Breaking News

DK. MWANJELWA: TAKUKURU MSIKUBALI KUTUMIKA NA WATU WENYE NIA MBAYA KUKWAMISHA JITIHADA ZA SERIKALI.NAIBU  Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi wa TAKUKURU (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipotembelea ofisini kwao Jijini Dar es Salaam  kwa lengo la kuhimiza mapambano dhidi ya rushwa, leo Januari 9, 2019. (Picha zote na Jamas Mwanamyoto-UTUMISHI).

                                 Na Mary Mwakapenda
SERIKALI imewataka watumishi wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa Nchini (TAKUKURU) kutokubali kutumika na watu wenye nia mbaya ya kukwamisha jitihada madhubuti za Serikali. 

Imesema, TAKUKURU ni taasisi nyeti itakayoliwezesha taifa kulinda rasilimali zake na kuleta maendeleo nchini, hivyo isikubali kuikwamisha Serikali ya Awamu ya Tano  katika mapambano dhidi ya rushwa na ufisadi bali ihakikishe inatekeleza wajibu wake kikamilifu na uadilifu mkubwa.

Rai hiyo ilitolewa leo Januari 9, 2019 na  Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza na watumishi wa TAKUKURU Makao Makuu, Dar es Salaam.


NAIBU Waziri Dk. Mary Mwanjelwa, akisisitiza jambo wakati akizungumza  na Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani kabla ya kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo.


Dk. Mary, alikuwa katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya taasisi hiyo na kujionea namna inavyotekeleza wajibu wake.

Kwa mujibu wa Naibu Waziri huyo, ni kosa kubwa  na marufuku kwa mtumishi wa TAKUKURU kutumika vibaya ili kukwamisha utendaji kazi ikizingatiwa TAKUKURU ndiyo yenye dhamana ya kupambana na vitendo vya rushwa na ufisadi ili kulinda rasilimali za taifa na hatimaye kuwezesha ukuaji wa uchumi. 

Alisitiza kuwa, watumishi wa TAKUKURU wanatakiwa kuwa mfano wa kuigwa na jamii kwa kupinga, kupambana na kuzuia  vitendo vya rushwa nchini.


BAADHI  ya watumishi wa TAKUKURU Makao Makuu wakimsikiliza kwa makini Dk. Mary (hayupo pichani), wakati alipokuwa akizungumza nao.


“Mtumishi yeyote akiwa ni muumini wa rushwa hafai kuwa mtumishi wa umma katika Serikali ya Awamu ya Tano ambayo Jemedari wake Mkuu, Dk. John Magufuli, ndio mpambanaji mashuhuri wa vita dhidi ya rushwa na ufisadi.

Akitoa salamu kwa niaba ya watumishi wa TAKUKURU, Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Kamishna wa Polisi, Diwani Athumani, alimshukuru Dk. Mwanjelwa, kwa kuwahimiza kutekeleza vema jukumu lao.

Kmishna huyo alisema, ni wajibu wao kupambana na rushwa na kuahidi kuwa haitamuangusha Rais Dk.  Magufuli, katika kutekeleza jukumu kubwa na muhimu la kupambana na rushwa kwa faida ya nchi na Watanzania kwa ujumla.


NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya TAKUKURU baada ya  kuzungumza na watumishi wa taasisi hiyo.


Kwa upande wake, Naibu Mkurugenzi Mkuu wa TAKUKURU, Brigedia Jenerali, John Mbungo, alimhakikishia Dk. Mwanjelwa kuwa, itahakikisha inazingatia maelekezo yote aliyoyatoa ili rushwa itokomezwe nchini.

Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, baada ya kuzungumza na watumishi hao wa TAKUKURU, anaendelea na ziara yake ya kikazi Jijini Dar es Salaam kuzitembelea taasisi zilizo chini ya ofisi yake kwa lengo la kuhimiza uwajibikaji.

No comments