Breaking News

WAZIRI KALEMANI ATOA ONYO KALI KWA WATAKAOBAINIKA KUHUJUMU MIUNDOMBINU YA UMEME.


             
WAZIRI wa Nishati, Dk. Medard Kalemani, akiwasha umeme katika nyumba ya mmoja wa wakazi wa Kijiji cha Ibindo, wilayani Kwimba, akiwa katika ziara ya kikazi jana Desemba 29, 2018. Kulia kwake ni Mbunge wa Jimbo la Sumve, Richard Ndasa.

                   Na Veronica Simba, Kwimba

Waziri wa Nishati Dk. Medard Kalemani, amefanya ziara wilayani Kwimba, mkoa wa Mwanza na kutoa onyo kali kwa watu wenye tabia ya kuhujumu miundombinu ya umeme pamoja na vishoka.

Akizungumza jana Desemba 29, 2018, kwa nyakati tofauti katika Vijiji vya Ngulla na Ibindo, akiwa kwenye ziara ya kikazi kukagua utekelezaji wa miradi ya umeme, kuwasha umeme na kuzungumza na wananchi, Waziri Kalemani alitahadharisha kuwa Serikali haitamvumilia yeyote atakayebainika kufanya uharibifu huo.

“Mtu atakayebainika akikata nguzo, akiiba nyaya, akichezea transfoma kiasi cha kukosesha umeme wananchi, mkuu wa wilaya wa eneo husika atalazimika kumsweka korokoroni,” alisema.

DK. Kalemani, akizungumza na wananchi wa Kijiji cha Ibindo, wilayani Kwimba, ambapo aliwasha rasmi umeme kijijini hapo akiwa katika ziara ya kikazi.

Aidha, alisema kwa wale vishoka wanaounganisha umeme kwenye nyumba za wananchi pasipo kuwa na taaluma hiyo, vilevile watakamatwa na kufunguliwa mashtaka.

“Ikitokea tumekukamata, hatutajali wewe ni kibarua wa mkandarasi anayetekeleza miradi yetu ya umeme sehemu yoyote, utakamatwa na kuwekwa ndani,” alisisitiza Waziri.

Waziri Kalemani, aliwaasa wananchi kuendelea kuwa makini kwa kujiepusha kuwatumia vishoka kwa kazi ya kufunga nyaya za umeme katika nyumba zao.

MBUNGE wa Jimbo la Sumve, Richard Ndasa akizungumza na wananchi (hawapo pichani), wakati wa ziara ya Waziri wa Nishati Dk. Kalemani katika Kijiji cha Ngulla.

Katika hatua nyingine, aliwataka wananchi kuutumia umeme ambao serikali yao imewapelekea kwa kuanzisha viwanda vidogo vya kati na hata vikubwa ili uwe na tija kwao na taifa kwa ujumla.

Naye Mbunge wa Jimbo la Sumve, Richard Ndasa, pamoja na kuishukuru Serikali kwa kuwapelekea wananchi wa jimbo lake umeme; aliwahamasisha kujitokeza kwa wingi kulipia ili waunganishiwe huduma hiyo.

“Umeme huu unapokuja unahitaji watumiaji na watumiaji ni ninyi. Gharama za kupeleka umeme ni kubwa…ni vizuri muwe mnajitokeza kwa wingi kuwasilisha maombi TANESCO ili muunganishiwe na kuanza kuutumia kuboresha maisha yenu,” alisema Kalemani.
MKUU wa wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga (kushoto), akitoa taarifa ya hali ya umeme wilayani humo kwa Waziri wa Nishati, Dk. Kalemani.

Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Kwimba, Senyi Ngaga, aliipongeza Serikali kuwapelekea wananchi umeme na kuomba vijiji vichache ambavyo havijafikiwa na huduma hiyo vipelekewe ili nao wautumie katika shughuli za kujiongezea kipato na kuboresha hali zao za maisha.

Kwa mujibu wa taarifa ya TANESCO, Wilaya ya Kwimba ina jumla ya vijiji 119 ambapo mpaka kufikia Julai 2020, vijiji 78 vitakuwa vimepatiwa umeme, sawa na ,asilimia 66 ya vijiji vyote vya wilaya hiyo.

No comments