SERIKALI YAPIGA MARUFUKU WAAJIRI KUHAMISHA MTUMISHI AKIWA NA KESI KAZINI *WATAKAOSHINDWA KUWASILISHA VIELELEZO VYA RUFAA ZILIZOKATWA NA WATUMISHI WA UMMA KUKIONA.
Na Mary Mwakapeda
WAJIRI na Mamlaka za Ajira Nchini watakaoshindwa kuwasilisha vielelezo vya
rufaa zilizokatwa na watumishi wa umma
kwenye Tume ya Utumishi wa Umma ndani ya siku 14 kama sheria
inavyoelekeza, watachukuliwa hatua za kinidhamu kwa kuikwamisha tume hiyo kutekeleza
jukumu lake la kushughulikia kwa wakati rufaa hizo.
Kauli hiyo imetolewa jana Januari 16, 2019 Jijini Dar es Salaam na Naibu
Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk.
Mary Mwanjelwa.
Naibu Waziri Mary, alikuwa akizungumza na watumishi wa Tume ya Utumishi wa
Umma Makao Makuu ya Tume hiyo, akiwa
katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa
kina majukumu ya Tume na kujiridhisha namna Tume hiyo inavyotekeleza majukumu yake.
KAIMU Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo, akieleza majukumu
ya Tume ya Utumishi wa Umma kwa Naibu Waziri Dk. Mary.
Alisema, kitendo cha waajiri hao kutowasilisha vielelezo vinavyohitajika na
Tume ya Utumishi wa Umma kwa wakati ili kuiwezesha tume kufanya maamuzi sahihi
ya rufaa, imekuwa ni kikwazo cha
utekelezaji wa majukumu yake kama vile kusimamia, kufuatilia na kutathmini
uzingatiaji wa Sheria, Kanuni na taratibu zinazosimamia Utumishi wa Umma Nchini.
Dk. Mary, alisisitiza kuwa Menejimenti ya Tume ya Utumishi wa Umma kuhakikisha inatoa elimu kwa umma kuhusu
utaratibu wa kufanyia kazi rufaa zinazowasilishwa ili waweze kujua ni muda gani
unaotumika kushughulikia rufaa zao, na kuongeza kuwa elimu hiyo itapunguza
malalamiko dhidi ya tume kuwa haifanyii kazi rufaa zao kwa wakati.
Aidha, alisema kuwa, kuanzia sasa ni marufuku kwa mwajiri yeyote kumhamisha
mtumishi aliyebainika kuwa na kosa
mahala pa kazi kwasababu Tume ya Utumishi wa Umma itashidwa
kushughulikia suala la mtumishi huyo na kuna uwezekano mkubwa akafanya tena
makosa yale yale anakohamia.
BAADHI watumishi wa Tume ya Utumishi wa Umma wakimsikiliza Naibu Waziri
Mary (hayupo pichani).
Kwa upande wake, Kaimu Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma, Richard Odongo alisema
kuwa, majukumu ya Tume ya Utumishi wa Umma yameainishwa katika Sheria ya
Utumishi wa Umma Sura 298 Kifungu 10 (1)
ambapo imepewa mamlaka ya kutoa miongozo na kuhakikisha Utumishi wa Umma katika
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania unaendeshwa kwa mujibu wa Sheria, Kanuni na
Taratibu.
Odongo alisema, Tume ya Utumishi wa Umma ni Mamlaka ya Rufaa kwani inapokea
na kushughulikia rufaa za watumishi wa umma, hivyo inafanya kazi kama mahakama
ndani ya Utumishi wa Umma na ni chombo cha kutoa haki kwa watumishi wanaoonewa
na inasimama kama mdhamini kuhakikisha haki inatendeka pande zote yaani kwa
mwajiri na mtumishi.
Naye, Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dkt. Steven
Bwana, amemshukuru Dkt. Mwanjelwa kwa maelekezo ya kuboresha utendaji kazi
aliyoyatoa na kuahidi kusimamia utekelezaji wake.
MWENYEKITI wa Tume ya Utumishi wa Umma, Jaji Mstaafu, Dk. Steven Bwana,
akifafanua majukumu ya bodi yake.
Tume ya Utumishi wa Umma iliundwa kwa Mujibu wa Sera ya Menejimenti na Ajira
katika Utumishi wa Umma ya Mwaka 2008 ili kuhakikisha kuwa, Utumishi wa Umma
unakuwa mmoja na watumishi wote wanakuwa na taratibu za usimamizi, hadhi, haki
na masilahi yanayofanana.
No comments