Breaking News

RAIS DK. MAGUFULI AFANYA MABADILIKO MADOGO BARAZA LA MAWAZIRI, ATEUA VIONGOZI WAPYA KADHAA.


KATIBU Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi akitangaza mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri pamoja na uteuzi wa viongozi wapya kadhaa uliofanywa na Rais Dk. John Magufuli, leo Januari 8, 2019, Ikulu Jijini, Dar es Salaam.


                                      Na Thomas Mtinge

RAIS Dk. John Magufuli,  amefanya mabadiliko madogo katika Baraza la Mawaziri na kufanya uteuzi wa viongozi mbalimbali wa wizara na taasisi za Serikali.

Mabadiliko ya Baraza na uteuzi wa viongozi hao uliotangazwa leo Januari 8, 2019 na Katibu Mkuu Kiongozi,  Balozi John Kijazi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Katika mabadiliko hayo, Magufuli amemteua aliyekuwa Waziri wa Madini Anjellah Kairuki kuwa Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu anayeshughulikia Uwekezaji.


Uteuzi huo  wa waziri anayeshughulikia masuala ya uwekezaji, una lengo la kuongeza msukumo na kuimarisha usimamizi wa masuala ya uwekezaji hasa baada ya kuamua Kituo cha Uwekezaji Tanzania (TIC) kihamishiwe Ofisi ya Waziri Mkuu.

Aidha, Rais Magufuli amemteua Doto Biteko kuwa Waziri wa Madini. Kabla ya uteuzi huo,  Biteko alikuwa Naibu Waziri wa wizara hiyo.

Kufuatia uteuzi huo, Wizara ya Madini sasa itakuwa na Naibu Waziri mmoja ambapo Stanslaus Nyongo anaendelea na wadhifa wake.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amemteua Mhandisi Joseph Nyamuhanga kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI).

Kabla ya uteuzi huo Mhandisi Nyamuhanga alikuwa Katibu Mkuu Ujenzi, na anachukua nafasi ya Mhandisi Mussa Iyombe ambaye amestaafu.

Pia, Magufuli amemteua Dk. Zainabu Chaula kuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (anayeshughulikia afya). Kabla ya Uteuzi huo Dk. Chaula alikuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (afya).

Katika hatua nyingine, Arch. Elius Mwakalinga ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu Ujenzi. Kabla ya uteuzi huo Mwakalinga alikuwa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Majengo Tanzania (TBA) na anachukua nafasi ya Mhandisi Nyamuhanga ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu TAMISEMI.

Naye, Dorothy Mwaluko ameteuliwa kuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera na Uwekezaji). Kabla ya Uteuzi huo, Dorothy alikuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Wakati huo huo, Dk. Dorothy Gwajima ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu TAMISEMI (Afya). Kabla ya uteuzi huo Dk. Dorothy alikuwa Mkurugenzi wa Tiba wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto.

Kwa mujibu wa Katibu Mkuu Kiongozi, Balozi John Kijazi, Dk. Francis K. Michael ameteuliwa kuwa Naibu Katibu Mkuu, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora.

Kabla ya uteuzi huo Dk. Francis K. Michael alikuwa Mhandiri wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam (UDSM).

Balozi Kijazi alisema, Rais Magufuli amemteua Dk. Mpoki Ulisubisya kuwa Balozi.

Kabla ya uteuzi huo Dk. Ulisubisya alikuwa Katibu Mkuu wa Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto (akishughulikia afya).

Imeelezwa kuwa, kituo cha kazi cha Dk. Ulisubisya kitatangazwa baadaye.

Rais Magufuli pia, amemteua Prof. Faustin Kamuzora kuwa Katibu Tawala wa Mkoa wa Kagera.

Kabla ya Uteuzi huo Prof. Kamuzora alikuwa Katibu Mkuu, Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu na anachukua nafasi iliyoachwa wazi na  Athumani Diwani Msuya ambaye ameteuliwa kuwa Mkurugenzi Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU).

Uapisho wa viongozi hao utafanyika kesho  Januari 9, 2019 saa 3:30 asubuhi, Ikulu Jijini Dar es Salaam.

Aidha,  Rais Magufuli ameifuta nafasi ya Naibu Katibu Mkuu wa Wizara ya Ulinzi. Nafasi hiyo ilikuwa inashikiliwa na Immaculate Ngwalle ambaye amestaafu.

Katika hatua nyingine, Rais Magufuli amefanya uamuzi wa kufungua Ubalozi Mpya wa Tanzania nchini Cuba. Balozi wa Tanzania nchini Cuba atateuliwa baadaye.

No comments