Breaking News

NHC JENGENI OFISI ZENYE KIWANGO SAWA NA WIZARA YA FEDHA NA MIPANGO-DK. ASHATU KIJAJI.

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji, jana akipata ufafanuzi wa masuala mbalimbali yanayohusu ujenzi wa Ofisi mpya ya Hazina, kutoka kwa Meneja wa Mradi wa  Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Mhandisi. Haikamen Mlekio, alipotembelea eneo la Mji wa Serikali ambapo ofisi ya wizara hiyo inatarajiwa kujengwa, Ihumwa-Dodoma.  (Picha zote na Josephine Majura-Wizara ya Fedha na Mipango).


Na Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma

NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, amelitaka Shirika la Nyumba na Taifa, NHC, lililopewa kandarasi ya kujenga ofisi za Hazina katika eneo la Mji wa Serikali, Ihumwa mkoani Dodoma, kuhakikisha kuwa inajenga ofisi hizo kwa umakini, umahiri na viwango vya ubora wa juu vinavyokwenda sambamba na hadhi ya wizara hiyo.

Dk. Kijaji alitoa rai hiyo jana Desemba 4, 2018, kwa uongozi wa Kampuni ya Ujenzi ya Shirika la Nyumba Tanzania-NHC, baada ya kutembelea eneo zitakapojengwa Ofisi za kudumu za Wizara hiyo katika mji huo wa Serikali ambapo jengo la kwanza litakalo gharimu shilingi bilioni moja, linatarajiwa kukamilika mwishoni mwa mwezi Desemba mwaka 2018.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji. akisisitiza jambo. 

Aidha, Dk. Kijaji ameielekeza NHC kuhakikisha kuwa inajenga jengo kubwa la Wizara kwa kuzingatia teknolojia inayo hifadhi mazingira ikiwemo kuweka miundombinu ya kuwezesha kupatikana kwa nishati mbadala ya umeme katika jengo hilo.


MENEJA  wa mradi wa  ujenzi wa Ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Shirika la Nyumba Tanzania (NHC), Mhandisi Haikamen Mlekio (wa pili kulia) akitoa maelezo kuhusu mradi huo kwa Naibu Waziri wa Fedha na Mipango Dk. Ashatu Kijaji , alipotembelea eneo hilo la ujenzi-Ihumwa, Dodoma.

"Muda wa kukaa mjini Dodoma umemalizika, tunataka ukamilishe jengo hilo kwa wakati na kwa viwango vya juu ili Wizara yote Ihamie hapa Ihumwa na tunataka Bajeti Kuu ya Serikali iandaliwe hapa na ikasomwe Bungeni tukitokea Ihumwa, hilo ni jambo la muhimu sana" aliongeza Dk. Kijaji
Kwa upande wake, Msimamizi wa Ujenzi wa Jengo la Wizara ya Fedha na Mipango kutoka Shirika la Nyumba la Taifa (NHC) Mhandisi Haikamen Mlekio, amemhakikishia Naibu Waziri wa Fedha na Mipango, Dkt Ashatu Kijaji, kwamba watahakikisha majengo ya ofisi za Wizara ya Fedha na Mipango katika Mji wa Serikali wa Ihumwa yanajengwa kwa viwango vya hali ya juu.

No comments