Breaking News

NAIBU WAZIRI ULEGA AITAKA SUMA JKT KUMALIZA UJENZI WA JENGO LA WIZARA YAKE IFIKAPO DESEMBA 30, MWAKA HUU.


NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega (wa mbele  kulia) akipewa maelezo na Katibu Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuvi, anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Gabriel (wa mbele kushoto), mara baada ya kufikia katika eneo linapojengwa jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi, aliyepo nyuma katikati ni Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dk. Rashid Tamatama.Na Edward Kondela, Dodoma
NAIBU Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, amemtaka mkandarasi SUMA JKT, aliyepewa kazi ya kujenga jengo la Ofisi za  Wizara hiyo katika Mji wa Serikali eneo la Ihumwa, Jijini Dodoma, kuhakikisha jengo hilo linakamilika kwa kiwango na wakati ifikapo Desema 30 mwaka huu.
Akizungumza jana Desemba 3, 2018, mara baada ya kufika katika eneo hilo, kukagua hatua za awali za ujenzi wa jengo la ofisi za wizara hiyo, akiambatana na Makatibu Wakuu wake, anayeshughulika Mifugo Prof. Elisante Ole Gabriel pamoja na wa Mifugo na Uvuvi, Dkt. Rashid Tamatama, Ulega alisema zaidi ya sh. Bilioni moja tayari zimetengwa kwa ajili ya ujenzi wa jengo hilo.
“Sisi tunamuahidi Rais Dk. John Magufuli, wizara yetu imeanza kazi ya kujenga jengo letu hapa Jijini Dodoma kwa kufuata maelekezo yake, hivyo tunatarajia kufika Desema 30 mwaka huu tukabidhiwe jengo hili na tuanze kulitumia mara moja, hivyo mkandarasi SUMA JKT ahakikishe anakamilisha jengo kwa wakati, tunajivunia tunahamia rasmi Dodoma kwa vitendo.” Alisema Ulega.
ULEGA (katikati)  akipewa maelezo ya ujenzi wa jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi katika eneo la Mji wa Serikali Ihumwa mjini Dododma jana, kutoka kwa Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Gabriel (kulia) na Katibu Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Uvuvi Dk. Tamatama (Kushoto.Kwa upande wake Katibu Mkuu  Prof. Ole Gabriel, alimweleza Naibu Waziri Ulega kuwa jengo hilo linalojengwa kwa sasa ni la awali ambalo litaweza kuwahudumia waziri, naibu waziri, makatibu wakuu pamoja na baadhi ya wakurugenzi wa wizara hiyo, kabla ya kuanza kwa ujenzi wa jengo kubwa katika eno hilo la Ihumwa.
“Naibu waziri hili eneo lina ukubwa wa hekari sita na sasa katika hatua za ujenzi tunahakikisha, huduma zote muhimu ziweze kufikishwa hapa tukianza kutumia jengo hili ikiwemo huduma ya maji na umeme. 
“Pia, tunazingatia utunzaji wa mazingira katika ujenzi huu ili eneo hili la Mji wa Serikali liwe la kipekee hususan katika majengo yetu ya wizara ya mifugo na uvuvi yatakayojengwa.” alisema Prof. Gabriel  
Naye Katibu Mkuu Dk. Tamatama alisema katika bajeti ya mwaka wa fedha 2019/2020, Wizara ya Mifugo na Uvuvi, inatarajia kuanza mchakato wa kujenga jengo kubwa katika eneo hilo ambalo litakuwa na uwezo wa kuwahudumia wafanyakazi wote wizara hiyo waliopo makao makuu ya nchi mjini Dodoma.
“Tunajitahidi kuhakikisha tunakamilisha dhamira ya Rais Dk. Magufuli, kuhakikisha tunakuwa na jengo letu na katika bajeti ijayo tunatarajia kutenga fedha ambazo zitawezesha kujenga jengo kubwa, kwa sasa tunajenga hili ambalo litatumika na viongozi kutii agizo la Rais.” alisema Dk. Tamatama.
Eneo la Ihumwa katika mji wa Dodoma ni eneo rasmi ambalo limetengwa na serikali kwa ajili ya ujenzi wa majengo ya serikali yakiwemo ya wizara ikiwa ni sehemu ya utekelezaji wa ofisi za serikali kuhamia rasmi mjini Dodoma, kutokana na agizo lililotolewa na Rais Magufuli wakati akiingia madarakani mwezi Novemba mwaka 2015, ambapo kwa sasa ofisi mbalimbali za serikali zinafanya shughuli zake katika majengo ya kupangisha.


No comments