Breaking News

SERIKALI YAIAGIZA BODI YA WATAALAM WA UNUNUZI NA UGAVI KUDHIBITI MAADILI YA WATAALAM WA UNUNUZI NA UGAVI.

KAIMU Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Fedha na Mipango, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Idara ya Mipango wa Wizara hiyo, Richard Mkumbo, akifunga Kongamano la Tisa la Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPTB), kwa niaba ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara hiyo, Susana Mkapa, ukumbi wa DCC, Dodoma jana Desemba 6, 2018. (Picha zote na Josephine Majura-WFM).

                         Na Josephine Majura, WFM, Dodoma

NAIBU Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Susana Mkapa, ameiagiza Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi Nchini (PSPTB), kuhakikisha kuwa inadhibiti maadili ya wafanyakazi wa sekta ya ununuzi na ugavi ili fedha za Serikali zinazotumika kwenye ununuzi ziwe na tija kwa wananchi.

Susana, alitoa maagizo hilo jana Desemba 6, Jijini Dodoma, katika hotuba iliyosomwa kwa niaba yake na Kaimu Naibu Katibu Mkuu, ambaye pia ni Mkurugenzi wa Mipango wa Wizara ya Fedha na Mipango, Richard Mkumbo, wakati akifunga kongamano la tisa la wataalam wa ununuzi na ugavi kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

Akizungumza kwa niaba ya Susana, Mkumbo alibainisha kuwa licha ya vitengo vya matumizi mabaya ya fedha za umma kupitia sekta ya ununuzi na ugavi, ikiwemo rushwa kuendelea kupungua, bodi inatakiwa kuhakikisha kuwa vitendo vya rushwa vinadhibitiwa ipasavyo.


BAADHI ya Washiriki wa Kongamano la Tisa la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPSTB), wakiimba wimbo wa Taifa wakati wa hafla ya kufunga kongamano hilo la siku tatu lililofanyika Jijini Dodoma na kuwashirikisha wataalam 650 kutoka Tanzania Bara.

Kwa mujibu wa Mkumbo, asilimia 75 ya fedha za umma zinatumika kupitia mchakato wa manunuzi ambao taarifa ya mdhibiti na mkaguzi wa hesabu za serikali (CAG) na Mamlaka ya Ununuzi nchini PPRA, umebaini kuwepo kwa viashiria vya rushwa katika utekelezaji wa miradi mbalimbali ya wananchi.

Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Bodi ya Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi, Sister Dk. Hellen Bandiho, alisema kuwa bodi yake itahakikisha inasimamia kikamilifu maadili ya watumishi wa sekta ya ununuzi ili iweze kushiriki katika kukuza uchumi wa viwanda.
BAADHI ya Washiriki wa Kongamano la Wataalamu wa Ununuzi na Ugavi (PSPSTB), wakifuatilia hotuba ya mgeni rasmi,  Kaimu Naibu Katibu Mkuu Wizara ya Fedha na Mipango, Richard Mkumbo (hayupo pichani), wakati  akifunga kongamano hilo. 

Kongamano hilo limewashirikisha wataalam wa ununuzi na ugavi wapatao 650 kutoka mikoa yote ya Tanzania Bara.

No comments