Breaking News

...NANI KAMA RAIS MAGUFULI? * AAGIZA KUSITISHWA MARA MOJA KWA ZOEZI LA KUVIONDOA VIJIJI NA VITONGOJI VINAVYODAIWA KUWEPO KATIKA MAENEO YA HIFADHI *WANANCHI WAMFAGILIA KWA UAMUZI WAKE. RAIS Dk. John Magufuli, akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Doroth Mwanyika  (hawapo pichani) kuhusu kusitisha zoezi la kuwaondoa wananchi wanaoishi katika vijiji na vitongoji vilivyopo katika maeneo ya Hifadhi. Ikulu Jijini Dar es salaam leo Januari 15, 2019. (Picha zote na Ikulu).

                                   Na Thomas Mtinge

NANI kama Rais Dk. John Magufuli?. Ndivyo unavyoweza kusema baada ya Rais huyo kuagiza kusitishwa mara moja kwa zoezi la kuviondoa vijiji na vitongoji vinavyodaiwa kuwepo katika maeneo ya hifadhi na amewataka viongozi wa wizara zote zinazohusika kukutana ili kubainisha na kuanza mchakato wa kurasimisha maeneo ya vijiji na vitongoji hivyo.

Agizo hilo la Rais Magufuli, limekuja huku kukiwa na malalamiko mengi kutoka kwa wananchi hao, wakidai kuvamiwa, kubomolewa na kuchomwa moto makazi yao na maofisa wa hifadhi kwa kushirikiana na  wa wilaya husika kutokana na kufanya Oparesheni za kuwaondoa katika maeneo hayo.
Rais Maguful,i alitoa agizo hilo leo Januari 15, 2019 Ikulu Jijini Dar es Salaam alipokutana na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk. Hamis Kigwangallah, Katibu Mkuu Kiongozi. Balozi John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi, Abdallah Ulega, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mhandisi Joseph Nyamhanga na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Dorothy Mwanyika. 

Pamoja na agizo hilo, Rais Magufuli ametaka viongozi wa wizara husika kubainisha maeneo ya hifadhi za wanyamapori na misitu ambayo hayana wanyamapori ama misitu ili yagawiwe kwa wafugaji na wakulima ambao kwa sasa wanataabika kupata maeneo ya kufugia wanyama na kuzalisha mazao.
Pia, Dk. Magufuli ameitaka Wizara ya Maliasili na Utalii kuangalia upya zoezi la uwekaji wa mipaka ya hifadhi na makazi, na kutumia busara katika uwekaji wa mawe ya mipaka hiyo ili kutowaondoa wananchi katika maeneo ambayo hayana ulazima wa kuwaondoa. 

“Mimi sifurahii kuona wafugaji kila mahali wanafukuzwa, kama kuna eneo ambalo tunafikiri lilikuwa hifadhi ya wanyama lakini halitumiki, tutabadilisha sheria, tunalimega na tunaligawa kwa wafugaji, vivyo hivyo hata kwa wakulima kama kuna eneo tunaona ni hifadhi lakini halina msitu wala wanyamapori, na lina rutuba, na wakulima wanataka kulima nalo tunalimega tunawapa wakulima.

“Baadaye tutajua kabisa eneo hili ni la hifadhi, hili ni la mifugo, hili ni la wakulima, hili ni la makazi. Kwa hiyo nyinyi Mawaziri na Makatibu Wakuu mkakae mkatangulize maslahi ya hawa tunaowaongoza ambao ni wakulima, wafugaji, wavuvi nakadhalika, lakini pia tunahitaji wanyamapori, sijasema sasa hifadhi zote za wanyama tunazimaliza, hapana, hifadhi za wanyama lazima tuzihifadhi,” alisisitiza Rais Magufuli.

RAIS Dk. John Magufuli, akizungumza na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Doroth Mwanyika  kuhusu kusitisha zoezi la kuwaondoa wananchi wanaoishi katika vijiji na vitongoji vilivyopo katika maeneo ya Hifadhi. Ikulu Jijini Dar es salaam leo Januari 15, 2019.

Magufuli, aliagiza vijiji vyote 366 vilivyoainishwa kuwepo ndani ya maeneo ya hifadhi hapa nchini, visiondolewe katika maeneo hayo na badala yake ametoa mwezi mmoja kwa viongozi wa wizara zote zinazohusika kubainisha maeneo ya vijiji hivyo na kuanzisha mchakato wa mabadiliko ya sheria ili yawasilishwe katika kikao kijacho cha Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Alifafanua kuwa, ni lazima Serikali ifanye maamuzi hayo sasa kwa kuwa idadi ya Watanzania imeongezeka hadi kufikia Milioni 55, idadi ya mifugo imeongeza hadi kufikia Milioni 35 na hivyo kuna ongezeko kubwa la mahitaji ya maeneo ya ardhi ikilinganishwa na wakati nchi inapata uhuru ambapo Watanzania walikuwa Milioni 9 na mifugo ilikuwa Milioni 10.

Aidha, aliagiza sheria ya vyanzo vya maji pia iangaliwe upya ili kutowazuia Watanzania wanaozalisha mazao kandokando mwa mito na ameelezea kutofurahishwa kwake na vitendo vya kufyeka mazao ya wakulima kwa madai kuwa wamelima ndani ya mita 60.

Halikadhalika, Magufuli ameipongeza Wizara ya Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi kwa kuwasilisha kwake mapendekezo ya kufutwa kwa mashamba ambayo hayajaendelezwa na ameagiza wizara hiyo iendelee kumpelekea mapendekezo ya mashamba yote yaliyotelekezwa ili ayafute na wananchi wagawiwe kwa ajili ya kuyatumia kwa uzalishaji wa mazao na mifugo.

Dk. Magufuli akifurahi jambo na Waziri wa Maliasili na Utalii Dk.Hamis Kigwangala, Katibu Mkuu Kiongozi Balozi Dk. John Kijazi, Naibu Waziri wa Mifugo na Uvuvi Abdallah Ulega, Katibu Mkuu TAMISEMI Mhandisi Joseph Nyamuhanga pamoja na Katibu Mkuu Wizara ya Ardhi Doroth Mwanyika  mara baada ya kumaliza mazungumzo na viongozi hao.

Hata hivyo, Magufuli alisema maagizo hayo hayana maana kuwa sasa wananchi waruhusiwe kuvamia maeneo ya hifadhi, na ametaka zoezi la uwekaji wa mipaka lifanyike haraka na kwa uwazi.

Agizo hilo la Magufuli, limepongezwa na wananchi wengi hususan waliojenga karibu na maeneo hayo wakisema kuwa limekuja wakati muafaka.

“Sijui tumfananishe na nani Rais wetu. Anafanya vitu vya kihistoria sana kama ilivyokuwa kwa Mitume…Mambo kama haya tuliyaona enzi za Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Nyerere.

Katika kipindi cha uhai wake, Nyerere kamwe hakutaka kuona  ama mwanananchi akiionea serikali au serikali kuwaonea wananchi,” alisema mwananchi mmoja kutoka mkoani Morogoro ambaye hakutaka jina lake lichapishwe.

Alisema migogoro baina ya viongozi wa mbuga za hifadh, wakulima na wafugaji imeleta shida sana katika kipindi kirefu bila kupatiwa ufumbuzi wa kudumu.

Kwa mujibu wa mwananchi huyo, hali hiyo ilisababisha wakulima na wafugaji kupoteza mali na makazi yao na hivyo kukata tama na maisha.

Mwananchi huyo alitoa mfano wa hivi karibuni ambapo viongozi wa hifadhi hiyo kwa kushirikiana na viongozi wa wilaya ya Mvomero mkoani Morogoro walivamia, kuharibu kwa kuchoma moto makazi ya wananchi waliodaiwa kuishi ndani ya hifadhi ya wanyamapori.
RAIS Magufuli, akiwa katika picha ya pamoja na viongozi hao baada ya kumalizika kwa kikao chao.
“Niseme tu Rais wetu si wa kawaida kwani ni mtu ambaye anaona mbali sana. Naamini kila siku hakuna jambo linalotendeka katika nchi yake bila kulifuatilia kwa karibu. Hatuna cha kumpa zaidi ya shukrani na tunaahidi kumpa ushirikiano kwa kuheshimu agizo lake,” alisema.

Alisema huu ni huu wakati muafaka kwa viongozi waliopewa madaraka na Magufuli,  kujitafakari na kutambua Rais wao anataka nini na si kujiamulia mambo yanayokwenda kinyume ambayo mwenyewe  IMagufuli) hayapendi.

1 comment:

  1. Piga picha kwa kulaza simu,wanaone ana warefuu sura Ina Inapotea

    ReplyDelete