Breaking News

IDARA YA KUMBUKUMBU NA NYARAKA ZA TAIFA YATAKIWA KUFUATILIA UTUNZAJI WA NAYARAKA ILI KUDHIBITI UVUJAJI WA SIRI ZA SERIKALI.KAIMU Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Firimin Msiangi (kulia), akitoa ufafanuzi kwa Dk. Mary, kuhusu mifumo ya TEHAMA inavyofanya kazi katika utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka.ji katika idara hiyo.

                       Na Mary Mwakapenda, Dodoma
IDARA ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa imetakiwa kufanya ufuatiliaji wa utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu katika taasisi zote za umma kwa lengo la kuondoa tatizo la uvujaji wa siri za serikali.

Hayo yalisemwa leo Januari 25, 2019 na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi katika ofisi hiyo Jijini Dodoma.

Ziara hiyo ina lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya idara hiyo na kujiridhisha namna idara hiyo inavyotekeleza majukumu yake ya kila siku.

Dk. Mary alisema, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ndiyo inayohusika na masuala yote ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka, hivyo inatakiwa ijiwekee utaratibu wa kufanya ufuatiliaji wa namna ya nyaraka zinavyotunzwa na kushauri namna bora ya utunzaji wa nyaraka hizo.

“Tujenge tabia ya kufanya ufuatiliaji wa miongozo tunayoitoa ili kuona kama inatekelezwa inavyotakiwa kwani tusipofanya hivyo taasisi zinafanya inavyotaka na matokeo yake ni kuvuja kwa siri za serikali,” alisisitiza Dk. Mary.

Naibu Waziri huyo alimtaka Mkurugenzi wa idara hiyo kuwa mkali na kuchukua hatua za kinidhamu kwa taasisi zote za umma zinazoshindwa kutekeleza ipasavyo jukumu la utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka na hatimaye kusababisha siri za serikali kuvuja. 

Aidha, aliipongeza idara hiyo kwa kutumia njia za kisasa za TEHAMA katika kutunza kumbukumbu na nyaraka na kuwataka kuongeza kasi ya kuzihifadhi nyaraka hizo kidigitali ili kuimarisha usalama wake.

Naye Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi, ameyataja majukumu ya idara yake kuwa ni pamoja na kuweka mifumo ya utunzaji kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma.

Pia, kutoa ushauri juu ya utunzaji bora wa kumbukumbu na nyaraka na kuratibu mipango ya kutunza na kuhifadhi kumbukumbu muhimu katika taasisi za umma, kuweka na kusimamia viwango vya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka katika taasisi za umma.

Aliyataja majukumu mengine kuwa ni kukusanya na kuhifadhi nyaraka zenye umuhimu kitaifa ili kulinda urithi andishi wa nchi yetu, kuandaa na kusimamia utekelezaji wa miongozo ya kutunza na kuteketeza kumbukumbu katika taasisi za umma.

Mengine ni kufanya tathmini ya kumbukumbu tuli (majalada yaliyofungwa) ili kutambua yale yenye umuhimu wa kudumu kwa ajili ya kuyahifadhi, kuhifadhi nyaraka kwa kutumia teknolojia ya kisasa ili kurahisisha upatikanaji na kulinda nakala halisi na kukusanya, kutunza na kuhifadhi kumbukumbu za vitu vya waasisi wa Taifa. 

Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa ilianza kutekeleza majukumu yake kama idara inayojitegemea tangu Julai, 2015 baada ya Rais wa Awamu ya Nne Jakaya Kikwete, kupitisha muundo wa Idara Februari 12  2015. 

Hata hivyo, idara hiyo ilianzia mwaka 1963 wakati Rais wa Awamu ya Kwanza, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, alipotoa Waraka Na.7 wa Mwaka 1963 ulioelekeza kutunza, kuhifadhi na kuteketeza nyaraka za Serikali.

NAIBU Waziri Dk. Mary Mwanjelwa (wapili kushoto), akishiriki kutoa nakala ya nyaraka ili kuihifadhi katika mfumo wa TEHAMA. Anayemsaidia kutoa nyaraka hizo ni Kaimu Mkurugenzi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa, Firimin Msiangi.

DK. Mary (wapili kulia), akishuhudia baadhi ya kumbukumbu na nyaraka zilizohifadhiwa katika majalada kwa ajili ya rejea ya kiofisi.
 MTUNZA Kumbukumbu Msaidizi Joyce Maro (kushoto) akitoa maelezo Dk. Mry, juu ya kumbukumbu zilizohifadhiwa katika Kituo cha Taifa cha Kumbukumbu, Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa.
 NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora  Dk. Mary Mwanjelwa (kulia), akisisitiza namna bora ya utunzaji wa kumbukumbu na nyaraka za serikali ili kuondokana na tatizo la uvujaji wa siri za serikali alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa Jijini Dodoma leo Januari 25, 2019. (Picha zote na James Mwanamyoto-UTUMISHI).
NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na watumishi wa Idara ya Kumbukumbu na Nyaraka za Taifa alipofanya ziara ya kikazi kuhimiza uwajibikaji katika idara hiyo Jijini Dodoma.

No comments