Breaking News

JUKWAA LA UWEKEZAJI WA BIASHARA DUNIANI KUFUNGUA KITUO CHA MAFUNZO ZANZIBAR.


                             
MAKAMU wa Pili wa Rais Zanzibar,  Balozi Seif  Ali Iddi (kulia), akimuonyesha na kumkabidhi kitabu cha masuala ya Uwekezaji Vitega Uchimi Zanzibar,  Mwenyekiti wa Jukwaa la Uwekezajiwa Biashara Duniani la Malaika (WBAF) Baybars Altuntas baada ya kumaliza mazungumzo yao jana Desemba 21, 2018. (Picha zote na – OMPR – ZNZ).
                                 Na Mwandishi Wetu, Zanzibar
UONGOZI wa Jukwaa la Uwekezaji wa Biashara Duniani lijulikanalo Malaika (WBAF) unakusudia kuanzisha kituo cha mafunzo Visiwani Zanzibar hapo mwakani kitakachosimamia uratibu wa kukusanya mawazo, fikra na utaalamu utaobuniwa na vijana katika muelekeo wa kuwajengea uwezo wa kujitegemea.
Mwenyekiti wa Taasisi hiyo yenye Makao Makuu yake Mjini Instanmbul, Nchini Uturuki, Baybars Altuntas, aliyeuongoza ujumbe wa taasisi hiyo, alieleza hayo jana Desemba 21, 2018 wakati wa mazungumzo yake na Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi, Vuga Mjini Zanzibar.
Altuntas alisema, Jukwaa la Uwekezaji Biashara Duniani la Malaika limeamua kuanzisha kituo hicho ili kwenda sambamba na malengo ya vijana katika dhana nzima za kujipatia ajira na kuondokana na mazingira hatarishi yanayowapelekea kujiingiza katika matendo ya hatari.
 BALOZI Iddi (katikati), akizungumza na Meneja wa Jukwaa la Uwekezajiwa Biashara Duniani la Malaika (WBAF) Tawi la Dar es salaam Tanzania DK. Sabetha . Mwambenja. Kushoto ni Altuntas.
Alisema Zanzibar imebarikiwa kuwa na fursa nyingi za Uwekezaji hasa katika Sekta ya Utalii ambazo kama zitatumiwa vyema zinaweza kuwaunganisha vijana katika ajira baada ya kupatiwa mafunzo sahihi na ya msingi ya ujasiri amali.
“Tumekuwa tukitoa mafunzo sambamba na mitaji na kuongeza fursa zaidi iwapo mjasiliamali ataongeza na kuonyesha juhudi za ubunifu,” alisema Altuntas.
Mwenyekiti huyo wa Jukwaa la Uwekezaji wa Biashara Duniani la Malaika alimueleza Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar kwamba WBAF imejitolea kutoa mafunzo na uwezeshaji kwa vijana waliojikubalisha kutumia ujuzi na maarifa yao katika Ubunifu.

BALOZI Iddi (kushoto),  akizungumza na Ujumbe wa viongozi wa Jukwaa la Uwekezajiwa Biashara Duniani la Malaika (WBAF)..
Akitoa ufafanuzi wa masuala ya Takwimu  Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango Zanzibar, Khamis Mussa, alisema kuanzishwa kwa kituo hicho, Zanzibar mbali ya kusaidia wahusika ambao ni vijana lakini pia kitaleta faraja kwa Serikali Kuu.
Khamis alisema Takwimu za Dunia ikiwemo pia Zanzibar zinaonyesha kuwa vijana wanaendelea kuwa kundi kubwa katika idadi ya watu Duniani kundi ambalo bado linakumbwa na ukosefu wa ajira.
Akitoa shukrani zake Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar Balozi Seif Ali Iddi alisema Serikali ya Mapinduzi ya Zanzibar iko tayari kuuunga mkono jitihada zinazochukuliwa na taasisi za kiraia katika kuona kundi la vijana linaimarika kiuchumi.
 BALOZI iddi (watatu kulia), akiwa katika picha ya pamoja na uongozi wa Jukwaa la Uwekezajiwa Biashara Duniani la Malaika (WBAF) ukiongozwa na Mwenyekiti wake Baybars Altuntas baada ya kumaliza mazungumzo yao.
Balozi Iddi, alisema zipo juhudi zilizoanza kuchukuliwa na Serikali katika kuwajengea mazingira mazuri vijana pamoja na wanawake katika masuala ya uwezeshaji kiuchumi.
Makamu wa Pili wa Rais wa Zanzibar, aliuomba uongozi wa Jukwaa la Uwekezaji wa Biashara Duniani la Malaika kupitia Tawi lake liliopo Dar es salaam, Tanzania kuendelea kutoa mafunzo zaidi kwa kundi hilo linaloonekana kuongezeka kila mwaka baada ya kumaliza masomo yao.

No comments