Breaking News

SERIKALI YAWATAKA WATANZANIA KUSHIRIKI KATIKA KUIMARISHA UTAWALA BORA ILI KUTOA MCHANGO KATIKA MAENDELEO YA TAIFA.


NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akifafanua jambo kabla ya Waziri wake, Kapeteni mstaafu. George Mkuchika, kuzungumza na wadau wa maadili na haki za binadamu, wakati wa uzinduzi wa maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, jijini Dodoma jana. (Picha zote na James Mwanamuyoto )


                                 Na Mwandishi Wetu, Dodoma

SERIKALI imewataka Watanzania wote kushiriki katika kuimarisha utawala bora nchini ili kutoa mchango wenye tija kwa maendeleo ya taifa badala ya kuviachia jukumu hilo vyombo vinavyosimamia masuala ya utawala bora.

Wito huo ulitolewametolewa jana Desemba 4, 2018 na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Kapt (Mst) George Mkuchika, wakati  akizindua maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa, Jijini Dodoma.

Mkuchika alisema, ili kuwa na utawala bora katika nchi yetu, Watanzania wote wanahusika kwa maana ya wale waliopewa dhamana ya kusimamia utawala bora na wananchi wa kawaida, kwani wenye dhamana ya kusimamia utawala bora wanahitaji ushirikiano kutoka kwa wananchi ili waweze kutekeleza majukumu yao kikamilifu.
WAZIRI Mkuchika, akizungumza na wadau wa maadili na haki za binadamu

Aliongeza kuwa,  Mtanzania wa kawaida anatakiwa abadilike kimtazamo na kifikra kuhusu uzingatiaji wa maadili, nidhamu ya kazi, vita dhidi ya rushwa, haki za binadamu, uwazi na uwajibikaji, na kusisitiza kuwa mabadiliko haya yawe ndio utamaduni wa mtanzania wa kila siku.

Wairi huyo alifafanua kuwa, duniani kote suala la utawala bora linapewa kipaumbele, kwasababu bila nchi kuwa na mfumo madhubuti wa maadili kuanzia ngazi ya familia haiwezi kufanikisha vita dhidi ya mmomonyoko wa maadili. Aidha, ametoa wito kwa Watanzania wote nchini kuwa waadilifu ili kuwa mfano wa kuigwa na vizazi vijavyo.

Naye, Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dk. Mary Mwanjelwa,  aliwataka wananchi kuwa wazalendo kwa kutanguliza masilahi ya umma kwa ajili ya maendeleo ya Taifa.

WAZIRI Mkuchika na Naibu wake Mary, wakifurahia jambo pamoja na viongozi wengine.

Mwanjelwa alisema, kupitia kauli mbiu ya maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu ya mwaka huu inayosema “Udhibiti wa Mgongano wa Masilahi-Nguzo Muhimu Kujenga Utawala Bora” ni vema kwa kila mtu kutanguliza masilahi ya umma mbele badala ya masilahi binafsi ili kufikia lengo la uchumi wa kati wa viwanda kama inavyohimizwa na Rais Dk. John Magufuli.

Kwa mujibu wa Mwanjelwa, utekelezaji wa kauli mbiu hii ni muafaka kwasasa kwani taifa liko katika utekelezaji wa miradi mikubwa ya maendeleo ambapo uzalendo na uadilifu ni nguzo kuu itakayowezesha utekelezaji wa miradi hiyo.

Awali,  akitoa neno la utangulizi, Kamishna wa Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma, Jaji mstaafu. Harold Nsekela, alisema, maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa ni muhimu kwani yanahimiza na kutukumbusha kuzingatia misingi ya maadili, haki za binadamu, uwajibikaji, mapambano dhidi ya rushwa hasa kwa watumishi wa umma ambao jukumu lao kubwa ni kutoa huduma kwa wananchi.

WAZIRI Mkuchika na  Naibu wake, Mary, wakimkabidhi zawadi  Mlezi wa Klabu ya Maadili wa shule ya Sekondari Dodoma, mwalimu Marco  Magwa,  mara baada ya kuzindua maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa,  Jijini Dodoma jana. Kushoto ni Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Patrobas Katambi.Maadhimisho ya Siku ya Maadili na Haki za Binadamu Kitaifa huratibiwa na Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa, Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Mamlaka ya Udhibiti wa Manunuzi ya Umma, Ofisi ya Taifa ya Ukaguzi wa Hesabu za Serikali, Tume ya Utumishi wa Umma, Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, lengo likiwa ni kuhamasisha uadilifu, uwazi, uwajibikaji na utawala bora nchini.

No comments