Breaking News

UTUMISHI YAUNGA MKONO KWA VITENDOFISI KAMPENI YA MAKAMU WA RAIS, SAMIA SULUHU HASSAN YA KULIFANYA JIJI LA DODOMA KUWA KIJANI.


KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Utawala na Usimamizi wa Rasilimaliwatu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Musa Joseph, akishiriki kuchimba mashimo kwa ajili kupanda miti Ihumwa katika Mji wa Serikali Jijini Dodoma leo Desemba 29, 2018.
Na James  Mwanamyoto, Dodoma
OFISI ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, imeunga mkono kwa vitendo kampeni iliyozinduliwa na Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan, ya kulifanya Jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kupanda miti katika ofisi yake inayojengwa  Ihumwa kwenye Mji wa Serikali.
Hayo yamesemwa leo Desemba 29, 2018 na Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma  Dk. Laurean Ndumbaro, mara baada ya watumishi  wa ofisi yake kukamilisha kazi ya kupanda  miti katika mji huo,  eneo ambalo  kunajengwa ofisi za wizara hiyo ili kutoa huduma kwa umma.
Dk. Ndumbaro, alisema kazi ya kupanda wa miti katika eneo hilo ni endelevu na kwamba ofisi yake itahakikisha miti hiyo inatunzwa kwa kuimwagilia maji ili hatimaye kuwe na mandhari ya kijani.
MKURUGENZI wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mathew Kirama, akishiriki kupanda miti Ihumwa katika Mji huo wa Serikali.
Naye, mmoja wa watumishi wa Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Menyeaichi Koka, alisema watumishi wa ofisi hiyo wameitikia wito wa Makamu wa Rais, Samia Suluhu Hassan wa kupanda miti ili kulifanya Jiji la Dodoma kuwa kijani na kuishukuru menejimenti ya  ofisi kwa kusimamia vizuri kazi hiyo ambayo kila mtumishi aliifanya kwa hiyari na kwa moyo mkunjufu.
Menyeachi, ahaidi kuuhudumia vizuri mti alioupanda kwa kuumwagilia maji ya kutosha ili uweze kustawi vizuri na kuwa  miongoni mwa miti iliyopandwa na kufanikiwa kukua vizuri na hatimaye kuchangia Jiji  la Dodoma kuwa kijani.

BAADHI ya  watumishi wa  Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, wakijiandaa kupanda miti katika ofisi yao inayojengwa Ihumwa kwenye Mji wa Serikali Jijini Dodoma ikiwa ni hatua ya  kuunga mkono kwa vitendo kampeni ya kulifanya jiji hilo kuwa la kijani. (Picha zote na James Mwanamyoto).

Makamu wa Rais  Samia Suluhu Hassan, Julai 21, 2017, alizindua kampeni za kulifanya Jiji la Dodoma kuwa kijani kwa kuongoza kazi ya kupanda miti ikiwa ni sehemu ya  kuunga mkono kwa vitendo uamuzi wa Rais Dk. John Magufuli, wa kuhamishia Makamo Makuu ya Nchi kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma.

No comments