Breaking News

KATIBU MKUU WIZARA YA MIFUGO NA UVUVI AWASHTUKIZA SUMA JKT USIKU.

 
 MUONEKANO wa Jengo la Wizala ya Mifugo na Uvuvi likiendelea kujengwa usiku na mchana. (Picha zote na Edward Kondela). 
 
                                      Na. Edward Kondela
 KATIBU Mkuu Wizara ya Mifugo na Uvuvi anayeshughulikia Mifugo Prof. Elisante Gabril amefanya ziara ya kushtukiza usiku kukagua ujenzi wa jengo la wizara hiyo linalojengwa na Mkandarasi SUMA JKT katika Mji wa Serikali, Ihumwa, mkoani Dodoma.
Ziara hiyo ya kushtukiza, aliifanywa jana Januari 13, 2019 saa 5:30 usiku ili kujiridhisha kama mkandarasi huyo anafanya kazi usiku na mchana kama walivyokubalia kwa lengo la kuharakisha ujenzi kumalizika haraka.
Katibu Mkuu huyo, mara baada ya kufika katika eneo hilo alikuta ujenzi wa jengo ukiendelea kama ambavyo mkandarasi SUMA JKT alivyokubaliana na Wizara ya Mifugo na Uvuvi kujenga jengo hilo kwa saa 24.
KATIBU Mkuu wa Wizara ya Mifugo na Uvuzi anayeshugulikia mifugo Profesa. Elisante Gabriel, akishiriki ujenzi wa jengo la wizara yake jana Januari 13, 2019 saa 5.30 usiku baada ya kufanya ziara ya kushtukiza kumkagua mkandarasi SUMA JKT kama anatimiza makubaliano yao ya kujenga saa 24 jengo hilo. 
Kututokana na kutekelezwa kwa makubaliano hayo, Profesa Gabriel, alieleza kuridhishwa kwake na ujenzi unavyoendelea na kushukuru ushirikiano unaotolewa na wafanyakazi wa wizara na mkandarasi huyo.
“Tunaridhika kwa kweli kama uongozi wa wizara ikiwa ni pamoja na viongozi wetu wa kisiasa Waziri wa Mifugo na Uvuvi  Luhaga Joelson Mpina, amekuwa akitutaka kuwa tusilale tufuatilie kama kazi zinafanyika ndio maana leo hii (jana), nimeamua kuja usiku, maana unaweza kuambiwa watu wanafanya kazi usiku na mchana kumbe nikilala na kazi huku zinalala,” alisema Prof. Gabriel.
Aidha, Prof. Gabriel alimtaka mkandarasi SUMA JKT kutobweteka kwa kile alichoelezwa kuwa hadi sasa anafanya kazi nzuri katika ujenzi wa jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi na kumkumbusha aendelee kufanya kazi kwa kufuata makubaliano yaliyopo katika mkataba waliosaini kwa kujenga jengo hilo kwa ubora na kulikabidhi kwa wakati. 
 MMOJA wa mafundi kutoka SUMA JKT akifanya kazi ya kujenga jengo hilo usiku kama alivyokutwa na Katibu Mkuu Gabriel (hayupo pichani).
Katibu mkuu huyo pia, alisema hatua ya Shirika la Umeme Nchini (TANESCO) kufikisha huduma ya umeme katika eneo hilo, imesaidia kufanya kazi ya ujenzi kuwa na kasi zaidi na kupunguza gharama ya mafuta ya dizeli ambayo yalikuwa yakitumika kwenye jenereta hususan nyakati za usiku kwa ajili ya kuwashia taa na kusukumia mitambo ya ujenzi.
Prof. Gabrie pia,  aliitaja  Wizara ya Mifugo na Uvuvi kuwa ni moja ya wizara ambayo imechimba kisima chake katika eneo hilo na kutumia maji ya kisima kwa ajili ya ujenzi.
Kwa mujibu wa mkandarasi SUMA JKT, jengo la Wizara ya Mifugo na Uvuvi linatarajiwa kukamilika mwezi februari mwaka huu na kuanza kutumiwa na baadhi ya watendaji wa juu wa wizara kabla ya kujengwa jengo jingine kubwa katika eneo hilo, ambalo litatumiwa na wafanyakazi wote wa wizara waliopo mkoani Dodoma katika mwaka ujao wa fedha wa 2019/2020.

No comments