Breaking News

MAMIA YA WAOMBOLEZAJI WAJITOKEZA KUMZIKA MAMA MZAZI WA WAZIRI MKUCHIKA.WAZIRI Mkuchika, akiwaongoza wanafamilia kuwasha mishumaa juu ya kaburi la mama yake mzazi marehemu Tecla Mkuchika jana, aliyefariki Januari 2, 2019 katika Hospitali ya Misheni Ndanda, alikokuwa akipatiwa matibabu. 
                             Na James Mwanamyoto, Mtwara


VIONGOZI mbalimbali wa serikali, dini, vyama vya siasa, watumishi wa umma na wananchi wilayani Newala wamejitokeza kwa wingi kuungana na Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapteni Mstaafu. George Mkuchika,  kuomboleza kifo cha mama yake mzazi, Tecla Bernadetha Mkuchika, aliyefariki Januari 2, 2019.

Tecla, aliyefariki akiwa na umri wa miaka 93, alizikwa jana Januari 6, wilayani Newala na mamia ya waomborezaji wakiwemo viongozi mbalimbali.
 WAZIRI wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Kapten Mstaafu. George Mkuchika, akipewa pole kwa kufiwa na mama yake mzazi Tecla na  Naibu Waziri wake Dk. Mary Mwanjelwa, alipokwenda kumfariji nyumbani kwake katika Kijiji cha Nambunga wilayani Newala jana. (Picha zote na James Mwanamyoto).

Enzi za uhai wake, marehemu Tecla, alitoa mchango mkubwa kwa serikali na jamii kwa ujumla akiwa mtumishi wa umma na  hospitali zinazoendeshwa na taasisi za kidini. 

Akisoma  wasifu wa marehemu wakati wa ibada takatifu ya maziko iliyofanyika katika Kanisa la Anglikana la Msalaba Mtakatifu lililopo kijiji cha Nambunga wilayani  Newala, Msemaji wa familia, Noel Boma, alisema  marehemu alijiunga na mafunzo ya Ukunga  katika Chuo cha Kanisa Anglikana (UMCA), mwaka 1943 na baada ya kuhitimu alianza kazi St. Mary’s Hospital, wilayani Newala.

 MKUCHIKA, akipewa pole kwa kufiwa na mama yake mzazi na  Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dorothy Mwaluko, nyumbani kwake Nambunga.

Boma,  aliongeza  kuwa, marehemu Bibi Mkuchika alihamishiwa Serikalini kutokana na uchapakazi wake, weledi na uadilifu aliokuwa nao wakati akifanya kazi kwenye zahanati ya kanisa la Nambunga na Mnyambe. 

Boma aliainisha kuwa, marehemu akiwa serikalini alifanya kazi katika zahanati za Mihambwe, Mchichira, kitangari, Kilidu na Nambunga mpaka anastaafu.
 

 KUTOKA kulia Maaskofu  wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Masasi, Dk. James Almasi, Askofu Mstaafu Dk. Mwachiko Boma, Askofu Oscar Mnung’a wa Dayosisi ya Newala na Waziri Mkuchika wakiwa katika ibada ya maziko ya marehemu Tecla, mama mzazi wa waziri huyo kabla ya kumpumzisha katika nyumba yake ya milele kijijini kwao Nambunga Wilayani Newala.

Aidha, alisisitiza kuwa, marehemu Tecla, ataendelea kukumbukwa  na jamii kwa mchango wake  mkubwa alioutoa wakati akihudumu Zahanati ya Kilidu ambayo hivi sasa inatambulika kama Samora kwa kitendo cha kushiriki kikamilifu kutoa huduma usiku na mchana kwa majeruhi wa vita vya ukombozi wa Msumbiji ambavyo vilipamba moto wakati huo.

Sanjari na hayo, Boma alisema  marehemu atakumbukwa kwa sifa ya ucheshi, ukarimu na  huruma kwa wagonjwa hususani wa uzazi, sifa ambazo ziliishawishi Serikali kuendelea kumuomba mara kwa mara kuwahudumia wazazi katika Kijiji cha Nambuga licha ya kustaafu.
 BAADHI ya waombolezaji waliojitokeza kushiriki ibada ya maziko hayo.

Naye, Baba Askofu wa Kanisa la Anglikana, Dayosisi ya Masasi, Dk. James Almasi, aliwataka waombolezaji kuwalea vizuri wazee katika maeneo wanayoishi kama alivyolelewa marehemu Tecla, ikiwa ni namna bora ya kutambua na kuenzi mchango walioutoa  katika taifa. 

Dk. Almasi, amewahimiza waumini na waombolezaji,  kuhakikisha wanawatunza wazazi kwani kwa kufanya hivyo wataishi miaka mingi na yenye heri duniani kama maandiko matakatifu yanavyosema, na kuongeza kuwa asiyetunza wazee wake ni mbaya kama shetani na kamwe hawezi kupata baraka za mwenyezi Mungu ambaye ni mwingi wa rehema.

 MKUCHIKA na ndugu zake wakiweka shada la maua kwenye kaburi la mama yao mpendwa marehemu Tecla.

Kwa upande wake mjukuu wa marehemu aitwae Tecla, Mkuchika,  kwa niaba ya wajukuu wote wa marehemu bibi yao, aliwasilisha mchango wa sh. Milioni Moja kwa ajili ya kuendeleza shule ya awali ya watoto ya kanisa la Anglikana la Nambunga ikiwa ni sehemu ya kuenzi upendo aliokuwa nao marehemu kwa watoto wadogo wakiwemo wao wenyewe wajukuu.
 NAIBU Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akiweka shada la maua  kwenye kaburi la marehemu Tecla, mama mzazi wa Mkuchika. 
Ibada ya maziko ya marehemu Tecla Bernadetha, ilihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa Serikali akiwemo Katibu Mkuu Ikulu, Dk. Mosses Kasiluka, aliyemwakilisha Rais Dk. John Magufuli, Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa.

No comments