SERIKALI YAZISHAURI BENKI NCHINI KUSHUSHA RIBA ZA MIKOPO KUCHOCHEA UCHUMI WA VIWANDA.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akihutubia
wakati wa ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine, Jijini Dodoma, jana
Desemba 6, 2018. (Picha na Saidina Msangi-WFM).
Benny Mwaipaja, WFM, Dodoma
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango,
Dk. Ashatu Kijaji, amezitaka benki nchini, kushusha viwango vya riba za mikopo
ili kuwawezesha wananchi wengi zaidi wakiwemo wakulima kunufaika na huduma za
kifedha zinazotolewa na taasisi hizo za fedha kwa ajili ya kujiletea maendeleo
yao.
Dk. Kijaji aliyasema hayo Jijini
Dodoma jana Desemba 6, 2018, wakati akifungua rasmi Tawi la Benki Azania,
Sokoine, na kusisitiza kuwa benki zina nafasi kubwa wa kuisaidia nchi kufikia
azma yake ya kuwa ya viwanda ifikapo mwaka 2025 kwa kukuza mitaji na biashara
za wananchi.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji (katikati),
akiwa katika ufunguzi wa tawi jipya la Benki ya Azania, Sokoine, Jijini Dodoma.
Kulia ni Mkurugenzi wa Benki hiyo Charles Itembe, na Mwenyekiti wa Bodi ya
Benki hiyo Eliud Sanga.
Alisema
kuwa hivi karibuni Serikali imechukua hatua madhubuti za kiutawala na kisera
ili kuhakikisha kuwa riba za mikopo katika soko zinapungua, ikiwemo Benki Kuu kutoa
mikopo ya muda mfupi kwa benki za biashara, kushusha riba kutoka asilimia
16.0 hadi asilimia 9.0.
"Tumepunguza
kiwango cha chini cha amana kinachotakiwa kuwekwa Benki Kuu na benki za
biashara kutoka asilimia 10.0 hadi asilimia 8.0, hatua ambazo zimesaidia
kupunguza riba katika soko kutoka wastani wa zaidi ya asilimia 20 hadi asilimia
17.
Dk. Ashatu, akipokea zawadi kutoka kwa Mwenyekiti wa bodi ya
Benki ya Azania, Eliud Sanga, baada ya kuhutubia katika ufunguzi wa tawi la
benki hiyo la Sokoine Jijini Dodoma.
"Kama
haya yote yamefanyika, iweje benki ziendelee kutoza riba ya asilimia 17 kwa
kisingizio cha kuogopa mikopo chechefu wakati Serikali kupitia Benki Kuu,
imeanzisha kanzi data ya kuhifadhi na kutoa taarifa ya wakopaji? (Credit
Reference Bureau System)," alihoji Dk. Kijaji
Aidha,
Dk. Kijaji, alielezea kusikitishwa kwake na hatua ya benki hiyo kuwa miongoni
mwa benki 5 zilizofungiwa kwa kipindi maalum kushiriki katika kuuza na kununua
fedha za kigeni baada ya kukiuka taratibu za biashara hiyo.
NAIBU Waziri Dk. Ashatu Kijaji, akikata utepe kuashiria ufunguzi
rasmi wa tawi jipya la benki hiyo.
" Kisheria, benki zote za
biashara zinatakiwa kutoa taarifa Benki Kuu kuhusu miamala ya Soko la Fedha za
Kigeni kati ya benki waliyofanya kwa siku, lakini benki yako ni miongoni mwa
benki zilizovunja utaratibu huu, hii niaibu!," alisisitiza Dk. Kijaji.
Mkurugenzi
Mtendaji wa Benki ya Azania, Charles Itembe, alisema benki yake imeendelea
kufanya vizuri katika soko kwa kupata faida na kwamba imejipanga kutoa mikopo
na huduma za kifedha kwa wananchi mkoani Dodoma kwa viwango vya juu.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akiagana na
Mkurugenzi wa Benki ya Azania, Charles Itembe, mara baada ya kukamilisha
ufunguzi rasmi wa tawi hilo.
"Benki
yetu, mwaka 2017, imetengeneza faida ya shilingi bilioni 1.81 ikilinganishwa na
hasara ya Shilingi bilioni 6 iliyoripotiwa Desemba 2016, na imeongeza
rasilimali zake kutoka sh. bilioni 338 hadi bilioni 390," alisema Itembe.
Dk. Ashatu Kijaji, akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti
na wageni waliokuwa meza kuu mara baada ya kufungua rasmi Tawi la Benki ya
Azania.
Alisema kuwa benki yake imeongeza kiasi cha
mikopo iliyotoa kutoka sh. bilioni 129 mwaka 2016 hadi sh. bilioni
187.7 mwaka 2017, sawa na ongezeko la asilimia 10.23 huku akiba za
wateja zikiongezeka kutoka shilingi bilioni 236 mwaka 2016 hadi sh. bilioni 271
mwaka jana.
NAIBU Waziri wa Fedha na Mipango, Dk. Ashatu Kijaji, akiwa
katika picha ya pamoja na wadau wa benki ya Azania ambao walihudhuria katika
ufunguzi wa tawi hilo jipya.
Naye Mwenyekiti wa Bodi ya Wakurugenzi wa
Benki ya Azania ambaye pia ni Mkurugenzi Mkuu wa Mfuko wa Hifadhi ya Jamii ya
Watumishi wa Umma (PSSSF), Eliud Sanga, aliitaka benki hiyo kutekeleza mkakati
wake wa kuanza kutoa mikopo ili kuimarisha sekta ya ujenzi wa viwanda nchini.
No comments