Breaking News

WATUMISHI WA UMMA WATAKIWA KUWA TAYARI KUFANYA KAZI MAHALI POPOTE NCHINI ILI KUWAHUDUMIA WANANCHI.NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dk. Mary Mwanjelwa, akisisitiza jambo kwa watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma katika wizara yake (hawapo pichani) alipotembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu yake na kuhimiza uwajibikaji jana Jijini Dodoma. (Picha zote na Jamws Manamyoto).

Na James Mwanamyoto, Dodoma

WATUMISHI wa umma wametakiwa kuwa tayari kufanya kazi mahali popote na katika mazingira yoyote nchini ili waweze kuwahudumia wananchi ambao ndio walengwa wakuu wa huduma zinazotolewa na Taasisi za Umma.

Hayo yalisemwa leo Desemba 19, 2018 na Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, alipokutana na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora kwa lengo la kufahamu majukumu ya Idara hiyo na kuhimiza uwajibikaji.

Dk. Mary, alisema, kitendo cha watumishi wa umma kuwa tayari kufanya kazi mahali popote na katika mazingira yoyote bila kujali maslahi binafsi kinaashiria uzalendo kwa Taifa na kinatoa haki kwa wananchi katika maeneo yote hususan ya pembezoni kupata huduma bora wanayostahili.

Mary,  aliitaka Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma kutorubuniwa na baadhi ya watumishi na waajiri wanaoomba vibali vya uhamisho kwa maslahi binafsi hivyo kuathiri utoaji huduma kwa umma.

Naibu Waziri huyo, aliongeza kuwa Idara hiyo inatakiwa kujiridhisha na hoja zinazowasilishwa kuombea vibali vya uhamisho kama hoja hizo zina tija na manufaa katika maendeleo ya Taifa.

Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora alipoitembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji.

Alisisitiza kuwa, Watanzania wote wana haki sawa ya kupata huduma bora bila kujali mazingira waliyopo hivyo, ni wajibu wa Idara hiyo kuhakikisha kuwa uhamisho wa watumishi hauathiri mahitaji ya huduma kwa wananchi.

Awali, akielezea majukumu ya idara yake, Mkurugenzi wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Mathew Kirama, alisema Idara hiyo ina sehemu ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Watumishi Waandamizi.

Pia, ina sehemu ya Huduma na Ushauri wa Kisheria ambazo kwa pamoja zinalenga kufanikisha uendeshaji wa utumishi wa umma kwa kuwezesha taasisi za serikali kupata watumishi wenye sifa na weledi unaohitajika kulingana na malengo yanayotekelezwa na taasisi hizo.

Alifafanua kuwa, idara hiyo  ina jukumu la kutoa ushauri wa kitaalamu kwa waajiri na watumishi kuhusu sera, sheria, kanuni na nyaraka mbalimbali za masuala ya ajira katika Utumishi wa Umma, kutoa ushauri wa kitaalamu kuhusu masuala ya sheria ikiwa ni pamoja na kusimamia taratibu mbalimbali zinazotawala utumishi wa umma.


MKURUGENZI wa Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Mathew Kirama (wa pili kulia), akifafanua majukumu ya Idara yake kwa Naibu Waziri, Dk. Mary Mwanjelwa, (kulia) alipoitembelea idara hiyo kwa lengo la kufahamu majukumu ya idara na kuhimiza uwajibikaji. 

Azungumzia suala la uhamisho,  Kirama alisema katika kuleta tija na ufanisi kwenye utumishi wa umma, wafanyakazi tumishi wa umma wanaruhusiwa kuhama ikiwa wamezingatia sheria, kanuni, taratibu na miongozo iliyopo likiwemo sharti la kukaa kwenye kituo kimoja cha kazi si chini ya miaka mitatu na kuwe uwepo wa nafasi iliyotengewa fedha kwenye kituo husika.


Aidha alieza kuwa, Serikali inaweza kumhamisha mtumishi kwa sababu mbalimbali ikiwa ni pamoja na kuboresha huduma katika maeneo yenye upungufu wa watumishi.

Naibu Waziri Dk. Mary, alitembelea Idara ya Utawala wa Utumishi wa Umma ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake katika Idara na Vitengo vya Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora ili kuhimiza uwajibikaji.

No comments