WAZIRI MKUU AZINDUA MKAKATI WA KUDHIBITI UKIMWI.
WAZIRI Mkuu,
Kassim Majaliwa, akizindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti Ukimwi Tanzania
(2018/19 – 2022/23) katika Maadhimisho ya Siku ya Ukimwi Duniani Kitaifa,
kwenye Uwanja wa Jamhuri Jijini Dodoma, leo Desemba 1, 2018. Wapili kushoto ni
Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Bunge, Ajira, Vijana na Wenye
Ulemavu, Jenista Mhagama na kulia ni Naibu Waziri wa Afya, Maendeleo
ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Dk. Faustine Ndugulile na Mkurugenzi Mtendaji wa Tume ya Kudhibiti UKIMWI Tanzania
(TACAIDS), Dk. Leonard Maboko. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu)
Na Mwandishi Wetu, Dodoma
WAZIRI Muu Kassim
Majaliwa, amezindua Mkakati wa Nne wa Taifa wa Kudhibiti UKIMWI 2018/19 - 2022/23,
ambao unatarajia kupunguza maambukizi mapya ya VVU kwa asilimia 75 ifikapo
mwaka 2020 na asilimia 85 ifikapo mwaka 2023.
Matokeo mengine
yanayotarajiwa kufikiwa kutokana na mkakati huo ni kupungua kwa maambukizi mapya ya VVU miongoni
mwa watoto kwa chini ya asilimia 5 ifikapo mwaka 2023 na chini ya asilimia 2
ifikapo mwaka 2030.
Waziri Mkuu alizindua
mkakati huo leo Desemba 1, 2018, kwenye kilele cha maadhimisho ya siku ya
UKIMWI Duniani yaliyofanyika Kitaifa Kijini Dodoma na kusema kuwa, matayarisho
yake yamezingatia matokeo ya mapitio ya Mkakati wa Tatu wa Taifa wa Kudhibiti
UKIMWI 2013/14 – 2017/18.
Alisema mbali na matokeo
hayo pia mkakati huo utawezesha kupungua kwa vifo vinavyohusiana na
ukimwi kwa asilimia 50 ifikapo mwaka 2020 na asilimia 70
ifikapo mwaka 2023 na kupunguza unyanyapaa na ubaguzi ifikapo 2023
na kuelekea kutokomeza kabisa ifikapo mwaka 2030.
Hata hivyo, Waziri Mkuu
alisema mkakati huo umewianisha na kupanga programu mbalimbali zinazosaidia
mwitikio wa Taifa zikiwemo afua zinazotekelezwa kupitia mpango wa dharura wa
Rais wa Marekani wa uKIMWI (PEPFAR).
“Pia Mfuko wa Dunia wa
kudhibiti UKIMWI, Kifua Kikuu na Malaria (Globa Fund) na jitihada nyingine za
makubaliano ya ushirikiano baina ya nchi mbalimbali na ili kupata matokeo
mazuri tunapaswa kuimarisha mawasiliano na uratibu miongoni mwa wadau wote
sambamba na kufuata na kutekeleza vipaumbele vilivyoainishwa.”alisema.
Kadhalika, Waziri Mkuu alisema maadhimisho
hayo husaidia kubaini changamoto, mafanikio na hivyo, kuja na mikakati ya
kupambana na maambukizi ya VVU na UKIMWI. “Siku hii hutoa fursa kote Duniani kutafakari kwa mara
nyingine kuhusu tulipotoka, tulipo na tunapokwenda katika mapambano ya UKIMWI
kwenye jamii zetu.”alisisitiza Majaliwa.
WATUMISHI wa Ofisi ya Rais,
Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora wakipita kwa maandamano mbele
ya mgeni rasmi, Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa (hayupo pichani), katika kilele cha maadhimisho hayo.
Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu alizungumzia kuhusu faida za
kampeni ya FURAHA YANGU aliyoizindua mwezi Juni mwaka huu, ambapo aliagiza
mikoa yote kufanya uzinduzi wa kampeni hiyo kwenye ngazi za mikoa na hata
wilaya.
Aliema takwimu
zinaonesha kuwa wakati wa uzinduzi wa kampeni ya FURAHA YANGU katika mikoa yote
nchini jumla ya wananchi 262,114 walijitokeza kupima VVU, wakiwemo wanawake
136,389 na wanaume 125,725.
“Natoa wito kwa Mikoa na Wilaya zote kuwa kampeni
hii iwe endelevu. Viongozi katika ngazi mbalimbali tuungane kwenye uhamasishaji
wa jambo hili kwani vita dhidi ya VVU na UKIMWI inahitaji dhamira ya dhati na
tafakuri ya kina katika kujilinda dhidi ya maambukizi mapya.”alisema.
Waziri Mkuu
amewahakikishia kuwa kuwa Serikali ya Awamu ya Tano inayoongozwa na Rais Dkt.
John Magufuli itaendelea kutekeleza na kuboresha huduma za upimaji wa Virusi
Vya UKIMWI, kuzuia maambukizi ya kutoka kwa mama kwenda kwa mtoto, matibabu ya
magonjwa nyemelezi na kupiga vita unyanyapaa wa aina zote kwa WAVIU.
No comments