Breaking News

TASAF TOENI HUDUMA NZURI KWA KAYA MASKINI ILI ZIJIKIMU KIMAISHA-DK. MARY.



 NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, akizungumza na watumishi wa Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF)  (hawapo pichani) wakati wa ziara yake ya kikazi alipowatembelea ofisini kwao Jijini Dar es Salaam  leo Januari 11, 2019. (Picha zote na Jamaes Mwanamyoto-UTUMISHI).                                 
                                Na Mary Mwakapenda

WATUMISHI wa Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) wametakiwa kuhakikisha wanufaika wa mpango wa kunusuru kaya maskini  wanahudumiwa vizuri kwa kupata ruzuku zao kwa wakati ili kuziwezesha kaya hizo kujikimu kimaisha na kuondokana na umaskini. 

Hayo yalisemwa leo Januari 11, 2019 Jijini Dar es Salaam na Naibu Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora, Dk. Mary Mwanjelwa, wakati akizungumza na watumishi wa TASAF Makao Makuu katika ziara yake ya kikazi yenye lengo la  kuhimiza uwajibikaji, kufahamu kwa kina majukumu ya TASAF na kujiridhisha namna inavyotekeleza wajibu wake.

Dk. Mary alisema, kwa kuwahudumia vizuri wanufaika hao, TASAF pamoja na Serikali itapata baraka za Mwenyezi Mungu ambaye kupitia vitabu vyake vitakatifu ameelekeza kuwasaidia maskini na pia watakuwa mfano bora wa kuigwa na nchini nyingine barani Afrika kwa kutekeleza vema mpango huo.

 MKURUGENZI Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga, akieleza  majukumu ya taasisi yake kwa Dk. Mry,  wakati wa kikao kazi cha Naibu Waziri huyo na watumishi wa TASAF kilichofanyika Makao Makuu ya TASAF. Kulia ni DK. Mary.


Dk. Mary, aliwataka watumishi wa TASAF kuwa tayari muda wote katika kuhakikisha kaya zote maskini  zinapata stahili  zao kwa wakati na kufurahia matunda na jitihada za Serikali ya Awamu ya Tano za kuziwezesha kaya maskini kuondokana na umaskini.

Aidha, Dk. Mary, aliitaka TASAF kuhakikisha inaweka taratibu madhubuti za kisheria zitakazo waadhibu na kuwadhibiti wote  watakaobainika kufanya udanganyifu kujipatia  fedha za mpango wakati hawana sifa za kuwa wanufaika.

Alisema, lengo ni kujenga nidhamu katika jamii ili fedha za mpango huo ziwafikie walengwa kama Rais Dk. John Magufuli, anavyotaka.


 BAADHI ya watumishi wa TASAF wakimsikiliza Naibu Waziri HUYO (hayupo pichani).


Katika kutekeleza azma hiyo, Dk. Mary, aliwataka watumishi wa TASAF kufanya kazi kwa ari na uzalendo mkubwa na kuipongeza TASAF kwa jitihada na mafanikio waliyoyapata katika kuzinusuru kaya maskini mpaka hivi sasa.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa TASAF, Ladislaus Mwamanga, amemhakikishia Dk. Mary, kuwa atahakikisha anasimamia vizuri utekelezaji wake wa kaya hizo kama alivyoelekeza.

Alisema, mpango huo utakuwa bora zaidi katika Bara la Afrika, na kuongeza kuwa, hadi sasa,  tayari umeonekana kuwa ni miongoni mwa mipango bora barani humoa kwani umeweza kuboresha maisha ya kaya maskini.

Mkurugenzi huyo alisema, utekelezaji wa mpango huo  umewezesha kuzitambua kaya maskini, umesimamiwa vizuri, malipo yanafanyika kwa wakati na hakuna ubadhilifu mkubwa wa fedha zilizotengwa kwa ajili ya wanufaika. 
  NAIBU Waziri, Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi wa Umma na Utawala Bora,  Dk. Mary Mwanjelwa, akiwa katika picha ya pamoja na Menejimenti ya Mfuko wa Maendeleo  ya Jamii (TASAF) mara  baada ya  kuzungumza na watumishi wa mfuko huo.

Akithibitisha ubora wa mpango, Mwamanga, alisema, hivi sasa Rais wa Benki ya Dunia katika utekelezaji wa majukumu yake ya kila siku, anapozungumzia programu za kupambana na umaskini, haachi kuutaja mpango wa kunusuru hizo unaotekelezwa nchini kuwa ni bora na unasimamiwa vizuri.

Serikali ya Awamu ya Tano, inayoongozwa na Rais, Dk. John Magufuli, aliyejipambanua kwa vitendo kuwajali wanyonge, imedhamiria kupitia mpango huo nchini, kuwafikia walengwa  katika kaya zote maskini nchini ili walengwa hao waweze kunufaika na kuboresha maisha yao.

No comments