Breaking News

SERIKALI IMETOA KIPAUMBELE MATUMIZI YA TEHAMA NCHINI-MAJALIWA * ATOA ONYO KWA WANAOTUMIA VIBAYA MITANDAO YA KIJAMII, ASISITIZA SHERIA IPO.


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa akimkabidhi Tuzo mshindi wa kwanza wa Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI, Emmanuel  Chaula, wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam katika sherehe za kukabidhi Tuzo hizo kwenye Hoteli ya Hayyat Regency,  Jijini Dar es Salaam, leo  Desemba 5, 2018. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Na Mwandishi Wetu

WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa amesema Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dk. John Magufuli, imetoa kipaumbele kwenye matumizi ya TEHAMA ili kuongeza uwazi, uwajibikaji na ufanisi katika utendaji kazi wa shughuli za Serikali za kila siku. 

Hivyo, amewataka wananchi kutumia vizuri teknolojia hiyo ya habari na mawasiliano kwenye shughuli za uzalishaji mali na utoaji huduma katika sekta mbalimbali kwa lengo la  kukuza uchumi na kuwapunguzia wananchi umaskini pamoja na kuongeza ajira.
MAJALIWA, akizungumza wakati alipokabidhi Tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI.

Waziri Mkuu aliyasema hayo leo Desemba 5, 2018 katika sherehe za utoaji tuzo za mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI yaliyofanyika Jijini Dar es Salaam, ambapo ametumia fursa hiyo kuwaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii nchini.

“Nawaonya watu wote wanaotumia vibaya mitandao ya kijamii waache. Ni vema wakatumia mitandao hiyo kwa kuhamasishana mambo mema zikiwemo shughuli mbalimbali  za maendeleo. Na kwa wataokiuka sheria ipo na inaendelea kufanya kazi,” alisema.
WAZIRI Mkuu Majaliwa, akisalimiana na Balozi wa China Nchini, Wang Ke, wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Hayyat Regency, Dar es Salaam, kutoa Tuzo za mashindano hayo.  Wapili kushoto ni Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa  Joyce Ndalichako  na kulia ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye. 

Aliema, Serikali inaamini kuwa matumizi ya TEHAMA yataongeza ufanisi katika kuwahudumia ipasavyo wananchi, mfano katika sekta ya elimu mwalimu mmoja anaweza kufundisha wanafunzi wengi kutoka katika shule tofauti kwa wakati mmoja. 

Waziri Mkuu aliongeza kuwa “Matumizi ya TEHAMA kwa kiasi kikubwa yatapunguza gharamaza za uendeshaji kwani yanaweza kufanikisha mawasiliano binafsi, warsha na maelekezo mbalimbali kuwafikia walengwa bila ya kusafiri nje ya vituo vyao vya kazi.”

Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa, akitia saini katika bango wakati alipowasili kwenye Hoteli ya Hayyat Regency,  Dar es Salaam kutoa Tuzo za mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI

Alitoa mfano, Juni 2017 Rais Dk. Magufuli, alizindua mfumo wa ukusanyaji Mapato ya Kodi ya Ongezeko la Thamani (VAT) na Ushuru wa Bidhaa (Excise Duty) kwa njia ya kielektroniki na kudhihirisha kuwa, sekta ya teknolojia ya habari na mawasiliano ni muhimili muhimu wa maendeleo kwenye sekta zote, ikiwemo viwanda, utalii, ujenzi, elimu, afya, kilimo, uvuvi na ufugaji.

“Kwa kuzingatia hayo, mwezi Juni 2018 wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma, Serikali ilizindua mifumo tisa ya TEHAMA, ambayo inalenga kuimarisha utendaji wa serikali hususan katika kuwahudumia wananchi kwenye sekta mbalimbali ikiwemo afya, ukusanyaji mapato na utoaji wa taarifa,”alisema Majaliwa.

KASSIM Majaliwa akiwa katika picha ya pamoja na viongozi walioshiriki katika sherehe za Utoaji Tuzo za Mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI kwenye Hoteli ya Hayyat Regency, Dar es Salaam. Kutoka kushoto ni Naibu Waziri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi, Atashasta Nditiye, Waziri wa Elimu, Sayansi na Tekinolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Afisa Mtendaji Mkuu wa Kampuni ya HUAWEI nchini, Frank Zhou na  Balozi wa China nchini, Wang Ke.


Kadhalika, Waziri Mkuu alisema Serikali itaendelea kuwekeza kwa kiasi kikubwa katika kutengeneza mifumo ya TEHAMA ili kutekeleza kwa vitendo azmaya kuwapatia wananchi maendeleo hususani waishio maeneo ya vijijini huduma bora na kwa wakati.

Alisema kwa sasa Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) inauwezo wa kuona na kubaini makusanyo yanayoendelea kukusanywa katika halmashauri mbalimbali nchini na kiasi kinachoingizwa benki kwa kupitia TEHAMA.

WAZIRI  Mkuu, Kassim Majaliwa, akiongozana na Balozi wa China nchini,  Wang Ke, (wapili kulia) na Waziri Profesa.  Joyce Ndalichako

Kwa mujibu wa Waziri Mkuu, Serikali inaendelea kuunganisha Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano kwenye taasisi zake ili kufanikisha azma ya serikali kutumia  mtandao, utaratibu ambalo unakwenda sambamba na kuunganisha baadhi ya shule
za msingi, shule za sekondari, ofisi za wakuu wa wilaya, polisi, hospitali za wilaya, vyuo vikuu na vituo vya posta.

Wakati huo huo, Waziri Mkuu aliipongeza Kampuni ya HUAWEI kwa uzinduzi wa Program yao ya Seed of the Future ambayo inalengo la kuwajengea uwezo wa TEHAMA wanafunzi mbalimbali nchini katika hatua za awali kabisa. 


WAZIRI Mkuu, Kassim Majaliwa na Viongozi wa Kitaifa na Kimataifa wakiwa katika picha ya pamoja na washindi wa mashindano ya TEHAMA ya HUAWEI baada ya kuwakabidhi Tuzo za ushindi  washindi hao kwenye Hoteli ya Hayyat Regency, Dar es Salaam.

Alisema iwapo TEHAMA itatumika vizuri itatoa fursa kwa watu wote kupata elimu, kuleta usawa katika elimu, kujenga mazingira na mbinu bora za ufundishaji na kujifunza, kuongeza weledi wa walimu, kuimarisha usimamizi wa masuala ya elimu, uongozi na utawala.  

Mashindano hayo ya TEHAMA ya HUAWEI yaliasisiwa mwaka 2015 na baadaye mwaka 2016 yakazinduliwa huko Afrika Kusini, ambapo hadi kufikia mwaka 2017 tayari wanafunzi wapatao 40,000 wameshiriki mashindano hayo. 

                                     MAJALIWA akihutubia

Kwa upande wa Tanzania, yalizinduliwa mwaka huu, ambapo wanafunzi 500 walishiriki na baadaye kubaki 50, ambapo  waliokabidhiwa tuzo ni saba na watatu kati yao ni mkufunzi mmoja wamepata fursa ya kushiriki hatua inayofuata ya mashindano hayo nchini Afrika Kusini. 

Sherehe hizo zimehudhuliwa na Balozi wa China nchini Tanzania, Wang Ke, Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, Naibu Wazri wa Ujenzi, Uchukuzi na Mawasiliano, Mhandisi Atashasta Nditiye, Mkurugenzi Mtendaji wa HUAWEI Tanzania Frank Zhou na wawakilishi mbalimbali wa taasisi za Umoja wa Mataifa Nchini.

No comments