Breaking News

MBUNGE AYSHAROSE AMWAGA VIFAA KUBORESHA MIUNDOMBINU SHULENI.

MBUNGE Aysharose Mattembe, akiendelea misaada mbalimbali kwa wananchi wake wiki hii.

                              Mwandishi Wetu, Singida

UHABA wa vyumba vya madarasa unaozikabili shule mbalimbali za msingi nchini umeanza kupatiwa ufumbuzi na serikali huku Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, akiungana mkono jitihada hizo kwa vitendo kwa kukabidhi mifuko ya saruji na vifaa vya ujenzi yakiwemo mabati kwa shule za mkoa huo.

Aysharose, ambaye amekuwa akifanya jitihada mbalimbali katika kusaidia wananchi wa Mkoa wa Singida tangu aliposhika nafasi hiyo, ameanza ziara ya kukabidhi vifaa hivyo vya ujenzi tangu Desemba 26, 2018.

Awali, akiwa kwenye ziara za kikazi mwezi uliopita kwenye wilaya mbalimbali za mkoa, mbunge huyo alitembelea shule na kukutana na kero ya uhaba wa vyumba vya madarasa, vyoo kwa wanafunzi hasa wa kike ambapo, aliahidi kwenda kulifanyia kazi na sasa amerejea akiwa na dawa mkononi.

Akizungumza wakati akikabidhi mifuko ya saruji katika Shule za Kata ya Kisiriri, Msisi na Pohama, Aysharose, alisema msaada huo utakwenda kusaidia uboreshwaji wa mazingira na miundombinu ya shule ili wanafunzi watakaporejea waweze kusoma kwa utulivu.

Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, imedhamiria kwa vitendo kuhakikisha watoto wa Kitanzania wanasoma bila vikwazo na kwamba, atahakikisha anaendelea kuunga mkono jitihada hizo bila kukoma.

"Nilifika kwenye shule hizi na kuona changamoto ya uhaba wa madarasa, vyoo na hata nyumba za walimu na mliniambia mahitaji yenu na sasa nimewaletea ili mwakani watoto wakifika hapa wakute mambo tofauti.

“Kama dhamira ya Rais wangu Dk. Magufuli, ya kutaka wanafunzi wasome kwa utulivu, nami ninapenda kuliona hilo likifanyika bila vikwazo.

"Ubunge wangu ni kwa ajili ya wananchi wa Singida hivyo, nitaendelea kupambana kwa hali na mali kwa kile kidogo ninachokipata kuwaletea ili tuijenge Singida yetu. Hakuna mtu wa kuja kutujengea mazingira zaidi ya serikali ya JPM na sisi wenyewe wananchi," alisema Aysharose.

Mbali na Shule za Pohama, Msisi na Kisiriri, shule zingine za wilaya mbalimbali zinatarajiwa kufikiwa na msaada huo wa vifaa vya ujenzi katika mkoa wa Singida, ambapo Aysharose, akiendelea na ziara yake iliyoanza Desemba 26, 2018.

No comments