ya usambazaji umeme vijijini, mlishafanya upembuzi wa maeneo mnayoenda kufanyia kazi na mnayafahamu vizuri, hivyo basi, iwe jua au mvua, tunataka kuona kazi hii inaendelea kutekelezwa ili wananchi wengi wapate huduma ya umeme,” alisema Mgalu
Aliongeza kuwa, wakandarasi hao wanapaswa kuwa na mipango mbalimbali  ya utekelezaji wa kazi kulingana na hali ya hewa ya maeneo wanayofanyia kazi ili kuweza kusambaza umeme katika vijiji vyote walivyopangiwa na Serikali ifikapo Juni 2019.
Awali, Mkuu Wilaya ya Makete, Veronica Kessy, alimweleza Naibu Waziri kuwa, jumla ya vijiji 29 vimepangwa kuunganishiwa umeme kupitia mradi wa REA III mzunguko wa kwanza ambapo mkandarasi anaendelea na kazi ya usambazaji umeme vijijini, ingawa uongozi wa wilaya hiyo umekuwa na wasiwasi na kasi yake katika usambazaji umeme.
Kuhusu hali ya upatikanaji umeme, alisema kuwa wilaya  hiyo inapata umeme kutokea mkoani Mbeya lakini laini hiyo ni ndefu na inapelekea changamoto ya kukatika kwa umeme mara kwa mara, hivyo aliomba wilaya hiyo ipate laini nyingine ya umeme kutokea mkoani Njombe.
Kuhusu suala hilo, Naibu Waziri wa Nishati, Subira, alisema kuwa, Serikali ilishaona changamoto hiyo ya umeme wilayani Makete na kueleza kuwa wilaya hiyo ipo katika mpango wa kupelekewa umeme kupitia mradi wa Makambako- Songea ambao umekamilika.
Akiwa wilayani humo, NaibuWaziri aliwasha umeme katika Kijiji cha Bulongwa na kukagua miundombinu ya umeme katika Vijiji vya Usagatikwa na Usungilo ambapo alimsisittiza mkandarasi kuongeza kasi ya kusambaza umeme.
WANANCHI wa Kijiji cha Usungilo Wilayani Makete, wakimsikiliza NaibuWaziri wa Nishati, Subira Mgalu (katikati) wakati alipofika kijijini hapo kukagua kazi ya usambazaji umeme jana.
Wilaya ya Makete ina vijiji 96 ambapo vijiji 29 tayari vimeshasambaziwa umeme, vijiji 29 vinasambaziwa umeme kupitia REA III mzunguko wa kwanza ambapo vijiji 38 vilivyosalia vitasambaziwa umeme kupitia mradi wa usambazaji umeme vijijini wa Awamu ya Tatu unaotarajiwa kuanza Julai mwakani.

No comments