Breaking News

SERIKALI YASTUSHWA KUONGEZEKA KWA IDADI YA WAGONJWA WA SARATANI .Na.WAMJW-LINDI

SERIKALI Kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, imesema kuwa kutoka kipindi cha mwaka 2002 mpaka hivi sasa kumekuwa na ongezeko kubwa la wagonjwa wa Saratani kutoka.

Ilisema, mwaka 2002 kulikuwa na wagonjwa 2500 na mpaka kufikia mwaka jana idadi hiyo imeongezeka na kufikia 6500, kutokana na mitindo tofauti ya maisha na mabadiliko ya sayansi na  teknolojia.


Hayo yalisemwa jana Desemba 22 2018 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, wakati akiwa katika ziara ya kukagua hali ya utoaji huduma za afya na uhamasishaji kwa wakulima kujiunga na mfuko wa Bima ya afya (#UshirikaAfya) katika Mkoa wa Lindi.


"Serikali imeshtushwa na ongezeko la wagonjwa wa Saratani  na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza, mwaka 2002 wagonjwa wa Saratani nchini walikuwa kati 1500 mpaka 2000, lakini kwa takwimu za mwaka Jana, wameongezeka kutoka 2500 hadi 6500" alisema Waziri Ummy.


Aliendelea kusema kuwa Serikali imeona upo ulazima wa kuchukua hatua za makusudi katika kupambana na Saratani ya mlango wa kizazi na magonjwa mengine yasiyo ya kuambukiza yakiwemo shinikizo la damu, magonjwa ya moyo na ugonjwa wa Kisukari.

Pia, Waziri Ummy, alisema kuwa katika kila wagonjwa 100 wa Saratani, 34 kati yao huugua Saratani ya Mlango wa Kizazi, 12 Saratani ya Matiti na kibaya zaidi katika kila wagonjwa 100 wa Saratani, 80 wanafika hospitali wakiwa wamechelewa kuanza matibabu na wengine ugonjwa ukiwa katika hatua ya tatu au ya nne, hivyo kupona kwao kunakuwa ni kugumu.
WAZIRI Ummy Mwalimu, akimjulia hali mtoto aliyefika kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi, wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi.


Awali akisoma taarifa ya mkoa, Katibu tawala Mkoa wa Lindi, Rehema Madenge, alisema kuwa mkoa umeweza kuanzisha utoaji wa chanjo ya kukinga  Saratani ya Mlango wa Kizazi (HPV) kwa wasichana wa umri wa miaka 9 hadi 14.

Hata hivyo, Rehema alisema kuwa, katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya mahudhurio 164,259 yalirekodiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za afya vya serikali, binafsi na vile vya dini huku Hospitali ya Mkoa Sokoine ikirekodi mahudhurio 39,324 na kulipwa sh. 1,654,964,965 katika kipindi hicho.

 Ummy, akikagua miundombinu  katika chumba cha X- ray  wakati alipofanya ziara ya kukagua hali ya utoaji Huduma za Afya kwa wananchi katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Lindi.
"Mkoa umeendelea kuhudumia wanufaika wa Bima ya Afya ya Taifa (NHIF) kwa ufanisi mkubwa na katika mwaka wa fedha wa 2017/2018 jumla ya mahudhurio 164,259 yalirekodiwa katika vituo vyote vya kutolea huduma za Afya vya Serikali, binafsi na vile vya dini" alisema Rehema.

Aidha,  alisema kuwa ili kuweza kuwafikia wananchi wengi kupitia makundi mbali mbali, mfuko wa Taifa wa Bima ya Afya umekuja na mpango uitwao #Ushirika Afya ambapo wakulima wanaungana pamoja katika vyama vyao vya mazao na kuweka mkakati wa kujiunga na Bima ya Afya kwa utaratibu wa ushirika wao.


No comments