Breaking News

WADAU WA UVUVI WA IGONBE WAKUBALIANA KUUNDA USHIRIKA. WATAKA UZINDULIWE RASMI NA WAZIRI MPINA. KIONGOZI wa Dawati la Sekta Binafsi timu ya Kanda ya Ziwa Anthony Dadu,akitoa maelezo ya umuhimu wa kuunda ushirika kwa vikundi kwa wadu wa uvuvi katika mwalo wa Igombe Mkoani Mwanza jana
Na Edward Kondela, Mwanza

WADAU wa uvuvi katika Mwalo wa Igombe Mkoani Mwanza, wameridhia kwa kauli moja kuunda ushirika, baada ya kupata darasa kutoka kwa wataalamu wa Dawati la Sekta Binafsi kutoka Wizara ya Mifugo na Uvuvi.

Hayo yalibainishwa leo Desemba 02, 2018 wakati wadau hao walipokutana na wataalamu wa dawati hilo, kwa lengo la kuelimishwa umuhimu wa kuunda ushirika kwa vikindi hivyo vya wavuvi, wakala na wachuuzi wa samaki na dagaa katika mwalo wa Igombe mkoani Mwanza.

Kiongozi wa Dawati la Sekta Binafsi timu ya Kanda ya Ziwa  Anthony Dadu, aliwaambia wadau hao kuwa, kujiunga katika ushirika kutawasaidia kuwa na chombo cha kuwasemea masuala yao na kuwatetea kupata haki zao na maoni mbalimbali kama vile kutafutata masoko yenye faida kwa bidhaa  kupitia ushirika.

Kwa mujibu wa Dadu, wadau hao watapata mikopo kutoka taasisi za fedha zinazotoa mikopo yenye riba nafuu kwa vyama vya ushirika pekee kama vile Benki ya Maendeleo ya Kilimo (TADB).

Wakiendelea kutoa maelezo ya umuhimu wa ushirika kwa wadau hao wa uvuvi, Mtaalamu wa Dawati kutoka TADB, Zakayo Penuel, alisema kuwa benki hiyo ilianzishwa kwa lengo la kusaidia kutoa mikopo kwa vikundi vya wajasiriamali waliojiunga katika ushirika ulioimara wasaidiwe kupata mikopo kwa masharti nafuu ili waboreshe uwekezaji wao na kuwa wenye tija endelevu.

Penuel, aliongeza kuwa baadhi ya mikopo inayotolewa kwa wavuvi ni pamoja na ununuzi wa boti ya kisasa inayoweza kuvua kina kirefu ili kupata samaki wengi wakubwa na bora, injini za boti, nyavu bora na sahihi kwa uvuvi endelevu, mashine kubwa na bora za kugandisha barafu, kujenga vyuma vya baridi, magari ya kusafirishia samaki na bidhaa za samaki pamoja na mkopo kwa ajili ya kujenga viwanda vya kati vya kuchakata samaki vinavyomilikiwa na ushirika wa wavuvi wenyewe.


  BAADHI ya wadau wa uvuvi katika mwalo wa Igombe, Mkoani Mwanza wakifuatilia maelezo yanayotolewa na Kiongozi wa Dawati la Sekta Binafsi timu ya Kanda ya Ziwa Bw. Anthony Dadu (hayupo pichani)


Aidha aliwaeleza wadau wa uvuvi kuwa kama wakipata mikopo hiyo wataboresha uwekezaji wao na kufanya kibiashara shughuli za uvuvi na kuziweka katika mnyororo wa samani, hivyo kuwa na uzalishaji wenye tija endelevu itakayowanufaisha wanaushirika wote kwa kipato na faifa kwa ujumla.

Naye Diwani wa kata ya Igombe, William Mashamba aliwasihi wadau uvuvi hawana budi budi kuunga mkono suala hilo na kuanza mchakato wa kuunda ushirika kwa kipindi kifupi, na kuonesha nia ya kumwalika Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Luhaga Mpina kuzindua ushirika wao.

Wadau wa uvuvi katika mwalo wa Igombe walikubaliana kwa pamoja kuanza mchakato wa kuunda ushirika ikiwa ni pamoja na kupata wataalamu wa idara ya ushirika kuanza kuwafundisha taratibu za kuanzisha ushirika.

Aidha walisema ikiwezekana kiwe chama cha kwanza kuanzishwa na kiwe cha mfano katika kanda ya Ziwa Victoria na kumuomba Waziri wa Mifugo na Uvuvi kuwa mgeni rasmi katika uzinduzi wa ushirika huo Desemba 29, 2018.

No comments