Breaking News

HOSPITALI YA MKOA WA GEITA YAPEWA SIKU 60 KUFUNGUA DUKA LA DAWA.

 WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akiangalia ramani ya majengo ya Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita wakati alipotembelea ujenzi huo juzi Januari 24, 2029. Pembeni ni msimamizi wa ujenzi huo Injinia Grace Elias. 
 
                                   NA WAMJW-GEITA

WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto  Ummy Mwalimu, ameuagiza uongozi wa Hospitali ya Mkoa wa Geita kuhakikisha wanafungua duka la dawa ili kutoa huduma karibu na wananchi na kuongeza mapato ya hospitali hiyo.

Alitoa  agizo hilo juzi Januari 24, 2019 wakati alipoitembelea hospitali hiyo ili kuona hali ya miundombinu pamoja na utoaji wa huduma za afya.

“Tumeshaagiza hospitali zote nchi nzima kuwa na maduka ya dawa katika kila hospitali husika, kwanini hapa hamjafungua duka lenu,”? alihoji Waziri Ummy.

Kutokana na kuwepo kwa hali hiyo, Waziri Ummy, alitoa miezi miwili kwa uongozi wa hospitali hiyo kufungua duka la dawa ili liweze kuwahudumia wagonjwa.

“Kuanzia sasa nawapa miezi miwili uongozi wa hospitali kuhakikisha mnafungua duka la dawa la hospitali ili liweze kuwasaidia kupandisha mapato, lakini pia kusogeza huduma karibu na wananchi,” alisema Waziri huyo.

Sambamba na hilo, Waziri Ummy, ameonekana kuridhishwa na hali ya upatikanaji wa dawa wa zaidi ya asilimia 90 na uboreshwaji wa huduma za afya zinazotolewa katika Hospitali hiyo.

Kabla ya hapo Waziri Ummy alitembelea ujenzi wa Hospitali Teule ya Mkoa wa Geita ambapo alishuhudia ujenzi huo ukiwa umekamilika kwa asilimia 54, lakini amemtaka mkandarasi anayesimamia ujenzi  huo ambaye ni wakala wa ujenzi (TBA) kufanya kazi usiku na mchana ili Hospitali hiyo ianze kufanya kazi ifikapo Mwezi Julai 2019.

Waziri Ummy alikamilisha ziara yake ya Mkoa wa Geita kwa kutembelea Hospitali ya Wilaya ya Chato ili kujiridhisha na hali ya utoaji wa huduma za afya na miundombinu pamoja na kuhakikisha kama vifaa na vifaa tiba vinapatikana Hospitalini hapo.

Waziri Ummy ameridhishwa na utolewaji wa huduma za afya lakini ameitaka Hospitali hiyo kuwa na chumba maalum chenye vifaa maalum vya uangalizi wa watoto wachanga mahututi na wale waliozaliwa kabla ya siku (watoto njiti) lengo likiwa ni kupunguza vifo vya watoto wachanga nchini.

Aidha, waziri huyo ameagiza uongozi wa hospitali hiyo kuanzisha kitengo cha huduma za wagonjwa wa dharura na wale waliopata ajali ikiwa ni agizo la serikali kwa hospitali zote za wilaya na mikoa nchi nzima.

Huo ni muendelezo wa ziara za Waziri Ummy katika mikoa ya kanda ya ziwa kutembelea Hospitali mbalimbali kuangalia hali ya miundombinu na utoaji wa huduma za afya.


WAZIRI Ummy, akiangalia mashine mpya ya X-ray ya kidigitali iliyifungwa katika Hospitali ya wilaya ya Chato wakati alipoitembelea hospitali hiyo kuona hali ya utoaji huduma za afya.
 UMYY, akimjulia hali mtoto aliyekuja kupata matibabu katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa ya Geita. Katikati ni mama wa mtoto huyo Jenista Benedicto.
 WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akiongozana na Kaimu Mkuu wa Mkoa wa Geita Josephat Maganga (kulia) wakitoka kukagua jengo la Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Geita.

No comments