Breaking News

RAIS MAGUFULI AFANYA MAAMUZI MAGUMU * AREJESHA MFUMO WA ZAMANI ULIPWAJI MAFAO KWA WASTAAFU.


 RAIS Dk. John Magufuli, akiwa meza kuu na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama na viongoz wa wafanyakazi na wa mifuko ya hifadhi ya jamii wakiwa wameshikana mikono kwa furaha huku wakiimba wimbo wa hamasa wa mshikamao wa wafanyakazi wa "Solidarity Forever" baada ya kuwasikiliza hoja zao, kuwahutubia na hatimaye kulipatia ufumbuzi suala la vikokotoo vya wafanyakazi alipokutana nao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Desemba 28, 2018. (Picha zote na Ikulu).
                                                       
                                   Na Mwandishi Wetu

RAIS Dk. John Magufuli, ameagiza kurejeshwa kwa utaratibu wa ulipaji wa mafao ya wafanyakazi wanaostaafu uliokuwa ukitumika kabla ya kuunganishwa kwa mifuko ya hifadhi ya jamii, na ametaka utaratibu huo utumike mpaka mwaka 2023 wakati wadau wakijadiliana juu ya kikokotoo kitakachotumika kulipa mafao hayo bila kuathiri mfuko na wastaafu kulipwa vizuri.

Alitangaza uamuzi huo leo Desemba 28, 2018 katika mkutano wake na viongozi wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi (TUCTA), vyama shiriki, viongozi wa mifuko ya hifadhi ya jamii (PSSSF na NSSF), Mamlaka ya Usimamizi wa Mifuko ya Hifadhi ya Jamii (SSRA) na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).

Katika mkutano huo, Magufuli, alisikiliza maoni ya viongozi hao kuhusiana na utekelezaji wa Sheria ya Mfuko ya Hifadhi ya Jamii kwa Watumishi wa Umma namba 2 ya mwaka 2018 na kanuni zake ambapo viongozi hao wameelezea changamoto zilizojitokeza kwa wastaafu kulipwa kiasi kidogo cha fedha za mafao ya mkupuo (25% badala ya 50% ya zamani), na taharuki iliyowakumba wafanyakazi ambao ni wastaafu wa baadaye.

BAADHI ya viongozi hao wakifurahia uamuzi wa Rais Magufuli.

Kabla ya kutangaza uamuzi huo, Magufuli, alisema uamuzi wa Serikali kuunganisha mifuko ya PSPF, LAPF, GEPF na PPF na kuunda mfuko mmoja wa wafanyakazi wa Serikali uitwao PSSSF, na pia kuwa na mfuko mmoja wa wafanyakazi wa sekta binafsi uitwao NSSF ulitokana na mapendekezo ya wadau yaliyolenga kuondoa mkanganyiko wa kikokotoo cha mafao ya wastaafu na pia kuokoa baadhi ya mifuko iliyokuwa mbioni kufa kutokana na kuelemewa na madeni ya wastaafu.

Alibainisha kuwa katika kunusuru hali hiyo, Serikali ya Awamu ya Tano imelipa deni la makato ya wafanyakazi kwa mifuko ya hifadhi ya jamii la shilingi Trilioni 1.23 ambalo lilimbikizwa na pia imewalipa wastaafu waliokwama kulipwa mafao yao kiasi cha shilingi Bilioni 550 kati ya shilingi Bilioni 774 walizokuwa wakidai huku waliobaki wakiendelea kulipwa kadiri uhakiki unavyofanyika.

Hata hivyo, alisema kufuatia hali ya sintofahamu iliyoibuka kutokana na kikokotoo cha mafao kilichotolewa baada ya kuanza kwa utekelezaji wa sheria mpya, Serikali haiko tayari kuona wafanyakazi wanakatishwa tamaa.

Pia, alisema Serikali haiko tayari kuona wastaafu wanapata shida baada ya utumishi mzuri kwa nchi yao, hivyo ameagiza urejeshwe utaratibu uliokuwa ukitumika kabla mabadiliko mpaka mwaka 2023 wadau watakapokubaliana utaratibu unaofaa kwa mifuko kuwepo na wafanyakazi kupata mafao mazuri.
        VIONGOZI hao wakiwa katika nyuso vya furaha

“Serikali hii haipo hapa kukatisha tamaa wafanyakazi, wala haipo hapa kuwaumiza wastaafu, kustaafu sio dhambi na mtu anayestaafu anatakiwa kuheshimiwa kwa sababu katika utumishi wake amejitolea kulitumikia Taifa lake kwa moyo wake wote, ameingia kazini akiwa kijana anaondoka amezeeka,” alisisitiza Magufuli.

Rais Magufuli, alisema katika kipindi cha mpito cha mpaka mwaka 2023 ambapo idadi ya wastaafu watakaolipwa mafao yao itakuwa 58,000 Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu,  Jenista Mhagama na SSRA waisimamie vizuri mifuko ya hifadhi ya jamii ili iepukane na matumizi mabaya ya fedha.

Kadharika, aliwataka mawaziri hao, waboreshe daftari la wastaafu kwa kuondoa wastaafu hewa na ijiepushe na uwekezaji usiokuwa na tija, hali itakayoiwezesha kujiimarisha na kumudu kulipa mafao ya wafanyakazi ipasavyo.
RAIS  Dk. John Magufuli, akiwa meza kuu na Katibu Mkuu Kiongozi Balozi John Kijazi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, ajira na Wenye Ulemavu Jenista Mhagama na viongozi wengine waandamizi   katika picha ya pamoja na viongoz wa wafanyakazi na wa mifujo ya hifadhi ya jamii wakiwa wameshikana mikono kwa furaha huku wakiimba wimbo wa hamasa wa mshikamao wa wafanyakazi wa "Solidarity Forever" baada ya kuwasikiliza hoja zao, kuwahutubia na hatimaye kulipatia ufumbuzi suala la vikokotoo vya wafanyakazi alipokutana nao Ikulu Jijini Dar es Salaam leo Desemba 28, 2018.

Mkutano huo umehudhuriwa na Katibu Mkuu Kiongozi. Balozi John Kijazi, Mwanasheria Mkuu wa Serikali Prof. Adelardus Kilangi, Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango Doto James, Katibu Mkuu Ofisi ya Waziri Mkuu Sera, Bunge, Kazi, Vijana, Ajira na Wenye Ulemavu Andrew Massawe na Katibu Mkuu Ofisi ya Rais Ikulu Dk. Moses Kusiluka.

No comments