Breaking News

MAGUFULI AISHUKURU SERIKALI YA KOREA KUFADHILI UJENZI WA DARAJA JIPYA LA SELANDRER HADI COCO BEACH.


 

RAIS Dk. John Magufuli, akishirikiana na Balozi wa Jamhuri ya Korea nchini Cho Tae-ick, kufunua pazia kuashiria   kuwekwa kwa jiwe la msingi la mradi wa ujenzi wa Daraja jipya la Selander na Barabara unganishi ya km 6.23 toka Hospitali ya Aga Khan hadi ufukwe wa Coco Beach Jijini Dar es salaam leo Desemba 20, 2018. Wengine katika picha ni Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Mama Janeth Magufuli na viongozi wengine wanashuhudia. (Picha na Ikulu).


Na Thomas Mtinge

RAIS Dk.John Magufuli, ameishukuru Serikali ya Jamhuri ya Korea kwa kufadhili ujenzi wa daraja jipya la Selander linalounganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam kwa lengo la kupunguza msongamano wa magari katika barabara ya Ali Hassan Mwinyi.

Kufuatia ufadhili huo, Rais Magufuli, alimuomba Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea hapa nchini, Cho Tae-ick kufikisha ujumbe wake kwa Rais wa Jamhuri ya Korea, Moon Jae-in kuwa Tanzania itaendeleza na kukuza zaidi uhusiano na ushirikiano wake na nchi hiyo hususani wakati huu ambapo inaendelea kufanya mapinduzi makubwa ya kiuchumi.

“Jamhuri ya Korea ni marafiki wetu wa kweli, wametusaidia kujenga daraja la Kikwete katika mto Malagarasi na wametusaidia kujenga Hospitali ya Taaluma na Sayansi ya Tiba Mloganzila na miradi mingine, tunawashukuru sana, naomba na sisi Watanzania tubadilike, tuchape kazi, tuwe wazalendo, tuwahimize vijana wetu waje wafanye kazi kwenye mradi huu,” alisema Magufuli.

Dk. Magufuli, aliyasema hayo  leo Desemba 20, 2018 katika hafla ya kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa daraja hilo jipya la Selander linalounganisha eneo la Aga Khan na Coco Beach Jijini Dar es Salaam.

Daraja hilo lenye urefu wa meta 1,030 na upana  wa meta 20.5 litakuwa na njia 4 za magari na njia 2 za watembea kwa miguu, na litajengwa pamoja na barabara unganishi zenye jumla ya kilometa 5.2.

Rais Magufuli, aliitaka Wizara ya Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano kutafuta jina la daraja jipya la Selander huku yeye (Magufuli), akipendekeza lipewe jina la Tanzanite linaloakisi Utanzania.

Aidha, Rais alitoa wito kwa Watanzania wote kuchapa kazi kwa juhudi na maarifa huku wakitanguliza uzalendo, kudumisha amani na upendo na kutokukatishana tamaa ili Tanzania ifanikiwe kupiga hatua za kimaendeleo kama ilivyofanya Jamhuri ya Korea ambayo uchumi wake ulikuwa sawa na Tanzania miaka ya 60 wakati Tanzania ikipata uhuru.

Katika hatua nyinguine, Rais Magufuli, alimpongeza Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano Mhandisi Isack Kamwelwe, kwa juhudi zake za kusimamia ukusanyaji wa mapato ya Serikali.

Aliitaja baadhi ya jitihada hizo kuwa ni pamoja na ukusanyaji mapato kuwa ni kitendo cha  kuhakikisha mabasi yote 49,000 yaliyopo nchini yanaanza kutoa tiketi za kielekroniki, kuongeza tija katika ukusanyaji wa mapato ya usafirishaji kwa njia ya reli na kufuatilia meli moja kubwa iliyonunuliwa kwa ushirikiano wa Tanzania na China ili ianze kuja nchini na kuinufaisha Tanzania.

Kwa upande wake, Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (TANROADS), Mhandisi Patrick Mfugale, alisema ujenzi wa daraja hilo utakaochukua muda wa miezi 30 kuanzia  Julai 23, 2018 utagharimu sh. Bilioni 256 zilizotolewa kwa mkopo nafuu kutoka Jamhuri ya Korea kupitia Mfuko wa Ushirikiano wa Maendeleo ya Kiuchumi (EDCF) na Serikali ya Tanzania.

Kwa mujibu wa Mfugale, daraja hilo litadumu kwa muda wa miaka 100 na litajengwa bila kuathiri nyumba zilizopo kando ya barabara za Kenyatta na Toure ambazo miongoni mwake wanaishi Mabalozi.

Mapema akizungumza katika hafla hiyo, Balozi Mteule wa Jamhuri ya Korea Mhe. Cho Tae-ick aliishukuru Tanzania kwa uhusiano na ushirikiano mzuri uliopo kati yake na Jamhuri ya Korea ambapo katika kipindi cha miaka 26 ya uhusiano huo.

Alibainisha kuwa, Jamhuri ya Korea imetoa ufadhili wenye thamani ya zaidi ya sh.Trilioni 1 na hivyo kuifanya Tanzania kuwa nchi inayoongoza kwa ufadhili wa nchi hiyo Barani Afrika.

Nae mwakilishi wa EDCF Hyon-jong Lee, alisema kwa umuhimu wa kipekee wa uhusiano ya Tanzania na Jamhuri ya Korea, Serikali za nchi hizo zinaendelea na majadiliano ya ufadhili wa miradi yenye thamani ya sh. Bilioni 687.6 itakayotekelezwa nchini Tanzania katika kipindi cha kuanzia mwaka 2018 hadi 2020.

Hafla hizo za kuweka jiwe la msingi katika mradi huo zimefanyika kwenye eneo la Aga Khan na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wakiwemo Mke wa Rais, Mama Janeth Magufuli, Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, Spika wa Bunge, Job Ndugai, Mawaziri, Wabunge, Mabalozi wa nchi mbalimbali, viongozi wakuu wa vyombo vya ulinzi na usalama, viongozi wa dini, viongozi wa vyama vya siasa na viongozi wa mkoa wa Dar es Salaam wakiongozwa na Mkuu wa Mkoa huo, Paul Makonda.

No comments