Breaking News

WAZIRI MKUU AAGIZA KUKAMILISHWA KWA KANUNI ZA MASOKO YA MADINI

*Ataka maagizo ya Rais kuhusu masoko ya madini yatekelezwe haraka
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, akisalimiana na Waziri wa Madini Dotto Biteko, wakati akiwasili kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma jana Januari 26, 2019, kufungua mkutano wa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa Tanzania Bara.
----------------------------
Na Khadija Mussa, Dodoma
WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa, ameuagiza uongozi wa Wizara ya Madini uhakikishe kanuni za uendeshaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini zinakamilika na kuanza kutumika kwa wakati ili kuongeza tija kwenye sekta hiyo.

Kauli hiyo ya Majaliwa, imekuja siku chache baada ya hivi karibuni, akizungumzia kuhusu changamoto ya kukabiliana na utoroshwaji wa madini nchini, Rais Dk. John Magufuli, aliagiza kuanzishwa kwa masoko ya madini kwenye mikoa yote.

Kutokana na agizo hilo, Waziri Mkuu aliitaka Wizara ya Madini na wakuu wote wa mikoa watekeleze agizo hilo la  haraka iwezekanavyo.

Majaliwa, alieyasema hayo jana Januari 26, 2019 wakati akifungua mkutano kuhusu uanzishwaji wa masoko ya madini katika mikoa yote nchini.

Mkutano huo wa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa, ulifanyika kwenye ukumbi wa Kambarage, Wizara ya Fedha na Mipango Jijini Dodoma na kuhudhuriwa na  mawaziri, manaibu waziri, makatibu wakuu na manaibu makatibu wakuu, watendaji wa Wizara ya Madini pamoja na wa Tume ya Madini.

Waziri Mkuu alisema katika kuanzishwa kwa masoko hayo, rasimu ya kanuni imeandaliwa na hivyo ni vema wakazielewa vizuri kwa sababu wao ndiyo watakaozitekeleza kwenye maeneo yao ili Serikali iweze kufikia lengo ililojiwekea katika kuimarisha sekta ya madini.

”Kutokana na umuhimu wa masoko hayo naagiza kanuni hizo zikamilishwe haraka iwezekanavyo ili kuwasaidia watu wetu kupata masoko ya uhakika ya madini na Serikali itanufaika na mrabaha na tozo mbalimbali zitakazokuwa zikitozwa kwa mujibu wa sheria,” alisema.

Kadhalika, Waziri Mkuu aliagiza pindi kanuni hizo zitakapokamilika, Wizara ya Madini ihakikishe zinafikishwa kwa wakurugenzi wa majiji, manispaa na halmashauri za wilaya, maeneo ya machimbo, wachimbaji na wafanyabiashara wa madini ili kuondoa migogoro.

Hata hivyo, Waziri Mkuu aliongeza kuwa OR-TAMISEMI kupitia wakuu wa mikoa na maofisa tawala wa mikoa wakishirikiana na Wizara na Tume ya Madini waandae taratibu zitakazowezesha Wakurugenzi wa halmashauri kutoa maoni katika kuanzisha masoko.

Katika hatua nyingine, Waziri Mkuu aliwataka wakuu wa mikoa wakasimamie kikamilifu masuala ya ulinzi na usalama kwenye masoko hayo ili kuwahakikishia wafanyabiashara, wachimbaji na wananchi usalama wa kutosha wakati wa kuuza madini hayo.

Alisema kwa muda mrefu Rais Dk. Magufuli, amekuwa akisisitiza kuhusu sekta ya madini kuchangia ipasavyo katika pato la Taifa na hivyo kuleta maendeleo ya kiuchumi na kijami kwa wananchi, lakini sekta hiyo imekuwa na matatizo ikiwemo utoroshwaji wa madini na migogoro kwa wachimbaji hususani wachimbaji wadogo.

”Jitihada mbalimbali zimekuwa zikichukuliwa kuhakikisha changamoto hizo zinaondolewa kwa lengo la kuongeza tija kwenye sekta ya madini..apenda mfahamu kuwa mna nafasi muhimu katika kuifanya sekta hii iweze kuleta manufaa yanayotarajiwa kwa Taifa,” alisema Majaliwa.

Kwa upande wake, Waziri wa Madini, Doto Biteko alisema mkutano muhimu kwa sababu linalenga kumaliza changamoto ya masoko ya madini nchini, hivyo amewataka wakuu wa mikoa wahakikisha walipa kipaumbele jambo hilo kwa kuwa linamanufaa kwa Taifa.

Alisema kwa sasa wachimbaji na wafanyabiashara wa madini hawana maeneo maalum wanayoweza kufanyia biashara  ya madini  hali ambayo inachangia kuwepo kwa utoroshwaji wa madini, jambo ambalo linasababisha Serikali kukosa mapato.

Waziri Biteko ameongeza kuwa ili  kukabiliana na changamoto ya masoko ya madini, Wizara iliunda kamati iliyojumuisha wajumbe kutoka katika taasisi mbalimbali za Serikali zikiwemo Ofisi ya Rais Ikulu, Ofisi ya Rais TAMISEMI, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Wizara ya Madini, Wizara ya Fedha na Mipango, Wizara ya Viwanda na Biashara, Benki  Kuu na Tume ya Madini. 

Alisema kamati hiyo iliundwa ili kuandaa rasimu ya Kanuni za kuanzisha na kusimamia Masoko ya Madini Nchini. “Katika kuandaa kanuni hizo, jina la kanuni linapondekezwa liwe The Mining (Mineral and Gem House) Regulations, 2019," aliesema Waziri Biteko.
 WAZIRI Mkuu akisalimiana na Mkuu (kushoto), wa Mkoa wa Dodoma Binilith Mahenge, wakati akiwasili kwenye mkutano wa wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa Tanzania Bara, katika ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma jana Januari 26, 2019. Katikati ni Waziri wa Madini, Dotto Biteko.
 WAKUU wa mikoa wakimsikiliza Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, wakati akiwahutubia kwenye ukumbi wa Hazina Jijini Dodoma.
BAADHI ya washiriki wa kikao hicho wakimsikiliza Majaliwa.
MAJALIWA akiwahutubia wakuu wa mikoa na makatibu tawala wa mikoa Tanzania Bara.
 WAZIRI Mkuu Kassim Majaliwa (kushoto), akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Njombe Christopher Ole Sendeka, mara baada ya kufungua mkutano huo. Katikati ni Waziri Dotto Biteko.
NAIBU Waziri wa Maliasili na Utalii Constantine Kanyasu (kulia), akimsikiliza  Waziri Mkuu Kassim Majaliwa, katika ukumbi huo. Kutoka kushoto ni Wakuu wa Mkoa ya Iringa Ally Hapi na Njombe Christopher Ole Sendeka.
MAJALIWA (kushoto) akimsikiliza Mkuu wa Mkoa wa Mara Adam Malima, mara baada ya kufungua mkutano huo. (Picha zote na Ofisi ya Waziri Mkuu).

No comments