Breaking News

MWENEZI CCM IKUNGI AMMWAGIA SIFA MBUNGE AYSHAROSE *ASEMA NI MFANO WA KUIGWA.


MWENYEKITI wa Bodi ya Sekondari ya Ntuntu iliyopo wilayani Ikungi, Pius Sanka (mbele), akimuongoza Mbunge wa Viti Maalum mkoa wa Singida (CCM) Aysharose Mattembe, kukagua maeneo mbalimbali shuleni hapo wakati alipofika kukabidhi msaada wa vifaa vya ujenzi zikiwemo saruji ili kuboresha miundombinu ya shule na kuhakikisha wanafunzi wanasoma katika mazingira tulivu mwishoni mwa wiki. 
                            Na Mwandishi Wetu, Singida
KATIBU Mwenezi wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Ikungi, Pius Sanka, amepongeza jitihada kubwa zinazofanywa na Mbunge wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, katika kuhakikisha wananchi wanaondokana na kero mbalimbali.
Sanka, ambaye pia ni Mwenyekiti wa Bodi ya Shule ya Sekondari ya Ntuntu wilayani Ikungi, alisema Mbunge Aysharose, amekuwa mstari wa mbele katika kuwahudumia wananchi wa Singida bila kukoma.
SANKA, akimuonyesha Mbunge Aysharose, moja ya majengo ya madarasa ambayo ujenzi wake haujakamilika, ambapo uongozi wa shule umekuwa kwenye harakati za kuhakikisha yanakamilika.

Alisema Aysharose, ni mfano wa kuigwa kwa wabunge wengine wa CCM kwa kuwa, amekuwa mstari wa mbele kutumia kipato chake kidogo anachopata kwa kuwaletea maendeleo wananchi na kwamba, Chama kitaendelea kuwa naye bega kwa bega.
Akizungumza mwishoni mwa wiki, kwenuye hafla ya kukabidhi vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji vilivyotolewa na mbunge huyo, kwa ajili ya kuboresha mazingira shuleni hapo, Sanka alisema: “Wabunge wa aina yako ndio hasa CCM inawataka, kazi yako unayofanya iko wazi na wenye macho wanaona kwa sababu kila siku unakwenda kwa wananchi kusikiliza na kutatua kero ukiwa na msaada mkononi.
MBUNGE Aysharose, akishiriki na viongozi wengine kukagua ujenzi wa shule uliokuwa ukiendelea shuleni hapo ambapo na kujionea hali halisi ya mahitaji yake.

“Huu ni mwisho wa mwaka, lakini hujachagua kupumzika na kufurahia maisha, umeamua kuzunguka kwa wananchi wako na kwenye shule mbalimbali kukabidhi saruji na mabati ili shule zikifunguliwa watoto wetu wakute mazingira salama.
“Ulikuja hapa kukagua maendeleo na Ilani ya CCM na ukakutana na changamoto ya uhaba wa vyumba vya madarasa, choo na uchakavu wa miundombinu na sasa umerudi na vifaa vya ujenzi ile wanafunzi wetu wasome kwa utulivu,” alisema.
WANAFUNZI na viongozi wengine wakishuhudia mbele ya Mbunge wao Aysharose, aliyetoa  msaada wa saruji kwa ajili ya kuboresha shule yao ili wasome katika mazingira mazuri na tulivu.

Alisema jitihada zinazofanywa na mbunge huyo ni nzuri kwakuwa zinaunga mkono mikakati na jitihada mbalimbali zinazofanywa na Rais Dk. John Magufuli, na kuongeza kuwa, ofisi yake itaendelea kukuunga mkono katika harakati zake zote za kuwaletea wananchi maendeleo.
Kwa upande wake, Mbunge Aysharose, alisema kuwa aliomba kazi ya kuwatumikia wananchi hivyo, jukumu lake ni kuendelea kufanya kazi kwa bidi.
MBUNGE Aysharose, akiwa na viongozi wa shule hiyo wakiongozwa na Sanka wakati wa makabidhiano ya saruji kwa ajili ya kusaidia kuboresha miundombinu shuleni hapo.


Alisema Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk. Magufuli, imedhamiria kuibadili Tanzania na kuwafanya wananchi kuishi kwenye mazingira salama na tulivu, ambapo ukiacha elimu pia sekta zingine amekuwa akizipa kipaumbele kikubwa.
“Ndugu zangu, nimeomba kazi, mkanipa kazi. Hivyo, sioni shida kuchapa kazi kwa kushirikiana nanyi katika kutatua kero mbalimbali zinazotukabili katika mkoa wetu.
AYSHAROSE, akikagua miundombinu ya shuleni hapo. Wengine katika picha ni viongozi wa CCM na shule hiyo. 
“Rais wetu alishasema ‘Hapa Kazi Tu’. Hivyo, ni lazima nimuunge mkono katika kubadili maisha ya Watanzania. Waajiri wangu ni wananchi wa Singida hivyo, sina sababu ya kupumzika kwa sababu CCM inafanya kazi saa 24 ndani ya mwaka,” alisema Aysharose.
Alisema hatua yake ya kusaidia vifaa vya ujenzi ikiwemo saruji na mabati ambapo shule zaidi ya 10 zitanufaika, ni mwendelezo wa kuunga mkono juhudi za serikali ya Awamu ya Tano chini ya Rais Dk. John Magufuli, ambayo imedhamiria kuinua elimu nchini.

No comments