Breaking News

SERIKALI YATOA BILIONI 2.5 KWA AJILI YA UJENZI WA JENGO LA MAMA NA MTOTO HOSPITALI YA RUFAA YA MKOA WA SHINYANGA.WAZIRI  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akzungumza wagonjwa katika Kituo cha Afya cha Kambarage mjini Shinyanga jana Januari 24, 2019.

                               
                               NA WAMJW-SHINYANGA

SESRIKALI kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto imetoa kiasi cha sh. Bilioni 2.5 zitakazotumika katika ujenzi  wa jengo la mama na mtoto katika Hospitali ya rufaa ya Mkoa wa Shinyanga, lengo likiwa ni kutoa huduma za kibingwa kwa akina mama wajawazito na watoto wachanga.

Hayo yalisemwa jana Januari 24, 2019 na Waziri wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, wakati alipotembelea ujenzi wa Hospitali hiyo na kukuta jengo la wagonjwa wa nje (OPD) na Utawala likiwa limekamilika.

Waziri Ummy, alisema fedha hizo zitafika katika hospitali hiyo ndani ya wiki mbili ili ziweze kuchochea kasi ya ujenzi na lengo  ifikapo mwezi Septemba 2019 ianze kutoa huduma za afya.

“Ninaahidi kutoa sh. Bilioni 2.5 ndani ya wiki mbili ziweze kutumika katika ujenzi wa jengo la mama na mtoto, lengo la serikali ni kuhakikisha kila mama mjamzito anapofika hospitalini kujifungua atoke akiwa salama yeye na kichanga chake,” alisema Waziri Ummy.

Waziri Ummy, amefikia uamuzi huo baada ya kupokea ripoti ya mkoa kuhusu vifo vitokanavyo na uzazi kutoka kwa Mganga Mkuu wa Mkoa Dk. Mfaume Rashid, ambapo kwa mwaka 2016/2017 kulikua na vifo 73, na mwaka 2017/2018 vikiwa ni vifo 56, hali ambayo Waziri huyo ameonekana kutoridhishwa nayo.

Hata hivyo, Waziri Ummy aliahidi kuongeza fedha zingine kiasi cha shilingi bilioni 3 ndani ya mwezi mmoja, zitakazotumika katika ujenzi wa jengo kwa ajili ya huduma za uchunguzi ikiwemo huduma za maabara, X-ray na CT-Scan pia jengo hilo litakua na vyumba vitatu vya upasuaji.

Waziri Ummy, alisisitiza ujenzi wa jengo hilo utumike wa  mfumo wa Force Account ambao utahakikisha wananchi wanashiriki kwa asilimia 100 katika kufanikisha ujenzi huo na huduma za afya zianze kutolewa mapema.

Wakati huo huo, Waziri Ummy, ametembelea kituo cha afya cha Kambarage katika Manispaa ya  Shinyanga kuona hali ya miundombinu ya kituo hicho na utoaji wa huduma za afya huku kwa kiasi kikubwa akionekana kuridhishwa na kasi ya ujenzi wa majengo ya huduma mbalimbali. 

Kuhusu uhaba wa watumishi wa kada za afya waziri huyo ameahidi kutatua changamoto hiyo hali inayopelekea kuwepo kwa msongamano wa wagonjwa.

Waziri Ummy amehitimisha ziara yake katika mikoa ya kanda ya ziwa kwa kutembelea Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga na kuridhishwa kwa kiasi kikubwa na hali ya utoaji wa huduma za afya hasa katika jengo la huduma za mama na mtoto na pia katika jengo la kuhifadhia watoto wachanga wenye uhitaji wa uangalizi maalumu (NICU).


UMMY,  akipanda mti wa kumbukumbu katika kituo cha Afya cha Kambarage kilichopo katika Manispaa ya  Shinyanga.
 


WAZIRI wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akikagua jengo la wagonjwa wa nje (OPD) ambalo limekamilika  katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Kushoto ni Mkuu wa Wilaya ya Shinyanga  Jasinta Mboneka na kulia ni Katibu Tawala wa Mkoa huo  Albert Msosela.
 


WAZIRI  wa Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto Ummy Mwalimu, akimjulia hali mtoto mchanga aliyezaliwa katika Kituo cha Afya cha Kambarage mjini Shinyanga.


WAZIRI Ummy, akioneshwa ramani ya majengo ya Kituo cha Afya cha Kambarage na Mganga Mkuu wa Wilaya Dk. Lusajo Mwakajoko, wakati alipotembelea kituo hicho jana kilichopo manispaa ya  Shinyanga.
  UMMY, akiangalia kichanga kilicholazwa katika chumba maalumu cha uangalizi wa watoto mahututi na wale waliozaliwa kabla ya siku (njiti) katika Hospitali ya Rufaa ya Mkoa wa Shinyanga. Kushoto ni Daktari Bingwa wa watoto Dk. Mwita Ngutunyi.

No comments