Breaking News

QUEEN MLOZIAMPA MZUKA MPYA MATTEMBE

Mbunge wa Viti maalum mkoa wa Singida Aysharose 
Mattembe akizungumza wakati wa ziara ya Queen Mlozi
Wilayani Manyoni.
Wanawake Na Mwandishi wetu
MBUNGE wa Viti Maalumu Mkoa wa Singida, Aysharose Mattembe, amesema kuwa amepata mzuka mpya wa kuongeza kasi ya kuwatumikia wanawake na wananchi wa mkoa wa Singida kutokana na ujio wa Katibu Mkuu wa UWT, Queen Mlozi.
Hivi karibuni Mlozi alifanya ziara ya kikazi mkoani Singida, ambapo alitembelea Wilaya za Manyoni, Itigi, Ikungi na Singida Mjini ambako alikagua shughuli za uzalishaji mali pamoja na kuzungumza na wanawake.
Pia, alikagua miradi ya maendeleo inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Tano chini ya Dk John Magufuli, ambayo imedhamira kuhakikisha Watanzania wanaondokana na kero kwenye sekta mbalimbali ikiwemo elimu, afya, maji na miundombinu.
Kupitia ziara hiyo ya Katibu Mkuu huyo wa UWT, Mattembe akasema kuwa amejifunza mambo mengi ikiwemo utendaji kazi wa wazi na shirikishi na umakini wa kiongozi huyo katika kutekeleza majukumu yake.
Akizungumza na waandishi wa habari kwenye ziara hiyo, Mattembe alisema kuwa atahakikisha kasi yake ya kuwaletea maendeleo wananchi wa Singida hususan wanawake na vijana itaendelea kwa nguvu ili kuendelea kuunga mkono jitihada za serikali.
Pia, ameupongeza uongozi wa UWT Taifa kwa kazi kubwa ya kuleta mageuzi ndani ya Jumuiya hiyo na kueleza kwamba, ndani ya kipindi kifupi UWT imeongeza ufanisi na kuifanya kuwa kimbilio la wanawake wote nchini bila kujali vyama.
Amesema chini ya uongozi wa Mwenyekiti wa UWT Taifa, Mama Gaudentia Kabaka na Mlozi na Baraza la Utekelezaji UWT imekuwa msaada mkubwa na kiunganishi kwa wanawake nchini.
Pia, amesema mabosi wake hao wamekuwa mstari wa mbele kuhamasisha ushirikiano miongoni mwa wanawake na kuelekeza wanawake fursa za kiuchumi zinazotolewa na serikali ili kuhakikisha mwanamke anazidi kukua na kushiriki kikamilifu kwenye ujenzi wa Tanzania Mpya.
“Nimefurahi na kufarijika sana na ziara ya bosi wangu (Katibu Mkuu), hakika huyu mama ni jembe na ana mambo mengi sana ya kujifunza kama unataka kupiga hatua. Yuko makini, mcheshi na mwenye hekima na anafanya kazi zake kwa vitendo. Hakika Mungu ametupa kiongozi mwenye maoni na kama unavyoona ndani ya kipindi kifupi cha uongozi wao katika UWT, mageuzi makubwa yamefanyika.
“Kwangu nimejifunza na siku chache nilizokuwa naye tukifanya kazi pamoja ziarani kumenipa mwelekeo mpya na nguvu ya kuwatumikia wananchi wangu. Namshukuru sana na ninamkaribisha tena Singida kwani, wanawake wamefurahi sana kwa sababu tunampenda kiongozi wetu,” alisema Mattembe.

No comments